Dili la Sesko Arsenal lilipokwama!

Muktasari:
- Mikel Arteta alikuwa akiwafukuzia mastraika wote hao wawili dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi, akijaribu kuandaa kikosi chake cha Arsenal kuwa tishio msimu ujao.
MUNICH, UJERUMANI: ARSENAL iliamua kurudi kwenye mazungumzo ya kumchukua straika Viktor Gyokeres baada ya kukwama kwenye makubaliano ya ada ya mkali, Benjamin Sesko, imefichuka.
Mikel Arteta alikuwa akiwafukuzia mastraika wote hao wawili dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi, akijaribu kuandaa kikosi chake cha Arsenal kuwa tishio msimu ujao.
Kwa muda wote wa dirisha hili la usajili, Arsenal ilikuwa imeweka nguvu kwa mastraika hao wawili, ikihitaji mmoja aende akaongoze safu yao ya ushambuliaji huko Emirates.
Lakini, kwa sasa kinachoonekana staa wa Sporting Lisbon, Gyokeres, ndiye atakayekwenda kuongoza safu hiyo ya ushambuliaji ya miamba ya Emirates. Arsenal imefika kwenye hatua nzuri kwenye usajili wa Gyokeres, huku mchezaji mwenyewe akipambana kusukuma dili hilo lifanikiwa.
Hilo limefanya dili la Sesko kwenda Emirates kushindikana. Ripoti zinafichua, bosi wa usajili wa Arsenal, Andrea Berta aliamua kuachana na dili la kumchukua Sesko baada ya klabu yake ya RB Leipzig kuhitaji walipwe Euro 100 milioni ili kukamilisha dili hilo.
Arsenal yenyewe iliripotiwa kupungiwa Euro 10 milioni, pia utaratibu wa malipo ambao Leipzig ilitaka ilipwe hizo pesa ulikuwa mgumu kwa Arsenal na kuamua kukimbilia kwa Gyokeres.
Wakati huo huo, ishu ya makubaliano binafsi na straika huyo yalionekana kuwa ni tatizo pia, kitu kilichowalazimisha Arsenal kujiweka kando. Lakini, wakala wa Sesko, Elvis Basanovic amefunguka wakati alipoulizwa juu ya ishu ya Arsenal kutaka mastraika wawili kwa wakati mmoja.
Wakala huyo alisema anadhani Sesko angekuwa chaguo bora zaidi kwa Arsenal, huku akimpiga kijembe Gyokeres kwa kulazimisha kuondoka Sporting Lisbon ili tu kuwapa urahisi The Gunners.
Basanovic alisema: “Ngoja niwaambie: Sesko hashindani na yeyote. Ni yeye dhidi ya yeye siku zote. Tuna mpango wa wazi kabisa kuhusu hatima yake na huu uvumi wa vyombo vya habari hautusumbui. Sesko si straika tu, bali ni straika spesho.”
Aliongeza: “Hata kama itakuwa au kwa mchezaji kuwa na malengo fulani ya kuhama, hatuwezi kulazimisha au kuirubuni RB Leipzig. Naamini hiyo sio njia sahihi, kwa sababu kwa namna unavyoka kwenye klabu ndivyo watu wanavyokuthaminisha. Hivyo, ndivyo utakavyokwenda kuthaminishwa kwenye klabu yake mpya.”
Bila kujali ni straika gani Arsenal itamsajili, kocha Arteta anahitaji jambo hilo likamilishwe haraka. Anataka straika mpya asajiliwe kabla ya Arsenal haijapanda ndege kwenda Singapore kwenye ziara ya pre-season huko Asia, Julai 19.