Wikiendi ya moto! Man City VS Man United… Arsenal, Liverpool mzigoni
Muktasari:
- Ushindi ni muhimu kwa pande zote mbili, mmoja ukijaribu kurejea kwenye ubora wake, wakati mwingine ukiendelea kujitafuta kwa wachezaji wake kuzoea mbinu na mfumo wa kocha mpya. Kazi ipo.
LONDON, ENGLAND: NI wikiendi ya Manchester derby. Kikosi cha Pep Guardiola kilichopoteza makali yake, Manchester City kitakuwa nyumbani Etihad kukabiliana na mahasimu wao Manchester United, ambao kwa sasa wanajitafuta chini ya kocha wao mpya, Ruben Amorim. Shughuli yenyewe ni kesho, Jumapili.
Ushindi ni muhimu kwa pande zote mbili, mmoja ukijaribu kurejea kwenye ubora wake, wakati mwingine ukiendelea kujitafuta kwa wachezaji wake kuzoea mbinu na mfumo wa kocha mpya. Kazi ipo.
Tangu Sir Alex Ferguson alipostaafu, Man City imetawala karibu katika kila idara; uwanjani, wafanyakazi wake na hata kwenye usajili. Man United imetumia pesa nyingi sana kusajili wachezaji wapya, ambao wameshindwa kuirudisha kwenye ubora, wakati mahasimu zao hao, waliowaita majirani wenye kelele, mambo yao ya uwanjani yamekuwa mazuri na kuonekana pesa wanayotumia kwenye usajili inalipa kutokana na mafanikio wanayopata.
Kesho patawaka moto. Mechi tano za mwisho miamba hiyo ilipokutana kwenye Ligi Kuu England, Man City imeshinda nne na imefunga mabao 17 katika mechi hizo. Man United imeshinda mechi moja tu, huku ikifunga mabao saba katika mechi hizo. Amorim atabadili hali ya mambo baada ya kutua Old Trafford?
Namba zinasoma kwamba, Man City na Man United zimekutana mara 54 kwenye Ligi Kuu England. Hii ni mechi yao ya 55. Lakini, kwenye mechi hizo zilizopita, sare ni tisa - Man City imeshinda 20, mara 11 nyumbani na tisa ugenini, huku Man United ikishinda 25, mara 12 nyumbani na 13 kwenye uwanja wa ugenini. Hii ina maana, Man United imeshinda mara nyingi kwenye uwanja wa Man City kuliko wao wenyewe kwenye Manchester derby.
Ukiweka kando kipute hicho cha Manchester derby kwa kesho, kutakuwa na mechi nyingine tatu, ambapo Brighton watajimwaga kwenye uwanja wao nyumbani kucheza na Crystal Palace, wakati Chelsea itakuwa Stamford Bridge kucheza na Brentford na Southampton watakuwa na kasheshe zito dhidi ya Tottenham Hotspur.
Kwa Chelsea na Brentford hiyo ni mechi ya saba kwa miamba hiyo kukutana kwenye Ligi Kuu England, lakini mechi hizo The Blues ni vibonde, ambapo kwenye mechi sita zilizopita, sare ni mbili, huku Chelsea ikishinda moja tu, ilipocheza ugenini, wakati Brentford ikishinda tatu na zenyewe pia ilishinda ugenini. Utamu wa mechi ya Chelsea na Brentford hakuna timu iliyoshinda nyumbani kwenye mechi za Ligi Kuu England zilipokutana zenyewe. Je, safari hii itakuwaje?
Southampton na Spurs shughuli yao ya huko St. Mary’s zitakutana kwa mara ya 49 kwenye Ligi Kuu England, ambapo kwenye 48 zilizopita, Soton imeshinda 14, mara 10 nyumbani na nne ugenini, huku Spurs ikishinda 25, mechi 18 kwenye uwanja wao wa nyumbani na saba ugenini, huku mara tisa timu hizo zilitoshana nguvu.
Wapinzani kwenye mbio za ubingwa wa ligi hiyo, Arsenal na Liverpool zitakuwa mzigoni pia. Chama la Mikel Arteta, Arsenal litakuwa nyumbani kukipiga na Everton, wakati Liverpool ya Arne Slot itakuwa Anfield kumalizana na Fulham. Mechi hizo zote ni muda mmoja.
Arsenal na Everton zimekutana mara 64 kwenye Ligi Kuu England, huku The Gunners imeshinda 38, mara 25 ikiwa nyumbani na 13 ugenini, wakati Everton imeshinda 12, mara 10 nyumbani na mbili ugenini, huku mechi 14 baina yao zilimalizika kwa sare. Safari hii itakuwaje?
Vinara, Liverpool na Fulham hii ni mechi yao ya 35 kwenye Ligi Kuu England, ambapo mara 34 zilizopita, Fulham ilishinda saba tu, mara tano nyumbani na mbili ugenini. Wakati mechi sita zikimalizika kwa sare, Liverpool imeshinda 21, mara 11 nyumbani na 10 ugenini.
Mechi nyingine za leo, Newcastle itacheza na Leicester, St James’ Park.