West Ham waimezea mate Ligi ya Mabingwa

LONDON, ENGLAND. MSHAMBULIAJI wa West Ham, Michail Antonio amesema hawawezi kukata tamaa kwenye mapambano ya kupigania nafasi ya kushiriki ya kushiriki msimu ujao kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kutupia mabao mawili dhidi ya Burnley.

Wagonga nyundo  wa London, wamesogea hadi nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, wapo nyuma ya Chelsea kwa pointi tatu huku ikiwa imesalia michezo minne kabla ya msimu kumalizika.

Burnley  ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao kwenye mchezo huo dakika ya 19  kupitia kwa Chris Wood  aliyefunga kwa mkwaju wa penalti, West Ham walisawazisha kichwa  dakika ya 21 kupitia kwa Antonio kufuatia krosi iliyonyunyizwa na Vladimir Coufal.

Dakika nane baadaye Antonio akapiga msumari wa pili na ushindi kwa West Ham.

Antonio, ambaye amerejea kikosini baada ya kuwa nje ya uwanja kwa wiki nne akiuguza majeruhi, alisema, "Itakuwa jambo kubwa kwetu,"

"Kila mtu anataka kucheza kwenye Ligi ya Mabingwa. Nimekuwa hapa miaka michache na kumekuwa na misimu mingi sana ambayo tulikuwa tukipigania ikiwemo kukaa  kwenye ligi na sasa tunayo nafasi ya kumaliza kwenye nne  bora,"

"Hatuwezi kukata tamaa kwenye hili. Tutaendelea kupambana hadi mwisho."

Upande wake kocha wa West Ham, David Moyes alisema,"Tunatakiwa kufanya vizuri kwenye michezo yetu  minne iliyosalia. Kucheza mashindano ya Ulaya kiukweli   yatakuwa mafanikio makubwa kwetu."