Wenger atatia tiki usajili wa Benzema

Muktasari:
- Arsenal ipo sokoni kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi kusaka straika mpya kwa sababu Kai Havertz hafungi mabao na Gabriel Jesus ni majeruhi, ambaye anatazamiwa kuwa nje ya uwanja hadi mwisho wa msimu baada ya kuumia misuli ya goti kwenye mechi dhidi ya Manchester United.
PARIS, UFARANSA: ARSENE Wenger anatazamiwa kuwa shabiki wa kwanza kwenye mpango wa Arsenal wa kufanya usajili wa fowadi supastaa, Karim Benzema.
Arsenal ipo sokoni kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi kusaka straika mpya kwa sababu Kai Havertz hafungi mabao na Gabriel Jesus ni majeruhi, ambaye anatazamiwa kuwa nje ya uwanja hadi mwisho wa msimu baada ya kuumia misuli ya goti kwenye mechi dhidi ya Manchester United.
Kutokana na kocha Mikel Arteta kuhitaji kuwa na kikosi chenye ushindani kwenye mbio za ubingwa, straika mpya sasa anahitajika kwa nguvu zote.
Alexander Isak alitarajiwa kuwa kwenye rada zao kwa muda mrefu, lakini timu yake ya Newcastle United haitakuwa tayari kumuuza kwenye dirisha hili.
Hiyo ina maana, kutafuta mbadala litakuwa chaguo sahihi kama kweli Arteta atahitaji kufanya kweli kwenye ligi msimu huu.
Gwiji wa Manchester United, Rio Ferdinand ameibuka na kuishauri Arsenal akiamini Benzema, ambaye kwa sasa anacheza huko Saudi Pro League katika kikosi cha Al-Ittihad, anaweza kuwa mtu sahihi wa kuifanya Arsenal kuwa na safu matata ya ushambuliaji.
Ferdinand aliambia TNT Sports: “Mimi ningekwenda kumchukua Benzema. Nitampa mkataba wa mkopo wa miezi sita, ni hivyo.”
Na hilo la Ferdinand linaweza kuungwa mkono na kocha wa zamani wa Arsenal, Wenger. Mfaransa huyo alijaribu kumsajili Benzema mara kadhaa kwa kipindi chake alichokuwa kwenye kikosi hicho cha Emirates, huku kocha huyo gwiji wa Arsenal ni shabiki mkubwa wa straika huyo.
“Anacheza soka lake linalozingatia pasi na muunganiko na wengine, hivyo ni mchezaji sahihi kwenye safu ya ushambuliaji,” alisema kocha Wenger alipomzungumzia Benzema mwaka 2021.
Benzema amefunga mabao 13 katika mechi 12 alizocheza msimu huu, lakini kinachoelezwa ni kwamba hajatulia sana huko Saudia kitu ambacho kocha Arteta anaweza kukitumia na kunasa saini ya mchezaji huyo.