Wanatoboa? Manchester City vs Real Madrid, Inter vs Milan

MANCHESTER, ENGLAND. MATAJI matatu wanabeba hawabebi? Swali hilo linawahusu Manchester City na kesho Jumatano ubishi utamalizwa.

Man City tayari imeshajiweka pazuri kwenye kunyakua taji la Ligi Kuu England msimu huu, wakihitaji pointi tatu tu katika mechi tatu walizobakiza kubeba ubingwa.

Tayari wameshafika fainali ya Kombe la FA na watakuwa na kibarua kizito cha kuwakabili Manchester United katika mchezo wa fainali utakaopigwa Juni 2 huko uwanjani Wembley. Hayo ni mataji mawili ambayo wamejiweka kwenye nafasi nzuri kabisa ya kuyabeba msimu huu. Lakini, taji la tatu wanalosaka, ili wawe na msimu wa kubeba mataji matatu yote makubwa yaliyoshindaniwa, utaamriwa usiku wa kesho wakati watakapokuwa na shughuli pevu ya kuwavua taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, Real Madrid. Man City na Real Madrid zitarudiana katika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya huko uwanjani Etihad baada ya mechi ya kwanza iliyofanyika Jumanne iliyopita, kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Safari hii, matokeo ya sare hayakubali, lazima mmoja ang'oke. Msimu uliopita, Man City na Real Madrid zilikutana pia kwenye hatua kama hiyo ya nusu fainali. Wakati ule, mechi ya kwanza iliyofanyika Etihad ilimalizika kwa Man City kushinda 4-3, walipokwenda Bernabeu kurudiana - Los Blancos ilishinda 3-1 baada ya dakika 120.

Msimu huu, kipute kilianzia Bernabeu, ambapo Vinicius Junior aliifungia Real Madrid bao la kuongoza, lakini Man City ilikuja kusawazisha kwa shuti kali la Kevin De Bruyne. Hiyo kesho hapatoshi.

Kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu, Real Madrid ishazitupa nje timu mbili za England, Liverpool na Chelsea, lakini safari hii mbele yao wapo Man City wanaocheza soka la kibabe kwelikweli. Man City haijapoteza mechi yoyote kati ya 22 zilizopita na imeshinda mechi 15 zilizopita ilizocheza Etihad, ikifunga walau mara mbili katika mechi 14 kati ya hizo na hawajapoteza mechi hapo kwenye Etihad kwa michuano ya Ulaya tangu Septemba 2018.

Real Madrid wanalitaka taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kukwama kwenye La Liga, ambako Barcelona wamenyakua taji hilo kwa msimu huu. Taji lao pekee ambalo wamebeba hadi sasa ni Copa del Rey.

Lakini, shida wanakwenda kuwakabili Man City kwenye wao wa nyumbani - mahali ambako Real Madrid hawajawahi kushinda mara zote nne walizokwenda kucheza hapo. Mshindi atasubiri kwenye kumenyana na ama Inter Milan au AC Milan huko Istanbul, Uturuki kwenye mchezo wa fainali, wakati miamba hiyo ya Italia itakapokabiliana kwenye nusu fainali ya pili usiku wa leo Jumanne huko Giuseppe Meazza. Mechi ya kwanza, Inter ilishinda ugenini 2-0.

Kuhusu kipute cha Etihad, kocha Pep Guardiola aliwapumzisha mastaa wake De Bruyne, Jack Grealish, Bernardo Silva na John Stones kwa ajili ya mechi hiyo - huku mashabiki wakisubiri kushuhudia bato nyingine baina ya Grealish na Dani Carvajal. Real Madrid ina wasiwasi juu ya hali ya kiafya ya staa wao, Eduardo Camavinga baada ya kutolewa dakika za mwisho kwenye mechi dhidi ya Getafe, lakini kinachoelezwa iliwapumzisha David Alaba, Karim Benzema na Rodrygo kwa ajili ya mechi hiyo ya Etihad. Patachimbika.

Kocha Carlo Ancelotti anamtarajia Eder Militao kurejea kikosini kama hilo litafanyika basi Camavinga atarudi kwenye nafasi yake ya kiungo kama ilivyo kawaida endapo kama atakuwa fiti kutumika kwenye mechi hiyo.

Kuhusu Milan derby, kocha wa Inter, Simone Inzaghi aliwapumzisha mastaa wake Lautaro Martinez, Denzel Dumfries na Andre Onana kwa ajili ya mechi hiyo, huku akiwa na kikosi chake kilichokamilika baada ya Robin Gosens na Federico Dimarco wote kuwa fiti kwa ajili ya mchezo huo. Milan Skriniar ndiyo atakosekana kwa kuwa majeruhi, huku Joaquin Correa akiwa na hatihati kubwa, huku kocha Inzaghi akiwa na chaguo la Edin Dzeko na Romelu Lukaku kupata mmoja wa kucheza na Martinez kwenye safu yake ya ushambuliaji. Upande wa Milan, haitakuwa na huduma ya Junior Messias, Rade Krunic na Ismael Bennacer - ambao wamekuwa majeruhi kwa muda mrefu, lakini matarajio ni makubwa ya Rafael Leao kurejea uwanjani. Alexis Saelemaekers litakuwa chaguo jingine, huku Olivier Giroud akirejea kwenye safu ya ushambuliaji na Divock Origi atakwenda benchi, huku nahodha Davide Calabria atarudi kikosini kwenye nafasi ya Pierre Kalulu katika beki ya kushoto. Milan inashughuli pevu ya kupindua matokeo ya kuchapwa 2-0 nyumbani.


Vikosi vinavyotarajiwa;

Man City: Ederson; Walker, Dias, Akanji; Stones, Rodri; Silva, Gundogan, De Bruyne, Grealish; Haaland

Real Madrid: Courtois; Carvajal, Militao, Rudiger, Alaba; Kroos, Camavinga, Modric; Valverde, Benzema, Vini Junior

Inter: Onana; Darmian, Acerbi, Bastoni; Dumfries, Barella, Calhanoglu, Mkhitaryan, Dimarco; Martinez, Dzeko

AC Milan: Maignan; Calabria, Tomori, Kjaer, Hernandez; Tonali, Pobega; Diaz, Krunic, Saelemaekers; Giroud