Wasaudia wamkomalia Vinicius Jr
Muktasari:
- Vinicius, 24, bado ana mkataba Real Madrid hadi 2027 na ni miongoni mwa wachezaji wanaolipwa mshahara mkubwa kwenye timu hiyo sambamba na Kylian Mbappe wote wakilipwa Pauni 12 milioni kila mmoja kwa mwaka.
MADRID, HISPANIA: REAL Madrid inakabiliwa na kazi ngumu ya kuwadhibiti mabosi wa Saudi Arabia kwenye mpango wa kuvamia Bernabeu kwenda kung’oa huduma ya winga wa Kibrazili Vinicius Jr.
Vinicius, 24, bado ana mkataba Real Madrid hadi 2027 na ni miongoni mwa wachezaji wanaolipwa mshahara mkubwa kwenye timu hiyo sambamba na Kylian Mbappe wote wakilipwa Pauni 12 milioni kila mmoja kwa mwaka. Lakini, Los Blancos inahitaji fowadi huyo asaini dili jipya litakalomfanya abaki kwenye timu yao kwa muda mrefu na ndiyo maana ipo kwenye mazungumzo na mawakala wa mchezaji huyo.
Kwa mujibu wa AS, mabosi wa Saudia wamedhamiria kumnasa Mbrazili huyo katika namna yoyote ile. Jambo hilo limewafanya kumpa Vini Jr ofa ya mkataba wa miaka mitano wenye thamani ya Pauni 832 milioni. Kwa ofa hiyo, hakuna namna yoyote Real Madrid itaweza kuifikia na kumfanya namba mbili huyo wa Ballon d’Or 2024 abaki kwenye kikosi.
Taarifa zinadai kwamba Vini yupo tayari kubaki Madrid, lakini kama atatambulika kuwa staa mkubwa kwenye kikosi hicho basi hata mshahara wake utapaswa kuwa mkubwa.
Rais wa Real Madrid, Florentino Perez amegoma kukutana na mabosi wa Saudia kwa ajili ya kukubaliana juu ya usajili wa Vini Jr, lakini bosi huyo wa Bernabeu amesisitiza kwamba kinachopaswa kufanyika ni kuangalia tu kipengele kilichopo kwenye mkataba wake kinachohitaji ilipwe Euro 1 bilioni kama kuna timu itahitaji huduma yake. Real Madrid inafahamu timu hizo za Saudi Pro League zitaendelea kusumbua juu ya kumpata Vini Jr na ndio maana inataka ikamilishe haraka mazungumzo ya dili jipya fasta.