Siri za mitoko ya mastaa
Muktasari:
- Ukweli ni kwamba, nyuma ya muonekano huo kuna siri nyingi ambazo watu wa kawaida huzipuuzia.
Ukiona staa ametupia picha kwenye Instagram au ametokea kwenye zulia jekundu akiwa amependeza kupita maelezo, usikimbilie kusema ana bahati au ana pesa nyingi.
Ukweli ni kwamba, nyuma ya muonekano huo kuna siri nyingi ambazo watu wa kawaida huzipuuzia.
Nguo ya gharama kubwa pekee haimfanyi mtu awe fashionable. Kinachobeba taswira ni namna alivyojiandaa na jinsi alivyochanganya kila kitu kwa umakini.
Hizi ni baadhi ya siri ambazo mastaa wengi huzitumia ili waonekane nadhifu na wenye mvuto kila wanapoonekana hadharani.
1. Wanajua kinachowafaa, si kinachovuma
Si kila mtindo unaotrend unamfaa kila mtu. Mastaa wengi huchagua mavazi yanayoendana na umbo lao, urefu wao na hata rangi ya ngozi. Ndiyo maana unaweza kuona nguo iliyopendeza kwa staa mmoja lakini isitoe mwonekano uleule kwa mwingine.
2. Rangi ni silaha yao kubwa
Fashion si kuvaa tu, bali ni kucheza na rangi. Mastaa hujifunza rangi zinazowapendezesha na kuzichanganya kwa usahihi.
Wengine hutumia rangi tulivu kuonyesha mvuto, huku wengine wakichagua rangi zinazowafanya waonekane sana kwa haraka katika umati wa watu wengi.
3. Viatu vinaamua kila kitu
Unaweza kuvaa nguo nzuri sana, lakini ukakosea viatu ukaharibu mwonekano wote. Mastaa hulipa uzito mkubwa uchaguzi wa viatu kwa kuhakikisha vinaendana na mavazi, mazingira na tukio husika.
4. Accessories zinanogesha
Saa, mkufu, pete, hereni, miwani au mkanda ni vitu vidogo vinavyoongeza thamani ya muonekano. Mastaa hawavai kila accessory waliyonayo kwa wakati mmoja. Huchagua chache zinazokamilisha mwonekano bila kuufanya uonekane umezidi.
5. Usafi ni sehemu ya fashion
Nguo inaweza kuwa ya kawaida kabisa, lakini ikiwa imepigwa pasi vizuri na ni safi, huonekana ya thamani zaidi.
Mastaa wengi huhakikisha mavazi yao hayana mikunjo, viatu vinang’aa na kila kitu kiko katika hali nzuri kabla ya kutoka.
6. Nywele na uso haviwezi kutenganishwa
Hakuna maana ya kuvaa vizuri ikiwa nywele hazijatengenezwa au uso unaonekana umechoka.
Ndiyo maana mastaa huwekeza muda katika kutunza nywele, ngozi na ndevu kwa wanaume ili mwonekano wao uwe kamili.
7. Hujiamini kuliko nguo wanazovaa
Kuna watu huvaa nguo za gharama kubwa lakini bado hawaonekani kuvutia. Siri mojawapo ya mastaa ni kujiamini. Wanavyotembea, kusimama na kuwasiliana na watu hufanya hata mavazi ya kawaida yaonekane ya kipekee.
8. Hawafuati kila trend
Siyo kila kinachotrend lazima kivaliwe. Mastaa wengi wenye fashion ya kudumu huchagua mitindo inayolingana na utambulisho wao badala ya kukimbizana na kila jambo jipya linalotokea.
9. Wanazingatia tukio
Nguo ya harusi si ya kwenda ofisini, na ya ufukweni si ya kuvaa kwenye mkutano rasmi. Mastaa huvaa kulingana na mazingira na aina ya shughuli, jambo linalowafanya waonekane wamepangilia kila kitu kwa umakini.
10. Fashion inaanza na kujitunza
Lishe bora, maji ya kutosha, mazoezi na usingizi wa kutosha huchangia ngozi yenye afya na mwonekano mzuri. Mastaa wengi hujua kuwa hata nguo nzuri haziwezi kuficha mwili usiotu nzwa.