Wilder amtaka Usyk kibabe ulingoni

DEONTAY Wilder, bondia mkali kwenye ngumi za uzito wa juu duniani (heavyweight) amemchana bingwa wa mikanda mitatu ya uzito huo, Oleksandr Usyk kwamba aache kumuogopa na wazipige ulingoni.

Wilder aliyewahi kushikilia mkanda wa WBC kwa zaidi ya miaka mitano kabla ya kupigwa mara mbili na Tyson Fury katika mara tatu walizopigana, amedai bondia huyo kutoka Ukraine mwenye mikanda ya WBO, IBF na WBA anahofia kucheza naye.

Usyk mara ya mwisho alimshinda Mwingereza Anthony Joshua kwa pointi za majaji wote watatu kwenye mapambano mawili waliyopigana ambapo hivi karibuni amekuwa na matarajio ya kupigana na Fury kuwania mikanda minne ya uzito huo.

Hata hivyo, Wilder hataki kusikia kuhusu pambano lake Usyk na Fury kama lipo au la, bali anachotaka ni bondia huyo akubali changamoto ya kupanda ulingoni dhidi yake na sio kushikilia mikanda ambayo anahofia kuitetea na kuchagua mpinzani.