Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

JOBLESS: Makocha waliolipa kisogo benchi muda mrefu

ZIDANE Pict

Muktasari:

  • Hata hivyo, wapo makocha mashuhuri ambao kwa kutotaka au uamuzi binafsi wamechagua kusubiri, kupumzika au kutafakari upya safari ya kazi ya ukocha.

LONDON, ENGLAND: KATIKA soka la kisasa lenye presha kubwa ya matokeo na uharaka ni nadra kuona makocha wakubwa wakikaa nje na hawana kazi kwa muda mrefu.

Hata hivyo, wapo makocha mashuhuri ambao kwa kutotaka au uamuzi binafsi wamechagua kusubiri, kupumzika au kutafakari upya safari ya kazi ya ukocha.

Majina makubwa ya makocha kama Zinedine Zidane, Joachim Low, Jurgen Klopp, Xavi Hernandez na Gareth Southgate yanaendelea kutawala vichwa vya habari licha ya kutokuwa na timu wanazozinoa kwa sasa.

Makala hii inakuletea makocha wenye majina makubwa ambao hawana timu kwa muda mrefu na sababu ambazo zimewafanya wasifundishe kwa sasa.

ZIDA 01

ZINEDINE ZIDANE

Zinedine Zidane ni miongoni mwa makocha wenye majina makubwa wasiokuwa na kazi kwa muda mrefu sasa.

Kocha huyo Mfaransa tangu alipoondoka Real Madrid 2021 hajapewa kazi na timu yoyote licha ya kuhusishwa mara kwa mara na klabu kubwa kama Manchester United, Paris Saint-Germain na Chelsea.

Taarifa zimekuwa zikidai kuwa Zidane amekuwa akikataa ofa nyingi anazopelekewa akiamini katika kusubiri fursa maalumu hasa nafasi ya kuinoa timu ya taifa ya Ufaransa.

Alipata mafanikio makubwa akiwa Real Madrid, ikiwemo kutwaa Ligi ya Mabingwa Ulaya mara tatu mfululizo na hiyo inaonekana kuzipa tamaa timu nyingi ambazo zimekuwa zikitaka huduma yake.

ZIDA 02

JOACHIM LOW

Low alichana na timu ya taifa ya Ujerumani mwaka 2021 baada ya kuitumikia kwa miaka 15, akiisaidia kupata ubingwa wa Kombe la Dunia 2014.

Tangu wakati huo, Low hajarejea tena kwenye kazi ya ukocha, na amekuwa hasikiki hata kuhusishwa na timu za taifa au klabu.

Kocha huyu muda wake mwingi aliutumia kufundisha Ujerumani na mara ya mwisho kufundisha klabu ilikuwa mwaka 2004.

Baadhi ya ripoti zinadai kocha huyu ameamua kustaafu kimya kimya na hataki tena kurudi katika masuala ya ukocha kwani anaamini miaka 15 ya kuifundisha pamoja na miaka mingine ya kufundisha timu mbalimbali imetosha.

ZIDA 03

JURGEN KLOPP

Baada ya kuondoka Liverpool mwaka 2024, Jurgen Klopp alitangaza wazi kuwa anahitaji mapumziko kutoka kwenye kazi ya ukocha.

 Kocha huyo aliyetamba na falsafa yake ya  “gegenpressing† akianzia Borussia Dortmund na baadae Liverpool, aliondoka Anfield kwa kumaliza safari yenye mafanikio makubwa, ikiwemo kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya na Ligi Kuu England.

Tangu wakati huo kocha huyu alikaa nje kabla ya baadae kupata kazi kama mkuu wa masuala ya soka duniani wa kampuni ya Red Bull ambayo inasimamia timu mbalimbali ikiwemo RB Leipzig.

Hata hivyo, bado tetesi zimeendelea kumwandama kwamba anaweza akarejea kwenye ukocha na sasa anahusishwa sana na mpango wa kuchukua mikoba ya kuinoa Real Madrid.


ZIDA 04

XAVI HERNANDEZ

Xavi Hernandez aliacha nafasi yake kama kocha wa Barcelona mwishoni mwa msimu wa 2023/24, baada ya kuipa timu hiyo taji la La Liga na Spanish Super Cup.

Kocha huyo alifanya kazi katika kipindi kigumu ambacho klabu ilikuwa inakumbana na  changamoto za kifedha kiasi cha kushindwa kusajili wachezaji iliowahitaji.

Tangu aondoka kwenye viunga vya Nou Camp, hajaajiriwa sehemu nyingine yoyote ingawa hivi karibuni alitajwa kwamba huenda angetua Chelsea kabla ya timu hiyo kuachana na mpango huo, pia mara kwa mara Manchester United ambayo kwa sasa ina kocha wa muda Michaek Carrick imekuwa ikihusishwa naye.

ZIDA 05

GARETH SOUTHGATE

Gareth Southgate alijiuzulu rasmi kama kocha wa timu ya taifa ya England baada ya Euro 2024, akihitimisha kipindi cha takribani miaka nane akiwa kocha wa taifa hilo, tangu alipoteuliwa 2016.

Katika muda huo, Southgate aliiongoza England kwenye mafanikio kadhaa  ya kihistoria, akianzia kwa kuvunja ukame wa muda mrefu wa kufika hatua za juu katika mashindano makubwa ya kimataifa.

Chini ya uongozi wake, England ilifika nusu fainali ya Kombe la Dunia 2018, fainali ya Euro 2020 (iliyochezwa 2021), robo fainali ya Kombe la Dunia 2022, pamoja na fainali ya Euro 2024, mafanikio ambayo hayakuwa yamepatikana kwa miongo kadhaa kabla yake.

Southgate pia aliwapa nafasi wachezaji wengi vijana, akijenga kizazi kipya kilichojaa vipaji kama Jude Bellingham, Bukayo Saka, Phil Foden na Declan Rice.

Licha ya kukosolewa mara kwa mara kwa mtindo wake wa uchezaji unaoonekana wa kujilinda zaidi, takwimu zinaonyesha kuwa England ilikuwa miongoni mwa timu zenye matokeo mazuri zaidi barani Ulaya katika kipindi chake.

Tangu aachane na England, Southgate ameendelea kupumzika na licha ya kutajwa katika timu mbalimbali bado hakuna yoyote iliyofanikiwa kuipata huduma yake.