Wikiendi ya ukubwa Italia

Muktasari:

  • Mechi kubwa ya kwanza itazikutanisha AC Milan na Juventus ambapo kama Milan itashinda itaendelea kusalia katika nafasi yake ya pili lakini hata ikifungwa pia itabaki hapo hapo ingawa pengo la alama litazidi kupungua.

ROME, ITALIA: Baada ya Inter Milan kutangaza ubingwa, Ligi Kuu Italia itaendelea tena wikiendi hii ambapo kutakuwa na mechi kubwa mbili pamoja na mechi zitakazokuwa zinashikilia hatma ya baadhi ya timu kubaki katika ligi ama kushuka daraja.

Mechi kubwa ya kwanza itazikutanisha AC Milan na Juventus ambapo kama Milan itashinda itaendelea kusalia katika nafasi yake ya pili lakini hata ikifungwa pia itabaki hapo hapo ingawa pengo la alama litazidi kupungua.

Juventus inayoshika nafasi ya tatu kwa nsasa ina pointi 64 huku Milan ina pointi 69 zote zikiwa zimecheza mechi 33.

Mchezo uliopita baina ya timu hizi Milan ikiwa katika uwanja wake wa nyumbani ilipoteza kwa bao 1-0, hivyo itakuwa inataka kulipiza kisasi.

Mechi nyingine kubwa itawakutanisha mabingwa wa msimu uliopita wa ligi hii Napoli wataoumana na AS Roma ambapo timu zote zinapambana ili kufuzu ushiriki wa michuano ya kimataifa.

Napoli iliyo nafasi ya nane kwa pointi 49 inataka walau kufuzu michuano ya Uefa Conference League kwa kumaliza katika nafasi ya sita wakati Roma iliyopo nafasi ya tano kwa pointi 58 inapambana kuishusha Bologna kwenye nafasi ya nne ili ifuzu Ligi ya Mabingwa msimu ujao.

Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza kati ya timu hizi mbili ulimalizika kwa Roma kufuta unyonge wa muda mrefu wa kutoshinda mechi yoyote katika mechi saba mfululizo. Katika mechi hii ilishinda mabao 2-0.

Leo ni Verona pekee ndio itakuwa inajitetea kuondoka kabisa kwenye janga la kushuka daraja ambapo itatakiwa kushinda mchezo wao dhidi ya Lazio na kupanda walau nafasi ya 14.

Lakini kesho ndio kuna shughuli zaidi kwani Sassuolo, Udinese, Empoli na Frosinone zilizopo kuanzia nafasi ya 18 hadi 16 ndio zitakuwa dimbani kujitetea.

Kati ya timu hizi tano ukizijumuisha na Verona, mbili ni lazima zishuke na mbili zibaki na hadi sasa utofauti wa alama kati yao ni mdogo sana, kuna zinazopishana alama mbili na nyingine tatu.

Yeyote atakayepoteza mechi anaweza kujikuta katika mstari mwekundu wa kushuka daraja.