Zamalek yapewa pointi 3 Ahly ikigoma kutokea uwanjani

Muktasari:
- Al Ahly iligomea mechi hiyo na kuamua kutopeleka timu uwanjani kutokana na ishu ya waamuzi wa mchezo, ikidai inataka kipute hicho kichezeshwe na refa wa kigeni.
CAIRO, MISRI: ZAMALEK imepewa ushindi wa mezani wa pointi tatu na mabao 3-0 baada ya wapinzani wao na mahasimu wakubwa, Al Ahly kushindwa kutokea uwanjani katika mchezo wa Ligi Kuu ya Misri uliotarajiwa kufanyika usiku wa jana Jumanne Machi 11, 2025 kwenye wa Uwanja wa Kimataifa wa Cairo.
Al Ahly iligomea mechi hiyo na kuamua kutopeleka timu uwanjani kutokana na ishu ya waamuzi wa mchezo, ikidai inataka kipute hicho kichezeshwe na refa wa kigeni.
Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Misri, walisusia mchezo huo baada ya Chama cha Soka Misri (EFA) kupuuzia ombi la timu hiyo kuahirisha mechi ili ateuliwe mwamuzi wa kigeni.
Taarifa ya Al Ahly ilisomeka hivi: "Tunasisitiza kwa heshima ya Ligi ya Misri (EPL) uamuzi na uhitaji wa kucheza mechi yetu ya usiku (Jumanne) ichezeshwe na waamuzi wa kigeni. Kama matakwa yetu yatashindwa kuafikiwa, Ahly haitaendelea na ligi."
Katika kusisitiza mgomo wao huo, Ahly ilishindwa kutokea uwanjani, jambo lililomfanya mwamuzi Mahmoud Bassiouny kumaliza mpira baada ya dakika 15 kupita kutoka kwenye muda uliopaswa mechi hiyo kuanza, saa 3:30 usiku kwa saa za Misri.
Kwa uamuzi huo, Zamalek ilipewa ushindi wa mabao 3-0 na pointi tatu, zinazowafanya kufikisha 35 kwenye msimamo wa ligi, ikishika namba tatu, pointi nne nyuma ya Al Ahly iliyopo nafasi ya pili na pointi 39. Pyramids FC, ndiyo vinara wa ligi hiyo baada ya kukusanya pointi 42.
Madai ya Al Ahly kutaka waamuzi wa kigeni ni kwamba hairidhishwi na viwango vya waamuzi wa ndani, ambao wamekuwa na upendeleo kwenye mechi zao zilizopita. Hilo limeibuka usiku wa Jumatatu baada ya EFA kuteua waamuzi wazawa kuchezesha mechi hiyo, licha ya huko awali EPL kuahidi kwamba waamuzi wa kigeni wangetumika kwenye mechi muhimu za kuelekea mwisho wa msimu. Wakati Ahly ikigomea waamuzi wa ndani, Zamalek ilikuwa tayari kucheza bila kikwazo.
EFA ilijitetea kwamba haikuwa na muda wa kutosha kutafuta waamuzi wa kigeni. Mechi hiyo ilikuwa na umuhimu mkubwa kwenye mbio za ubingwa wa Misri, ambapo Ahly inayofukuzia ubingwa wake wa tatu mfululizo, ipo nyuma kwa pointi tatu na vinara Pyramids FC. Lakini, Pyramids ina mchezo mmoja mkononi, ambapo ikishinda inaweza kutanua pengo la pointi hilo kufikia sita.
Kwa mujibu wa kanuni za EPL za msimu huu, timu yoyote ambayo itashindwa kutokea uwanjani, itahesabika kama imegomea hivyo itakatwa pointi tatu. Kama timu itajitoa kwenye ligi baada ya kuanza, itakabiliwa kushushwa daraja na kufungiwa kucheza Ligi Kuu kwa misimu miwili pamoja na adhabu nyingine za faini za kifedha.
Baada ya kushindwa kupeleka timu uwanjani kwenye Derby ya Jiji la Cairo dhidi ya mahasimu wao Zamalek, klabu ya Al Ahly imetangaza kurudisha viingilio vya mashabiki waliokuwa wamenunua tiketi kwa ajili ya kushuhudia mtanange huo.
Taarifa ya Ahly imeeleza kuwa klabu hiyo inafanya mchakato wa kuwasiliana na kampuni inayohusika na ununuzi wa tiketi ndani ya saa chache zijazo ili kuweka utaratibu wa kurejesha fedha hizo kwa Mashabiki wote waliokuwa tayari wamenunua tiketi kwa ajili ya mchezo huo