Man United yajitosa dili la Jonathan Tah

Muktasari:
- Tah ambaye aliweka wazi hana mpango wa kusaini mkataba mpya wa kuendelea kusalia Leverkusen huduma yake pia inahitajika na Real Madrid.
MANCHESTER United imeingia vitani dhidi ya Bayern Munich ili kuipata huduma ya beki wa kati wa Bayer Leverkusen na timu ya taifa ya Ujerumani, Jonathan Tah ambaye mkataba wake wa unamalizika mwisho wa msimu huu.
Tah ambaye aliweka wazi hana mpango wa kusaini mkataba mpya wa kuendelea kusalia Leverkusen huduma yake pia inahitajika na Real Madrid.
Licha ya kuingia kwenye dili hilo, Madrid inaonekana kuwa na nafasi kubwa ya kumpata ikiwa watafanikisha mchakato wa kumwajiri Xabi Alonso kama kocha wao kwani Mhispania huyo ana ushawishi mkubwa kwa Tah.
Barcelona inamhitaji fundi huyu lakini changamoto kubwa ni hali yao ya kiuchumi na wanatakiwa kuuza kwanza wachezaji ili kuendana na sheria ya usawa wa matumizi ya pesa ya La Liga.
Bryan Mbeumo
NEWCASTLE United inatamani kumsajili mshambuliaji wa Brentford na timu ya taifa ya Cameroon, Bryan Mbeumo, 25, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi, lakini haipo tayari kutoa Pauni 60 milioni inayohitajika na timu yake ili kumruhusu. Mbeumo ni mmoja wa washambuliaji walioonyesha kiwango bora tangu kuanza kwa msimu huu na hiyo imesababisha vigogo wengi kutaka kumsajili. Liverpool na Arsenal ni miongoni mwa miamba ya Ulaya inayoitaka saini yake dirisha lijalo.
Evan Ndicka
ARSENAL huenda ikakutana na upinzani mkali kutoka kwa Paris St-Germain kwenye harakati zao za kuiwania saini ya beki kisiki wa AS Roma na timu ya taifa ya Ivory Coast, Evan Ndicka dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Roma ipo tayari kumuuza fundi huyu lakini kwa kiasi cha pesa ambacho hakitopungua Pauni 25 milioni. Newcastle na Liverpool zinatajwa pia kuiwania saini ya nyota huyu ambaye tangu atue Roma amecheza mechi 59 na hana bao hata moja ila ameonyesha kiwango bora.
Enzo Fernandez
CHELSEA haina mpango wa kumuuza kiungo wao raia wa Argentina, Enzo Fernandez katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi licha ya tetesi zinazodai fundi huyu anaweza kujiunga na Real Madrid iliyoanza kuinyatia huduma yake tangu dirisha la majira ya baridi mwaka huu. Enzo ambaye alisajiliwa kwa dau nono la Pauni 107, kwa sasa ana umri wa miaka 24.
Florian Wirtz
Bayer Leverkusen inajaribu kufanya mazungumzo na kiungo wao mshambuliaji na timu ya taifa ya Ujerumani, Florian Wirtz, 21, ili kumwongeza mkataba mpya dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Wirtz ambaye ni mmoja wa mastaa wanaohusishwa sana na Bayern Munich, Manchester City na Real Madrid, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika 2027. Msimu huu amecheza mechi 45 za michuano yote na kufunga mabao 15.
Andriy Lunin
REAL Madrid ipo tayari kumwachia kipa wao wa kimataifa wa Ukraine, Andriy Lunin, 26, aondoke dirisha lijalo majira ya kiagazi na imepanga kuziba nafasi yake kwa kumsajili kipa wa Chelsea na Hispania, Kepa Arrizabalaga, ambaye kwa sasa anacheza kwa mkopo Bournemouth. Lunin anataka kwenda kujiunga na timu itakayompa nafasi kubwa zaidi ya kucheza.
Kevin de Bruyne
ASTON Villa bado ina mpango wa kumsajili kiungo wa Manchester City, Kevin de Bruyne, 33, ambaye ataondoka mwisho wa msimu huu. De Bruyne ambaye anahusishwa na baadhi ya timu za Marekani na Saudi Arabia anadaiwa kuwa bado ana mpango wa kuendelea kucheza soka la kiushindani. Mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu.
Adam Wharton
CRYSTAL Palace inahitaji kiasi kisichopungua Pauni 80 milioni ili kimuuza kiungo wao raia wa England, Adam Wharton, 21, dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Timu nyingi zimeonyesha nia ya kutaka kumsajili fundi huyu ikiwamo Tottenham. Mkataba wa sasa wa Wharton unatarajiwa kumalizika 2029.