Wirtz asababisha kwa Man City, Bayern Munich

Muktasari:
- Inaelezwa awali, Man City ndio walionekana kuwa na nafasi kubwa ya kumsajili staa huyu ambaye wanamwangalia kama mbadala wa Kevin de Bruyne anayetarajiwa kuondoka mwisho wa msimu.
BAYERN Munich wanaamini wapo katika nafasi nzuri ya kuipuku Manchester City kwenye harakati za kuiwania saini ya kiungo mshambuliaji wa Bayer Leverkusen, Florian Wirtz ambaye amepewa ruhusa ya kuondoka mwisho wa msimu huu.
Inaelezwa awali, Man City ndio walionekana kuwa na nafasi kubwa ya kumsajili staa huyu ambaye wanamwangalia kama mbadala wa Kevin de Bruyne anayetarajiwa kuondoka mwisho wa msimu.
Hata hivyo, kuingia kwa Bayern kwenye dili hilo kumesababisha ugumu kwa Man City kwani wababe hao wa Ujerumani wanadaiwa kuweka ofa nono zaidi ya ile ambayo wao wameweka.
Mkataba wa sasa wa Wirtz unatarajiwa kumalizika mwaka 2027, na tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 42 za michuano yote na kufunga mabao 15 akiwa injini ya Bayer Leverkusen.
Georginio Rutter
CHELSEA wameanza mazungumzo na mshambuliaji wa Brighton, Mfaransa, Georginio Rutter ambaye inataka kumsajili katika dirisha la majira ya kiangazi.
Rutter ameingia kwenye rada za Chelsea baada ya msimu huu kuonyesha kiwango bora akicheza mechi 34 za michuano yote na kufunga mabao nane.
Caoimhin Kelleher
WEST Ham inataka kumsajili kipa wa Liverpool na wa Jamhuri ya Ireland, Caoimhin Kelleher, mwenye umri wa miaka 26, katika dirisha la majira ya kiangazi.
Kelleher anataka kuondoka Liverpool kwa sababu hapati nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza cha majogoo hao.
Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2026.
Xavi Simons
MANCHESTER United wanafikiria kumgeukia kiungo mshambuliaji wa RB Leipzig, Xavi Simons, 22, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi kama dili la kumsajili mshambuliaji wa Wolves na timu ya taifa ya Brazil, Matheus Cunha, 25, litashindikana.
Kocha wa mashetani wekundu, Ruben Amorim kipaumbele chake cha kwanza ni kumsajili Cunha ikishindikana ndio ahamie kwa Simons.
Antony
REAL Betis imetuma maombi ya kumsajili tena kwa mkopo wa msimu mzima, mshambuliaji wa Manchester United na timu ya taifa ya Brazil, Antony, 25, ambaye anacheza kwa mkopo katika kikosi chao kwa sasa.
Antony ambaye ni mmoja kati ya mastaa waliokuwa hawapati nafasi ya kutosha Man United, mkataba wake na timu hiyo ya Old Trafford unatarajiwa kumalizika mwaka 2027.
Rodrygo
MSHAMBULIAJI wa Real Madrid na timu ya taifa ya Brazil, Rodrygo, mwenye umri wa miaka 24, anafikiria kuondoka Real Madrid katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi baada ya kupoteza nafasi yake kwenye kikosi cha kwanza cha wababe hao kutoka Santiago Bernabeu.
Inaaminika kuwa staa huyu anataka kutimkia nchini England ambako kuna timu nyingi zilizoonyesha nia ya kumsajili.
Ederson
MANCHESTER United na Juventus wapo kwenye vita kali ya kuiwania saini ya kiungo wa kati wa kimataifa wa Brazil, Ederson mwenye umri wa miaka 25 kutoka Atalanta.
Ederson ambaye msimu huu amecheza mechi 45 za michuano yote na kufunga mabao matano, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2027.
Emiliano Martinez
KIPA wa Aston Villa na Argentina, Emiliano Martinez, 32, pamoja na winga wao raia wa Jamaica Leon Bailey mwenye miaka 27,wapo katika rada za matajiri wa Saudi Arabia wanaohitaji kuwasajili katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Bailey na Martinez ni miongoni mwa wachezaji tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Aston Villa.