Penalti na mtihani mchezaji anayeingia dakika za mwisho
Muktasari:
- Inaelezwa kwamba kumwingiza mchezaji katika dakika za mwisho za muda wa nyongeza ili akapige penalti kumekuwa mwenendo wa kawaida katika mashindano makubwa. Lakini takwimu za Kombe la Dunia na mashindano ya soka ya Ulaya zinaonyesha huenda kuna madhara zaidi kuliko faida.
BOSTON, MAREKANI: WANASEMA ni presha, lakini kuna wanaoitaja kuwa ni kama ‘pressure cooker’. Yaani unatakiwa kuingia ili ukabadili matokeo kwa kupiga penalti tena katika dakika zile za lalasalama na ni hapo ndipo swali linapokuja, je kumwingiza mchezaji wa akiba dakika za mwisho ili apige penalti kweli kunafanya kazi?
Inaelezwa kwamba kumwingiza mchezaji katika dakika za mwisho za muda wa nyongeza ili akapige penalti kumekuwa mwenendo wa kawaida katika mashindano makubwa. Lakini takwimu za Kombe la Dunia na mashindano ya soka ya Ulaya zinaonyesha huenda kuna madhara zaidi kuliko faida.
Kupiga penalti, kwa nadharia, ni mojawapo ya kazi rahisi zaidi katika soka. Mpira umesimama na goli liko umbali wa mita takriban 10.5. Katika ngazi ya juu kabisa, unaweza kutarajia kila mchezaji afunge karibu kila mara, lakini shinikizo hufanya mambo kuwa tofauti kwa watu.
Fabian Balbuena aliingia uwanjani katika dakika ya 121 katika mchezo wa Paraguay wa hatua ya 32 bora dhidi ya Ujerumani, huku kocha Gustavo Alfaro akiamini uwezo wake wa kupiga penalti ungewasaidia. Beki huyo wa zamani wa West Ham United alipata nafasi ya kulipa taifa lake ushindi wa kihistoria alipofunga penalti ya tano ya Paraguay, lakini shuti lake liliokolewa na Manuel Neuer. Hata hivyo, aibu ya Balbuena ilifutwa baada ya Jonathan Tah kupiga penalti yake juu ya lango na Jose Canale kufunga na kuhitimisha mojawapo ya ushindi mkubwa zaidi katika historia ya Kombe la Dunia.
Bado, kukosa kwake penalti kunaonyesha mwenendo wa kuvutia wa mashuti ya penalti. Muda wa nyongeza unapokaribia kuisha, imekuwa kawaida zaidi kwa makocha kuingiza ‘wataalamu wa penalti’ ; wachezaji ambao kazi yao pekee ni kuingia na kufunga penalti katika michuano ya kupiga penalti inayotarajiwa muda mfupi baadaye. Kwa mtazamo wa juu, inaonekana ni wazo sahihi. Lakini hugeuka kuwa si rahisi hivyo kiufanisi.
Cha kushangaza, wachezaji wanane kati ya kumi wa mwisho walioingia viwanjani baada ya dakika ya 115 kabla ya michuano ya penalti katika Euro au Kombe la Dunia walikosa penalti zao. Hiyo ni asilimia 20 ya mafanikio na ni watatu kati ya hao wanane waliwakilisha England, bila shaka.
Jamie Carragher aliingizwa katika dakika ya 119 katika robo fainali ya Kombe la Dunia 2006 dhidi ya Ureno, akagusa mpira mara moja tu kabla ya kukosa penalti yake iliyopigwa upya na England kutolewa nchini Ujerumani.
Hivi karibuni zaidi, kocha wa England, Gareth Southgate aliamua kumwingiza Marcus Rashford na Jadon Sancho katika sekunde za mwisho za fainali ya Euro 2020 dhidi ya Italia. Wote wawili walikosa penalti na kuipa Italia nafasi ya kusonga mbele, na Azzurri wakashinda michuano hiyo muda mfupi baadaye.
Kwa England Wachezaji 10 wa mwisho waliopiga penalti baada ya kuingizwa baada ya dakika ya 115 katika mashindano makubwa ni Carragher, Rashford na Sancho angalau walipata nafasi ya kugusa mpira kabla ya kipenga cha mwisho, jambo lililowapa hisia ya kasi na mdundo wa mchezo. Wachezaji wawili hawakugusa hata mpira baada ya kuingia dakika za mwisho, na wote wawili walikosa penalti zao.
Majuzi, Balbuena alikuwa mchezaji wa hivi karibuni kuingia uwanjani bila kugusa mpira kabla ya kupiga penalti, akiungana na Simone Zaza, ambaye muda wake mfupi sana ulitokea katika mechi ya robo fainali ya Euro 2016 dhidi ya Ujerumani.
Kosa la Zaza la penalti lilimletea kejeli nyingi kutokana na mbinu yake isiyo ya kawaida na ya muda mrefu ya kukimbia kuuelekea mpira lakini ufanisi ukawa sifuri. Kumwingiza mchezaji dakika za mwisho hasa kwa ajili ya kupiga penalti katika michuano ya kupigiana penalti mwishoni ni mwenendo mpya kiasi. Ni wachezaji 12 pekee waliowahi kuingia baada ya dakika ya 115 katika Kombe la Dunia au Euro kabla ya kupiga penalti, na matukio matatu tu kati ya hayo yalitokea kabla ya Euro 2016.
Ni mwenendo wa ajabu hasa katika ulimwengu wa soka unaotawaliwa na takwimu, kwa sababu wachezaji wanaoanza mchezo wana uwezekano mkubwa zaidi wa kufunga penalti. Tangu Euro 1996, wachezaji walioanza mchezo wamepiga penalti 277 katika michuano ya mashindano makubwa ya kimataifa, wakifunga 201, ikiwa ni asilimia 73 ya mafanikio.
Wakati huohuo, wachezaji walioingizwa kipindi cha pili cha muda wa nyongeza wamepiga penalti 32 na kufunga 18 pekee, ikiwa ni asilimia 56 ya mafanikio. Huenda miguu mipya haimaanishi akili mpya wakati shinikizo likiwa juu zaidi.