Mkenya awinda mikoba ya Yona Amos
Muktasari:
- Yona aliyekuwa akihusishwa mara kadhaa kujiunga na Yanga na Simba tangu akiwa na Tanzania Prisons, inaelezwa anaweza kuondoka ndani ya kikosi hicho baada ya mkataba wake kumalizika, huku Singida Black Stars ikitajwa kumuhitaji.
MABOSI wa Pamba Jiji wameanza mchakato wa kimya kimya wa kukisuka kikosi hicho kwa ajili ya msimu ujao, ambapo kwa sasa wanaangalia uwezekano wa kusajili kipa namba moja wa Shabana FC, Mkenya Steve Ochieng ili kurithi mikoba ya Yona Amos.
Yona aliyekuwa akihusishwa mara kadhaa kujiunga na Yanga na Simba tangu akiwa na Tanzania Prisons, inaelezwa anaweza kuondoka ndani ya kikosi hicho baada ya mkataba wake kumalizika, huku Singida Black Stars ikitajwa kumuhitaji.
Kipa huyo aliyemaliza na clean sheets nane za Ligi Kuu Bara kwa msimu huu, inaelezwa amegoma kuongeza mkataba mpya na Pamba Jiji na sasa uongozi wa timu hiyo unafanya mazungumzo ya kumsajili, Steve Ochieng wa Shabana FC ya Kenya.
Taarifa kutoka Kenya zinadai, Ochieng amefanya mazungumzo ya awali na Pamba Jiji na makubaliano yameshafikiwa kwa lengo la kipa huyo kucheza Ligi Kuu Bara msimu wa 2026-2027, huku Kocha Mkuu, Francis Baraza akihusika kumshawishi nyota huyo.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Pamba Jiji (CEO), Peter Juma Lehhet alisema baada ya msimu kumalizika watafanyia tathimini ya kina kiujumla kutoka katika benchi la ufundi, kisha kuanza mipango ya kuimarisha kikosi hicho.
“Ni mapema sana kwa sababu msimu ndio umeisha, ila ni kweli kuna wachezaji watapishana na wengine kama ilivyo utaratibu wa misimu yote, maboresho ya kikosi chetu yatafanyika tutakapopokea tu ripoti ya benchi letu la ufundi,” alisema Lehhet.
Hata hivyo, Mwanaspoti linatambua, Yona Amos yupo mbioni kujiunga na Singida Black Stars na sasa uongozi wa Pamba Jiji unamuona Steve Ochieng ni mbadala sahihi, baada ya kuonyesha kiwango bora na Shabana FC na kumaliza na clean sheets 15.
Mbali na clean sheets 15, akiwa na Shabana FC, ila Steve aliiwezesha timu hiyo kumaliza Ligi Kuu ya Kenya msimuhuu, ikishika nafasi ya tano na pointi 52, baada ya kushinda mechi 14, ikitoka sare 10 na kupoteza pia 10, kati ya 34.
Ikiwa kipa huyo atajiunga na Pamba Jiji, atakuwa ni mchezaji wa pili kutoka Shabana baada ya mshambuliaji, Mkenya Mathew Momanyi Tegisi.