JICHO LA MWEWE: Lamine kagundua tunaendesha ligi yetu kisela

Tuesday June 23 2020
Lamine pic

LAMINE Moro kaniacha hoi wiki iliyopita. Kasafari mwendo wa hatua 30 kutoka katika eneo lake la ulinzi na kwenda kumpiga teke kiungo staa wa JKT Tanzania, Mwinyi Kazimoto katika ugomvi ambao Kazimoto hakuhusika.

Mchezaji anayesafiri umbali wa hatua 30 kwenda kupiga teke kama la Lamine ni wazi kwamba amedhamiria. Sio kwamba alikumbwa na ghadhabu. Hapana. Ameenda kufanya usela tu. Hatua 30 zinakupa muda wa kutafakari ubaya wa kitu unachoenda kukifanya.

Angekuwa yuko pale pale sawa. Angekuwa ameenda kumpiga teke mtu ambaye alikuwa amemkanyaga mchezaji mwenzake, Patrick Sibomana tungeweza kukubali. Alienda kumkanyaga Kazimoto ambaye hakuwa amefanya lolote baya.

Wote tulibaki midomo wazi. Hata mashabiki wa timu yake Yanga walibaki midomo wazi. Kwanini alifanya vile? Jibu ni rahisi tu. Amegundua kuwa mpira wetu ni wa kisela. Unaweza kufanya unavyotaka na maisha yakasonga mbele.

Lamine katoka Afrika Magharibi. Anajua nini maana ya kuwa mchezaji wa kulipwa kuliko ambavyo wachezaji wetu wanajua. Ana rafiki zake wanacheza Ulaya. Anawatazama kila siku jinsi wanavyojizuia dhidi ya hasira za kijinga.

Bado naamini kwamba kama yeye mwenyewe angekuwa anacheza Borussia Dortmund au Marseille asingeweza kufanya upuuzi alioufanya. Angejizuia. Ndivyo wachezaji wa kulipwa walivyo. Tunawaona jinsi ambavyo wanaweza kuanzisha timbwili zito lakini wakaishia kusukumanasukumana tu. Hakuna anayerusha ngumi wala teke.

Advertisement

Lamine kafanya alichofanya kwa sababu amegundua kuwa mpira wetu unaendeshwa kisela. Wachezaji, hasa wa timu kubwa huwa wanafanya ubabe mwingi lakini huwa wanabebwa ama na waamuzi au vyombo vinavyosimamia mchezo wenyewe.

Kwa mfano, Lamine huyu huyu alimpiga mchezaji wa Mbeya City teke kule Mbeya lakini mpaka leo hakuna hatua aliyochukuliwa. Wiki chache baadaye katika pambano la raundi ya kwanza kati ya Simba na Yanga, Paschal Wawa alimkanyaga kwa makusudi Ditram Nchimbi lakini hakuna adhabu iliyochukuliwa.

Kabla ya hapo Clatous Chama aliwahi kumkanyaga Feisal Salum kwa makusudi. Sikumbuki kama kuna hatua iliyochukuliwa. Kama vile haitoshi, kuelekea pambano la marudiano la watani wa jadi, staa wa Yanga, Bernard Morisson pamoja na staa wa Simba, Jonas Mkude wote walipaswa kuliko pambano hilo kutokana na matukio ya utovu wa nidhamu waliyoonyesha kabla ya hapo.

Hata hivyo Kamati ya Saa 72 imegeuka kuwa Kamati ya miezi 72. Mpaka leo kimya. Nadhani wote katika kamati walikubaliana kwamba hakuna haja ya kuwafungia kina Morisson kwa sababu pambano lingekosa ladha.

Usishangae sana wajumbe watakuwa wamechanganyika kati ya Simba na Yanga. Ni wazi kwamba kila mmoja aliona kwamba mchezaji wake ni muhimu. Wakaafikiana ujinga wa kuwaruhusu wacheze. Hata hivyo kuanzia pambano lile mpaka sasa Mkude na Morisson bado wanatesa tu.

Maisha yakiwa hivi ligi inakosa nidhamu. Nawajua wachezaji wa SImba na Yanga ambao kama wangekuwa wanacheza katika timu ndogo basi kila wikiendi wangekuwa wanapewa kadi nyekundu. Hata hivyo tumetengeneza utamaduni wa kuwalinda.

Kwa hili la Lamine nadhani Yanga watajitetea kwamba mchezaji ameomba msamaha, kocha ameomba msamaha na klabu imeomba msamaha. Watajitetea kwamba Lamine ameadhibiwa kwa kukatwa mshahara wake. Shilingi milioni moja.

Usiamini kwamba Yanga wana dhati sana katika hili. Hapana. Anaweza akatokea mtu mmoja mwenyewe pesa zake akampatia Lamine Shilingi milioni moja ya kufidia pesa ambazo atakatwa. Huu ndio mpira wetu.

Usidhani kama ataumizwa sana na hiyo faini. Anajua jinsi gani ambavyo Yanga wanamtegemea. Anajua jinsi gani ambavyo walikwama na wakaenda kumrudisha kutoka kwao wakati waliposhindwa kumlipa mshahara kisha akaondoka.

Anajua kwamba kwa sasa yeye ndiye beki tegemeo zaidi. Ni wakati wake wa kufanya ujinga wowote ule na mashabiki na viongozi wakamezea. Kama angekuwa anasota benchi asingeweza kufanya ujinga ule. Kila nafasi anayopata angeitumia kwa ufasaha ilia pate mkataba mpya. Huu ndio ukweli.

Usishangae sana nitakapokukumbusha kwamba hata mchezaji mwenyewe ambaye alipigwa teke, Kazimoto, miaka miwili nyuma aliwahi kumpiga Mwandishi wa Habari wa gazeti hili, Mwanahiba Richard wakati huo akiwa mchezaji wa Simba.

Alidai kwamba mwandishi huyo alikuwa anamfuatilia sana katika mambo yake. Kuna mashabiki kibao wa Simba waliona alichofanya ni sawa tu. Kuna viongozi wengi wa Simba wakaamua kwenda upande wa Mwinyi. Mabosi wa Simba wakamtishatisha Mwanahiba, wakamlinda Mwinyi.

Huu ndio mpira wetu ambao Lamine ameugundua. Yanga walichofanya majuzi ni rahisi tu. Waligundua aibu ambayo ingewakumbuka. Kupunguza makali wakatoa ile barua ya kuomba msamaha kwa haraka zaidi. Sijawahi kuona kasi ya Yanga katika masuala haya lakini kwa mara ya kwanza niliiona mpaka kwenye mitandao ya kijamii.

Advertisement