Wanasakwa wakavae buti za Rashford Man United
Muktasari:
- Miamba hiyo ya Nou Camp inampiga hesabu za kumchukua jumla winga huyo wa England na kama hilo likitokea kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi, basi Rashford atakuwa ameshacheza mechi yake ya mwisho na kumalizana na Man United.
MANCHESTER, ENGLAND: KINACHOONEKANA ni kama vile Marcus Rashford ameshacheza mechi yake ya mwisho kwenye kikosi cha Manchester United baada ya kuwa na msimu mzuri akiwa kwa mkopo huko Barcelona.
Miamba hiyo ya Nou Camp inampiga hesabu za kumchukua jumla winga huyo wa England na kama hilo likitokea kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi, basi Rashford atakuwa ameshacheza mechi yake ya mwisho na kumalizana na Man United.
Staa huyo wa kimataifa wa England aliondolewa katika mipango ya klabu ya Old Trafford kufuatia mzozo wake na kocha Ruben Amorim mwaka uliopita. Licha ya kwamba Amorim ameshafutwa kazi huko Man United, lakini Rashford anaonekana kufurahia maisha ya Barcelona na mabosi wa timu hiyo wanavutiwa na kile anachofanya, hivyo kuna kitu kinakwenda kutokea kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi.
Rashford amefunga mabao 10 na kuasisti mara tisa katika mashindano yote. Sasa Barcelona inaonekana kuwa na mpango wa kukifanya kazi kipengele cha kumsajili jumla, ambapo itahitaji kulipa ada ya uhamisho ya Pauni 25 milioni ili kumchukua jumla.
Na sasa kama Rashford atakamilisha uhamisho wake wa kujiunga na Barcelona mwishoni mwa msimu huu, jambo hilo litaifanya Man United kufanya usajili wa kuziba pengo lake na kwenye hilo kuna orodha ya wachezaji watano wanaopigiwa hesabu za kuletwa Old Trafford.
BRADLEY BARCOLA
Bradley Barcola akiwa sehemu ya kikosi cha Paris Saint-Germain kilichoshinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita, ameendelea kuwa bora kwenye kikosi hicho cha Parc des Princes chini ya kocha Luis Enrique. Mchezaji huyo mwenye miaka 23 amefunga mabao 10 na kuasisti mara nne msimu huu na anaendelea kujijengea sifa kama mmoja wa mawinga wenye vipaji vkubwa barani Ulaya. Amefunga mabao 10 katika Ligue 1. Gazeti la Sport linamwelezea kama mmoja wa winga wenye matumaini makubwa barani Ulaya na jina kubwa katika orodha hii.
YAN DIOMANDE
Yan Diomande mwenye miaka 19 anakipiga kwenye kikosi cha RB Leipzig na amekuwa na msimu mzuri sana akicheza kama winga. Amefunga mabao mabao 11 na pasi za mabao tano katika mashindano yote kutoka mechi 21 alizoanza. Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ivory Coast amewavutia mabosi wa Man United kwa kasi yake na uwezo wa kumiliki mpira. Anachukuliwa kama mmoja wa wachezaji chipukizi wenye vipaji vikubwa katika nafasi ya winga na hilo ndilo linalowafanya wababe hao wa Old Trafford kuhitaji huduma yake.
JESUS RODRIGUEZ
Man United inaripotiwa kumhitaji sana Jesus Rodriguez kutokana na kile anachokifanya huko Como 1907. Staa huyo mwenye umri wa miaka 20 ambaye anaendelea kufanya vizuri chini ya kocha Cesc Fabregas. Rodriguez ameanza mechi 15 katika Serie A msimu huu na ametoa pasi saba za mabao. Katika mashindano yote, amefunga mabao matatu baada ya kufunga na kutoa pasi ya bao katika ushindi wa Como 3–1 dhidi ya U.S. Lecce mwishoni mwa mwezi uliopita.
MARTIAL GODO
Man United iliwahi kumwamini mchezaji kijana aliyeitwa Anthony Martial zamani na sasa kuna chipukizi mwingine wa kuvutia nchini Ufaransa.
Martial Godo mwenye miaka 22 anakipiga katika kikosi cha RC Strasbourg amevutia klabu hiyo baada ya kufunga mabao 11 na kuasisti moja katika mashindano yote. Mchezaji huyo mzaliwa wa England aliwahi kuwa katika akademi ya Fulham na sasa anachezea timu ya taifa ya Ivory Coast na kiwango chake cha uwanjani ni kitu kinachowafanya mambo wa Man United kumfikiria.
ILIMAN NDIAYE
Ingawa msimu wake haujawa na mabao mengi sana kwenye kikosi cha Everton, gazeti la Sport linaamini kuwa Iliman Ndiaye amefanya vya kutosha kuwavutia Manchester United. Mchezaji huyo wa kimataifa wa Senegal amefunga mabao sita na kuasisti mara tatu katika mashindano yote na amekuwa mchezaji muhimu kwa kocha David Moyes msimu huu. Ameanza mechi 23 kati ya 29 za Ligi Kuu England za Everton na thamani yake inakadiriwa kuwa karibu Pauni 40 milioni kwa mujibu wa Transfermarkt.