Watano Liverpool nje Carabao Cup
Muktasari:
- Kocha huyo alizungumza baada ya kuongoza timu yake kushinda mara ya tano mfululizo msimu huu kwa kuichapa Everton mabao 2-1 katika Ligi Kuu England.
LIVERPOOL, ENGLAND: KOCHA wa Liverpool, Arne Slot amewataja wachezaji watano ambao hawataonekana katika mechi ya raundi ya tatu ya Kombe la Carabao dhidi ya Southampton leo, Jumanne.
Kocha huyo alizungumza baada ya kuongoza timu yake kushinda mara ya tano mfululizo msimu huu kwa kuichapa Everton mabao 2-1 katika Ligi Kuu England.
Katika mchezo huo, Slot alifanya mabadiliko kwa kuingiza wachezaji wanne katika kikosi kilichoanza dhidi ya Atletico Madrid Ligi ya Mabingwa Ulaya Jumatano ambao ni Conor Bradley, Milos Kerkez, Hugo Ekitike na Alexis Mac Allister wakati Andy Robertson, Jeremie Frimpong, Florian Wirtz na Alexander Isak wakianzia benchi.
Slot alithibitisha wachezaji watano waliokuwa kwenye kikosi cha ushindi dhidi ya Everton hawataanza mchezo dhidi ya Southampton Anfield.
“Hii ndiyo sababu timu kama yetu na zile za Ulaya zinahitaji kikosi kama hiki, unacheza michezo mingi sana, muda mwingine pia tumekuwa na changamoto, umeona Alexander Isak wakati anajiunga na sisi hakuwa amefanya mazoezi ya pamoja na timu yake kwa miezi minne, Mac Allister alikuwa na majeraha na wengine wengi.”
“Kitu kizuri ni nina chaguo la kupanga wachezaji ninaowataka ndani ya wiki na niseme wale waliocheza mechi tatu kwa dakika 90 wiki iliyopita ambao ni Virgil Van Dijk, Ibou (Ibrahima Konate), Mo (Mohamed Salah), Ryan (Gravenberch) na Dom (Dominik Szoboszlai), hutawaona Jumanne (leo).”
Slot pia alielezea maeneo ambayo anaamini Liverpool inaweza kuboresha licha ya kujivunia ushindi wake wa tano mfululizo katika Ligi Kuu msimu huu na wa sita katika mashindano yote.
“Tulionyesha mechi nzuri lakini kuna nyakati hatukuwa makini, tulipoteza sana mipira kwa wapinzani wetu na hatukuwa tunawekeza nguvu, jambo kama hili limetokea katika mechi dhidi ya Bournemouth, Newcastle na Atletico. Lazima tuelewe nyakati moja inaweza kubadilisha mchezo bila kujali unacheza vizuri kiasi gani.”