Kombe la Dunia katikati ya eneo la dawa za kulevya
Muktasari:
- Eneo hilo ambalo huwezi kulitofautisha na yale yanayopatikana katika nchi masikini, lipo umbali wa kilomita chache kutoka uwanjani. Wakati maelfu ya mashabiki wakiwa Boston, janga kubwa la matumizi ya dawa za kulevya linaendelea kulikumba eneo linaloitwa Methadone Mile.
BOSTON, MAREKANI: MASHABIKI wa soka wanakabiliwa na hali ya kutisha jijini Boston, Marekani ambako waraibu wa dawa za kulevya wanaofananishwa na “zombi” huzurura katika eneo maarufu linalojulikana kama Methadone Mile.
Eneo hilo ambalo huwezi kulitofautisha na yale yanayopatikana katika nchi masikini, lipo umbali wa kilomita chache kutoka uwanjani. Wakati maelfu ya mashabiki wakiwa Boston, janga kubwa la matumizi ya dawa za kulevya linaendelea kulikumba eneo linaloitwa Methadone Mile.
Eneo hilo, linajulikana kwa matumizi makubwa ya dawa za kulevya aina ya opioid zinazotengenezwa, liko takribani kilomita 31 kutoka Uwanja wa Boston ambao unatumiwa kwa mechi saba za Kombe la Dunia, ambapo wakazi hulitambua kama “Mass and Cass”.
Kwa miaka kadhaa, eneo hilo lilikuwa limejaa makambi ya muda ya watu wasio na makazi pamoja na biashara ya wazi ya dawa za kulevya, ingawa mamlaka za serikali ziliyaondoa mwaka jana, bado mitaa yake inaonekana kuwa na watu wengi wanaopambana na uraibu.
Baadhi ya wanahabari waliotembelea eneo hilo wanalifananisha na “mandhari kutoka katika filamu ya The Walking Dead,” wakieleza kuwa wauzaji wa dawa za kulevya huuza hadharani bila woga.
Mkurugenzi wa Huduma za Afya kwa Wasio na Makazi, Dk Jessie Gaeta, aliliambia The Boston Globe kuwa eneo hilo “kwa muda mrefu limekuwa mahali ambapo watu maskini wa Boston hupata huduma mbalimbali.”
Naye Sue Sullivan, mkuu wa chama cha wafanyabiashara wa eneo hilo, aliiambia WBUR News: “Hali ya kusikitisha inayotokea hapa siwezi kuivumilia. Watu wanaendelea kuumia.”
Jina Methadone Mile lilitokana na wingi wa kliniki zinazotoa methadone, dawa inayotumika kuwasaidia waraibu wa heroini kuacha. Hata hivyo, wataalamu wanaonya kuwa mfumo wa matibabu nchini Marekani bado unawaangusha wengi wanaopambana na uraibu.
Dk Chelsea Shover anasema soko haramu la dawa za kulevya Boston linatawaliwa na fentanyl, ambazo mara nyingi huchanganywa na dawa nyingine kama xylazine na medetomidine.
Akieleza sababu za hali hiyo, anasema ukosefu wa msaada wa kutosha kutoka kwa mamlaka umechangia tatizo hilo.
“Marekani imechukua hatua ambazo kwa kiasi kikubwa zimekuwa kinyume na ushahidi wa kisayansi na imeshindwa kukabiliana ipasavyo na ongezeko la matumizi ya dawa haramu,” anasema.
Anaongeza kuwa wakati nchi nyingi za Ulaya zilichukua hatua madhubuti kukabiliana na migogoro ya heroin katika karne iliyopita, Marekani haikufanya hivyo kwa kiwango kinachohitajika.
“Hakuna nchi iliyo kamilifu, lakini Marekani imekabiliana na tatizo hili vibaya sana. Watu wengi wamepoteza maisha na wengine wataendelea kupoteza maisha ikiwa hali haitabadilika,” anaonya.
Kwa mujibu wa Dk Shover, mojawapo ya changamoto kubwa ni sera kali za serikali kuhusu upatikanaji wa methadone.
“Methadone ni tiba iliyothibitishwa kisayansi kwa watu wenye uraibu. Inaweza kupunguza vifo vinavyotokana na matumizi ya kupita kiasi kwa zaidi ya asilimia 50,” anasema huku akisisitiza kuwa licha ya ufanisi wake, ni vigumu kuipata nchini Marekani kutokana na sheria kali zilizopo.
“Ni kliniki chache maalumu zinazoruhusiwa kuitoa. Mara nyingi wagonjwa hulazimika kwenda kila siku kuichukua, hata kama wanaishi mbali. Hali hii huathiri uwezo wao wa kufanya kazi, kutunza familia na kuendelea na maisha ya kawaida.”
Kutokana na macho ya dunia kuelekezwa Boston wakati wa Kombe la Dunia, polisi wameanzisha operesheni kubwa ya kusafisha mitaa.
Baadhi ya waraibu wamepewa chaguo la kwenda kupata matibabu ya uraibu au kukabiliwa na hatua za kisheria.
Mtafiti wa dawa za kulevya na matumizi yake, Dk. Traci Green, anasema: “Tumeshuhudia kupungua kwa vifo vinavyotokana na matumizi kupita kiasi ya dawa za kulevya. Hii ni sababu kubwa ya vifo kwa watu wasio na makazi Boston na kwa Wamarekani wenye umri wa miaka 18 hadi 44.”