Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Madrid ya Alonso, mtaomba poo!

Muktasari:

  • Kocha huyo Mhispaniola anahusishwa na mpango wa kwenda kuchukua mikoba ya kuinoa klabu hiyo ya Bernabeu baada ya kutangaza ataachana na Bayer Leverkusen mwisho wa msimu huu.

MADRID, HISPANIA: REAL Madrid itakuwa ya fomesheni ya tofauti kabisa chini ya kocha mpya Xabi Alonso.

Kocha huyo Mhispaniola anahusishwa na mpango wa kwenda kuchukua mikoba ya kuinoa klabu hiyo ya Bernabeu baada ya kutangaza ataachana na Bayer Leverkusen mwisho wa msimu huu.

Alonso atatua Real Madrid kwenda kuchukua mikoba ya Carlo Ancelotti, anayetarajia kutimkia Brazil.

Los Blancos imejipanga pia kufanya maboresho makubwa ndani ya uwanja kuhusu kikosi chao.

Miamba hiyo ya Bernabeu ipo kwenye hatua za mwisho kukamilisha dili la kumnasa beki wa kulia wa Liverpool, Trent Alexander-Arnold. Wachezaji wengine inaowasaka ni pamoja na beki wa kati wa Arsenal, William Saliba, staa wa Bournemouth, Dean Huijsen, mkali wa Girona, Miguel Gutierrez na kiungo wa Real Sociedad, Martin Zubimendi.

Kama itafanikiwa kunasa wakali wote inaowasaka, Real Madrid itakuwa kwenye muundo mpya kabisa na mbinu tofauti za kiuchezaji chini ya kocha Alonso. Kiungo huyo mchezeshaji wa zamani wa Liverpool na Bayern Munich amekuwa akitumia fomesheni tofauti katika kipindi chake alichofanya kazi ya ukocha.

Lakini, fomesheni maarufu ya Alonso kwenye kikosi cha Leverkusen ni 3-4-2-1, ambayo aliitumia kubeba ubingwa wa Bundesliga msimu uliopita bila ya kupoteza mechi yoyote kwenye ligi.

Kwa fomesheni hiyo, ina maana golini atakuwa kipa Thibaut Courtois na kulindwa na mabeki watatu wa kati ambao ni Saliba na Huijsen watakaoungana na Eder Militao kwenye ukuta huo.

Hiyo ina maana hakutakuwa na nafasi kwa staa wa zamani wa Chelsea, Antonio Rudiger na wa Bayern Munich, David Alaba - ambao kuna uwezekano mkubwa wakaonyesha mlango wa kutokea.

Juu ya ukuta wa mabeki hao watatu wa kati, kwenye wing-back kutakuwa na Alexander-Arnold upande wa kulia na Gutierrez kushoto, huku viungo wawili watakaokuwa kati mbele ya mabeki wa kati ni Federico Valverde na Zubimendi.

Juu yao kutakuwa na Jude Bellingham na Vinicius Jr, ambao watakuwa wanacheza nyuma ya mshambuliaji wa kati, Kylian Mbappe.

Fomesheni nyingine Alonso aliyokuwa akiitumia Leverkusen, hasa msimu huu ni ile ya 4-4-2.

Hiyo inahusu ukuta wa mabeki wanne, ambao utakuwa na Alexander-Arnold, Saliba, Huijsen na Gutierrez, ambao watakuwa na kazi ya kumlinda kipa Courtois.

Kwenye mtindo huo wa uchezaji, Bellingham atakuwa pacha wa Zubimendi kwenye eneo la kiungo, huku mawinga watakuwa Wabrazili wawili, Vinicius Jr na Rodrygo.

Katika eneo la fowadi, kinda Endrick anaweza kupata nafasi ya kuanza sambamba na Mbappe.

Mtindo wa mwisho wa kiuchezaji ambao Alonso anaweza kuutumia ni 4-2-3-1, fomesheni ambayo alikuwa akiitumia wakati alipokuwa akikinoa kikosi B cha Real Sociedad. Uzuri wa fomesheni hiyo ndiyo ambayo imekuwa ikitumika kwa sasa na Real Madrid chini ya kocha Ancelotti.

Na kwamba Alonso anaweza kuwa na ukuta ule ule wachezaji watano wakisaidiwa na viungo Zubimendi na Eduardo Camavinga. Rodrygo, Bellingham, Vinicius Jr na Mbappe watakuwa kwenye orodha ya wachezaji wanne ambao akili yao itakuwa kwenye kushambulia zaidi.

Kwenye kipute cha La Liga, Real Madrid usiku wa Jumapili itakuwa ugenini kukipiga na Barcelona katika mchezo muhimu kabisa wa mchakamchaka wa kufukuzia ubingwa wa ligi kwa msimu huu.

Barca inaongoza msimamo wa LaLiga baada ya kukusanya pointi 79 katika mechi 34, pointi nne zaidi ya Real Madrid, yenye pointi 75 katika mechi 34. Mechi hiyo imebeba hatima ya mbio za ubingwa wa La Liga msimu huu.