Wanatoboa, hawatoboi EPL leo

LONDON, ENGLAND. MAMBO ni moto. Ni huko kwenye Ligi Kuu England, ambapo Leo Jumapili, macho na masikio ya wengi yataelekezwa Emirates kushuhudia kipute cha North London derby, ambapo Arsenal itawakaribisha mahasimu wake wa miaka yote, Tottenham Hotspur.
Kuna mtu atapigwa. Mechi za Arsenal na Spurs zinapigwa, basi mambo ni moto.
Rekodi zinaonyesha kwamba miamba hiyo imekutana mara 69 kwenye mechi za Ligi Kuu England, ambapo Arsenal imeshinda 26, mara 19 ikiwa nyumbani na saba ugenini. Spurs imeshinda 18, mara 15 ikiwa nyumbani na tatu tu ugenini ilipokwenda kuifuata Arsenal. Watatoboa? Mechi 25 baina yao zilimalizika kwa sare, huku mara tano za mwisho walizokutana, Arsenal imeshinda tatu na Spurs mara mbili tu. Waache wauane.
Mechi nyingine ya mikikimikiki hiyo ya Ligi Kuu England itakayopigwa kesho, Chelsea itajaribu kuweka mambo yake sawa huko Stamford Bridge itakapoikaribisha Aston Villa. Kocha Mauricio Pochettino bado anajitafuta huko kwenye kikosi cha The Blues na sasa anaikaribisha Aston Villa, huku rekodi zikiwa upande wake baada ya kushinda mara 30 katika mechi 59 alizokabiliana nazo kwenye Ligi Kuu England na mechi 14 zilimalizika kwa sare. Katika mechi hizo, Chelsea yenye ilishinda mara 16 nyumbani na 14 ugenini, huku Aston Villa ushindi wake wote ni mechi 15, mara tisa nyumbani na sita ugenini. Lakini, kwenye mechi mbili za mwisho walizokutana kwenye ligi, Chelsea amepoteza zote.
Liverpool itakuwa nyumbani Anfield kucheza na West Ham United katika moja ya mechi matata kabisa. Mara 57 walizokutana kwenye Ligi Kuu England, Liverpool imeshinda 34, mara 20 nyumbani na 14 ugenini, huku West Ham imeshinda 10, tisa nyumbani na moja tu ugenini - wakati mechi 13 zilimalizika kwa sare.
Mechi mbili za mwisho walizokutana kwenye ligi, Liverpool imeshinda zote.
Brighton iliyoanza msimu huu huu kwa moto wake itakuwa na kazi mbele ya Bournemouth. Rekodi zinaonyesha kwamba Brighton inateswa na Bournemouth kwa mara walizokutana kwenye Ligi Kuu England, ambapo katika mechi 14, Bournemouth imeshinda sita, nne nyumbani na mbili ugenini, huku mechi nne zikilimalizika kwa sare wakati Brighton imeshinda nne, mbili nyumbani na nyingine mbili ilishinda ugenini. Mechi yake itakuwa moto balaa.
Mechi ya mwisho kwa hiyo kesho itakuwa huko Bramall Lane, ambapo Sheffield United itaikaribisha Newcastle United. Mechi ya kibabe sana, kwani mara 12 walizowahi kukutana kwenye Ligi Kuu England hakuna sare. Newcastle imeshinda tisa, tano nyumbani na nne ugenini, huku Sheffield United ikishinda tatu, mbili nyumbani na moja ugenini. Je, itaongeza idadi ya ushindi nyumbani?
Hata hivyo, shughuli hiyo ya mchakamchaka wa Ligi Kuu England itaanza leo Jumamosi, ambapo watu watakuwa wakiisikilizia Manchester United itafanya nini?
Baada ya kupokea vichapo vitatu mfululizo kwenye michuano yote, Man United itakuwa ugenini kukipiga na Burnley katika mchezo wa sita wa Ligi Kuu England msimu huu. Katika mechi tano ilizocheza msimu huu, imechapwa tatu na kushinda mbili tu. Mambo si matamu kabisa huko Old Trafford.
Mechi hiyo ni ya mwisho kabisa kwa siku ya leo, ambapo rekodi zinaonyesha Man United na Burnley zimekutana mara 17 kwenye Ligi Kuu England na wenyeji wa mchezo huo wa leo, wameshinda mara mbili tu, moja nyumbani na moja ugenini, wakati Man United imeshinda 10, tano nyumbani na tano ugenini, huku tano nyingine zilimalizika kwa sare. Mechi tano za mwisho, Man United imeshinda nne dhidi ya Burnley, huku mechi moja ilimalizika kwa sare.
Mabingwa watetezi, Manchester City watakuwa nyumbani Etihad kucheza na Nottingham Forest. Miamba hiyo imekutana mara tisa kwenye Ligi Kuu England, lakini Forest imeshinda tatu, mbili nyumbani na moja ugenini, huku Man City ikishinda mbili tu, moja nyumbani na nyingine ugenini, huku mechi nne baina yao zilimalizika kwa sare. Mechi ya mwisho baina yao ilimalizika kwa sare.
Brentford itakuwa nyumbani uwanjani Gtech Community kukipiga na Everton katika mechi itakayokuwa na upinzani mkali kabisa. Mara sita walizokutana kwenye Ligi Kuu England, Brentford imeshinda mbili, moja nyumbani na nyingine ugenini, huku Everton ikishinda mbili, ambapo zote ilipocheza nyumbani huku mechi mbili zilimalizika kwa sare.
Kutakuwa na kipute kingine matata cha London derby, ambapo Crystal Palace itakuwa Selhurst Park kukipiga na Fulham. Miamba hiyo imekutana mara 10 kwenye Ligi Kuu England, ambapo mechi tatu zilimalizika kwa sare, Palace ikishinda nne, mbili nyumbani na mbili nyingine ugenini, huku Fulham imeshinda tatu, mbili ugenini na moja tu nyumbani.
Luton Town itakuwa na kasheshe mbele ya Wolves, ambayo imewahi kukutana nayo mara moja kwenye Ligi Kuu England. Katika mechi hiyo moja waliyokutana, Luton ndio iliyoshinda ilipokutana Januari 2013 uwanjani Kenilworth Road, ambako kutapigwa kipute hicho cha leo. Ngoja tuone.