Arteta: Unabisha? Angalia takwimu

Muktasari:
- Arteta alirushiwa kijembe na Kocha wa Paris Saint-Germain, Enrique baada ya kudai kikosi chake kilikuwa bora uwanjani kwenye mechi zote mbili dhidi ya miamba hiyo ya Paris, licha ya kupoteza kwa jumla ya mabao 3-1 nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu.
LONDON, ENGLAND: MIKEL Arteta ameshikilia msimamo wake, Arsenal ilikuwa timu bora zaidi kati ya zote zilizocheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu na kumwambia Luis Enrique anayebisha “Kaangalie takwimu.”
Arteta alirushiwa kijembe na Kocha wa Paris Saint-Germain, Enrique baada ya kudai kikosi chake kilikuwa bora uwanjani kwenye mechi zote mbili dhidi ya miamba hiyo ya Paris, licha ya kupoteza kwa jumla ya mabao 3-1 nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu.
Kocha huyo wa Arsenal, Arteta alisema: “Nasimamia nilichokisema kwa asilimia 100. Nimetazama na kuona takwimu zote. Ukitazama takwimu zote muhimu, zile ambazo zinakupa nafasi ya kushinda mechi za mpira wa miguu, zilikuwa wazi kabisa tulikuwa bora. Hata ukitazama takwimu za matarajio ya bao, ilikuwa tano dhidi ya tatu, kwa mechi zote mbili, lakini yeye ndiyo kafika fainali.”
Madai hayo ya takwimu ya Arteta yanakumbushia tukio la kocha wa zamani wa Liverpool, Rafa Benitez wakati alipoingia kwenye mzozo na kocha wa Manchester United, Sir Alex Ferguson wakati alipotoa takwimu zake na kudai Liverpool ilikuwa bora mwaka 2009 zaidi ya miamba hiyo ya Old Trafford.
Arteta alisema: “Unapocheza na PSG na kisha wakakufunga, unashikana mikono na kusema. Bado hatupo tayari. Lakini, ukiwatazama usoni na namna tulivyowatesa, unaweza kuona ulivyo na timu bora.”
Lakini, bosi huyo wa Arsenal alikubali Liverpool imestahili kubeba taji la Ligi Kuu England msimu huu kwa sababu kikosi chake kilishuka ubora. Arteta mwanzoni alisema Liverpool imetangza ubingwa na pointi 82, wakati wao walivuna pointi 84 na 89 na kuishia nafasi ya pili kwa misimu miwili mfululizo, kitu ambacho Liverpool ilijibu wao wana uwezo wa kufikisha pointi 91, ambazo Arsenal haijawahi kuzifikia endapo itashinda mechi zake zote zilizobaki.