David Luiz ndo kama ulivyosikia

LONDON ENGLAND. BEKI Mbrazili, David Luiz amesema amezungumza na bosi wa Benfica, Luiz Filipe Vieira juu ya mpango wa kurudi kukipiga kwenye klabu yake hiyo ya zamani msimu ujao.

Luiz anajiandaa kuachana na Arsenal ikiwa haijazidi hata miezi 12 tangu alipotua Emirates huku miamba hiyo ya London ikifikiria kumfungulia mlango wa kutokea wakati msimu huu utakapofika mwisho. Beki Luiz alisaini mkataba wa mwaka mmoja wakati anatua Arsenal huku kukiwa na makubaliano ya kuongeza miezi 12 mingine mwishoni mwa msimu wakati aliponaswa kwa ada ya Pauni 8 milioni akitokea Chelsea mwaka jana.

Amekuwa akipata namba muda wote msimu huu, kuanzia kwa kocha aliyeondoka Unai Emery, yule wa kipindi cha mpito Freddie Ljungberg na wa sasa Mikel Arteta, wote wamekuwa wakitegemea huduma ya beki huyo mwenye uzoefu mkubwa.

Luiz alicheza mechi 32 za michuano hiyo katika kikosi cha Arsenal na kufunga mabao mawili, lakini kocha Arteta anataka kupunguza bili ya mishahara kwenye kikosi chake pamoja na kuondoa wachezaji wenye umri mkubwa jambo litakalomfanya aondoke dirisha la usajili wa majira ya kiangazi litakapofunguliwa. Beki huyo wa zamani wa PSG aliichezea Benfica kwa miaka minne, ikiwa ni klabu yake ya kwanza Ulaya, kabla ya kuachana nayo Januari 2011, ambapo alinaswa na Chelsea na sasa amepanga kurudi Lisbon.

“Nilishazungumza na Vieira. Kila kitu kitatokea kama rais ataruhusu hili na mashabiki watataka nirudi,” alisema.