Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nyota wa Serengeti Boys asiyetembea amtaja Msuva, Samatta

STAR Pict

Muktasari:

  • Baada ya kupitia safari ndefu ya kutafuta tiba kwa miaka kadhaa, Lipston anamuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan pamoja na wadau wengine wenye uwezo kumsaidia katika matibabu yake.

“Tulianza kutafuta msaada kila sehemu. Tulitembea maeneo mengi sana, tukaambiwa jaribu hiki, jaribu kile. Hakuna kitu tulichopuuzia kwa sababu tulikuwa tunatafuta suluhisho,” anasema.

SASA ENDELEA...

Katika safari hiyo, walijaribu njia mbalimbali za matibabu, ikiwemo tiba za asili ambazo watu wengi waliziamini zinaweza kumsaidia.


HOSPITALI WALICHOGUNDUA

“Miongoni mwa hospitali nilizofika kwa ajili ya kufanyiwa vipimo ni pamoja na Muhimbili jijini Dar es Salaam. Nilifanyiwa vipimo mbalimbali, lakini majibu yalionyesha kwamba hakukuwa na tatizo kubwa lililoonekana,” anasimulia Lipston.

“Ndipo nilipoanza kujiuliza maswali mengi, kwa sababu ndani ya mwili wangu nilikuwa nahisi kuna kitu kimebadilika. Nilikuwa naona hali yangu si ya kawaida, lakini vipimo havikuonyesha tatizo ambalo lingeweza kueleza kile nilichokuwa napitia.”

Lipston anasema kilichomuumiza zaidi ni kuona mabadiliko makubwa yakitokea katika maisha yake kwa muda mfupi, kutoka kuwa kijana mwenye ndoto hadi kushindwa kufanya hata mambo ya kawaida aliyokuwa akiyafanya kila siku.

“Nilitoka kwenye hali ya kutembea mwenyewe, kufanya shughuli zangu na kuishi kama watu wengine, lakini sasa imefika wakati siwezi kufanya chochote. Siwezi kutembea tena, muda mwingi nimekuwa mtu wa kulala na nahitaji msaada wa kufanya karibu kila kitu,” anasema kwa masikitiko.

STA 01

AMUANGUKIA RAIS SAMIA

Baada ya kupitia safari ndefu ya kutafuta tiba kwa miaka kadhaa, Lipston anamuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan pamoja na wadau wengine wenye uwezo kumsaidia katika matibabu yake.

Anasema yeye pamoja na familia yake wamepambana kwa muda mrefu kutafuta suluhisho la changamoto anayopitia, wakifika hospitali mbalimbali na kujaribu njia tofauti za matibabu, lakini uwezo wao wa kifedha umefikia ukomo.

“Familia yangu imepambana sana. Tumefanya kila tulichoweza, tumekwenda hospitali mbalimbali, lakini sasa tumefika mwisho wa uwezo wetu. Tunahitaji msaada ili niweze kupata matibabu na mazoezi yatakayosaidia kurejesha nguvu za mwili,” anasema Lipston.

Anasema pamoja na hali anayopitia ya kushindwa kutembea na kutegemea msaada wa watu wengine katika baadhi ya shughuli za kila siku, bado hajakata tamaa na anaamini ipo nafasi ya kubadilika endapo atapata matibabu sahihi.

Kwa sasa, ndoto yake kubwa si tena kuhusu kurudi uwanjani, bali ni kupata uwezo wa kusimama, kutembea na kuweza kufanya shughuli zake mwenyewe kama ilivyokuwa kabla ya changamoto hiyo.

MLA 04

MSIKIE BABA YAKE

Baba yake, Elibi Juma Mlagulwa, anakumbuka namna alivyogundua kipaji cha mwanaye akiwa bado mdogo. Anasema tangu akiwa shule ya msingi na baadaye sekondari, Lipston alikuwa tofauti na vijana wengine kutokana na uwezo wake mkubwa ndani ya uwanja.

“Alikuwa na kipaji kikubwa sana. Huyu alikuwa anacheza namba nane. Tangu akiwa mdogo watu walikuwa wanamjua hapa Mpwapwa kwamba anajua kucheza mpira. Hata wenzake walikuwa wanajua kabisa kuwa huyu mtoto ana kitu cha ziada,” anasema baba yake.

Anasema Lipston hakuanza safari yake ya soka akiwa na umaarufu mkubwa, bali alipambana kupitia hatua mbalimbali akitafuta nafasi ya kuonyesha uwezo wake. Baada ya kumaliza shule, alikwenda Mbeya, baadaye Zanzibar na hatimaye Mwanza ambako alijiunga na Mbao FC.

“Alitembea sehemu nyingi kidogo kutafuta maisha ya mpira. Alikuwa na ndoto kubwa sana. Mimi kama mzazi nilikuwa namuunga mkono kwa sababu niliona uwezo wake na nilijua anaweza kufika mbali,” anasema.

Kwa baba yake, moja ya mambo yaliyompa matumaini zaidi ni namna watu mbalimbali walivyokuwa wakimsifia mwanaye kila alipokuwa akicheza. Anasema kuna wakati aliamua kwenda mwenyewe kumuangalia uwanjani baada ya kusikia sifa nyingi kuhusu kipaji chake.

“Watu walikuwa wananiambia mtoto wako anacheza mpira sana. Nikawa najiuliza kweli huyu mtoto anaweza kiasi gani? Nilipoenda kumuona nikasema huyu ana kitu. Hata ndugu zake walikuwa wanajua uwezo wake,” anasema.

Anasema kwa wakati huo hakuwahi kufikiria kuwa siku moja angeona mwanaye akiwa katika hali ya kushindwa kufanya mambo ya kawaida. Badala yake, alikuwa na matumaini kuwa Lipston ndiye angekuwa sehemu ya kuondoa changamoto za maisha ya familia.

“Mimi nilijua huyu mtoto ndiye angenitoa kwenye shida. Niliona ana uwezo wa kucheza mpira, niliona watu wanamkubali. Nilikuwa na matumaini makubwa sana kwake,” anasema.

Anasema familia ilianza safari ndefu ya kutafuta tiba, wakimpeleka katika hospitali mbalimbali, lakini hawakupata majibu yaliyoweza kueleza kwa nini kijana wao aliyekuwa na afya njema alipoteza nguvu za mwili.

“Tulijaribu sehemu mbalimbali. Hata Muhimbili tulimpeleka, akapimwa zaidi ya mara moja. Waliangalia mifupa yake, wakasema iko vizuri. Lakini bado hali yake ilikuwa inaendelea kubadilika,” anasema.

Kwa sasa, anasema changamoto kubwa ya Lipston si tatizo la akili wala kumbukumbu, bali ni kupotea kwa nguvu za mwili ambazo zimemfanya ashindwe kujitegemea katika shughuli nyingi za kila siku.

“Kichwani yuko vizuri kabisa. Kila kitu anakumbuka. Tatizo ni nguvu tu zimeisha mwilini. Hata ukimuona mgongo wake unaonekana uko sawa, lakini mwili hauna nguvu,” anasema.

Anaeleza kuwa kwa sasa mwanaye anahitaji msaada hata katika mambo ya msingi kama kula, kuoga na kujihudumia, lakini bado ana uwezo wa kuwasiliana na kuelewa kila kitu kinachoendelea.

“Chakula anakula vizuri, lakini mpaka umlishe. Kuoga hawezi mwenyewe. Tunachotaka ni apate nguvu zake zirudi, hata kama si kwa ajili ya mpira tena, kikubwa aweze kusimama na kuishi maisha yake,” anasema.

Elibi anasema familia haijakata tamaa na bado inaamini kuna uwezekano wa Lipston kupata nafuu endapo atapata msaada wa wataalamu na mazoezi maalumu ya kurejesha nguvu za mwili.

“Wadau wakisaidia apate matibabu au sehemu ya kufanya mazoezi, tunaamini anaweza kubadilika. Tunachotaka ni kuona mtoto wetu anarudi kuwa na uwezo wa kufanya mambo yake mwe nyewe,” anasema.

MLA 03

MACHOZI YAMTOKA MAMA

Mama yake, Foibe Eliabi Mlagulwa, safari ya miaka mitano ya kumuuguza mwanaye imekuwa na maumivu makubwa kwa mzazi. Anasema aliumia sana kuona mtoto aliyemlea tangu utotoni akibadilika ghafla kutokana na changamoto hiyo.

“Hii shida amekuwa nayo muda mrefu, karibu miaka mitano sasa. Tumehangaika sana, tumejaribu sehemu mbalimbali, lakini mpaka leo bado tunapambana. Tunamshukuru Mungu kwa sababu bado anaendelea vizuri,” anasema.

Mama huyo anasema jambo lililobaki kwa sasa ni kupata msaada utakaomwezesha Lipston kupata tiba au mazoezi maalumu ya kumrudishia nguvu.

“Tunawaomba wadau wajitokeze wamsaidie. Sisi wazazi tumeshafika mwisho wa uwezo wetu. Tumehangaika sana, tumekimbia sehemu nyingi, lakini sasa tunahitaji msaada,” anasema.

Anasema kilichomuuma zaidi kama mzazi ni kuona kijana aliyekuwa na ndoto kubwa za soka akipitia hali hiyo akiwa bado mdogo.

“Niliumia sana. Nimemlea vizuri, amesoma mpaka kidato cha sita, nilikuwa na matumaini makubwa kwake. Nilijua huyu ndiye angekuja kunisaidia katika maisha. Lakini pamoja na yote yaliyotokea, bado namshukuru Mungu.”

Pamoja na maumivu hayo, Foibe anasema bado hajapoteza matumaini na anaamini siku moja mwanaye anaweza kusimama tena.

MLA 01

DAKTARI ATIA NENO

Kwa mtazamo wa kitabibu, hali anayopitia Lipston ya kushindwa kutembea baada ya awali kuwa na uwezo wa kufanya shughuli za kawaida inaweza kusababishwa na sababu mbalimbali zinazohusisha mfumo wa fahamu, misuli, uti wa mgongo au matatizo mengine yanayoathiri mawasiliano kati ya ubongo na mwili.

Daktari Shadrack Faustine ambaye aliwahi kufanya kazi katika Hospitali ya KCMC wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro, kwa sasa ni mbobezi wa mifupa anayendelee na masomo huko Ujerumani, amefanya tathmini ya awali, ikiwemo jinsi tatizo lilivyoanza, kama lilikuja ghafla au taratibu, kama kulikuwa na maumivu, jeraha, homa, kupungua nguvu za misuli au mabadiliko mengine ya mwili.

“Mgonjwa anayefika hatua ya kupoteza uwezo wa kutembea hatakiwi kuangaliwa kwa jicho moja pekee. Tunahitaji kujua chanzo halisi cha tatizo kwa sababu kushindwa kutembea kunaweza kutokana na matatizo tofauti kabisa,” anasema daktari huyo.

Kwa hali kama hii, vipimo vya awali vinaweza kuhusisha uchunguzi wa nguvu za misuli, mfumo wa fahamu, mwenendo wa mishipa ya fahamu pamoja na vipimo vya picha kama MRI au CT Scan endapo daktari ataona kuna uwezekano wa tatizo kwenye uti wa mgongo au ubongo.

“Wakati mwingine vipimo vya kawaida vinaweza kuonyesha hakuna tatizo kubwa, lakini bado mgonjwa akawa anaendelea kupata changamoto. Ndiyo maana ni muhimu kufanya uchunguzi wa kina zaidi unaolenga eneo linalosababisha dalili,” anaeleza.

Miongoni mwa sababu zinazoweza kuangaliwa ni pamoja na matatizo ya mishipa ya fahamu, maambukizi yanayoathiri mfumo wa fahamu, matatizo ya uti wa mgongo, upungufu wa baadhi ya virutubisho mwilini au matatizo yanayoathiri misuli.

Daktari huyo anasema tiba hutegemea kabisa chanzo kitakachobainika baada ya uchunguzi. Ikiwa tatizo linatokana na mishipa ya fahamu, mgonjwa anaweza kuhitaji dawa maalumu, mazoezi ya tiba (physiotherapy) na uangalizi wa karibu wa wataalamu. Kwa Lipston, hatua muhimu sasa ni kupata tathmini pana kutoka kwa wataalamu mbalimbali wakiwemo madaktari wa mfumo wa fahamu, mifupa na wataalamu wa tiba mazoezi ili kupata picha kamili ya tatizo lake.

MLA 06

AKUMBUKA SAFARI YA MOROCCO

Kabla ya maisha yake kubadilika na kumweka kwenye changamoto ya kushindwa kutembea, Lipston alikuwa miongoni mwa vijana waliokuwa wakipewa nafasi ya kuonyesha uwezo wao kwenye ngazi ya timu za taifa za vijana.

Akiwa katika kikosi cha Taifa Stars U17, Lipston anakumbuka kipindi hicho kama moja ya hatua muhimu katika safari yake ya soka, akitaja baadhi ya wachezaji aliokuwa nao ambao baadaye wameendelea kufanya vizuri kwenye soka la ushindani.

Miongoni mwao ni Ladack Chasambi ambaye kwa sasa ni mmoja wa wachezaji wanaotambulika akiwa na Simba, huku Lipston akiamini kizazi hicho kilikuwa na vipaji vingi vilivyokuwa na matumaini makubwa.

Anakumbuka pia safari ya Morocco ambayo ilikuwa sehemu ya maandalizi ya timu hiyo, lakini mipango yao ikavurugwa na janga la corona lililokuwa limeikumba dunia. “Nakumbuka tuliishia kucheza mechi moja tu ya kirafiki dhidi ya Uganda, lakini haikumalizika vizuri kwa sababu ilikatishwa kutokana na kisa cha corona. Baada ya hapo ilibidi turudi nyumbani, lakini kwangu ilikuwa ni uzoefu mkubwa sana,” anasema.

STA 03

AMTAJA MSUVA, SAMATTA

Katika safari yake ya soka, Lipston anasema alikuwa akipata hamasa kutoka kwa wachezaji waliotangulia na kufanikiwa kuvuka mipaka ya Tanzania.

Anawataja Mbwana Samatta na Simon Msuva kama baadhi ya wachezaji ambao wamekuwa mfano kwake kutokana na juhudi zao, nidhamu na uwezo wa kupambana hadi kufikia hatua ya kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.

“Samatta na Msuva ni wachezaji ambao nimekuwa nikivutiwa nao sana. Wameonyesha kuwa mchezaji Mtanzania anaweza kufika mbali kama akiwa na malengo, kujituma na kuwa na nidhamu katika kazi yake,” anasema.

STA 02

FEI TOTO ANAMKUBALI

Katika wachezaji wanaocheza nafasi iliyokuwa akicheza kiungo wa kati, Lipston anasema alikuwa akimfuatilia zaidi Feisa Salum ‘Fei Toto’ na kuna baadhi ya mashabiki walikuwa wakimwita jina hilo.

Anasema kilichokuwa kikimvutia kwa Feisal ni uwezo wake wa kufanya maamuzi ndani ya uwanja, ubunifu na namna anavyoweza kubadilisha mchezo.

“Feisal ni mchezaji ambaye nampenda sana. Ana uwezo mkubwa wa kushika mpira, kutoa pasi na kutengeneza nafasi. Namwona kama mmoja wa wachezaji wanaoweza kuendelea kuiwakilisha Tanzania vizuri,” anasema Lipston.