Baraka za Vatican zamfuata Messi Marekani
Muktasari:
- Baada ya mchezo huo uliochezwa usiku wa kuamkia Jumamosi Julai 4, 2026, Messi alikuwa akielekea kumaliza shughuli zake za mahojiano alipokutana na shabiki aliyefanikiwa kumkaribia.
MIAMI, MAREKANI:Nahodha wa Argentina, Lionel Messi, alipokea zawadi maalum iliyobarikiwa na Vatican baada ya tukio la kugusa hisia lililotokea kufuatia ushindi wa Argentina dhidi ya Cape Verde katika hatua ya 16 bora ya Kombe la Dunia 2026.
Baada ya mchezo huo uliochezwa usiku wa kuamkia Jumamosi Julai 4, 2026, Messi alikuwa akielekea kumaliza shughuli zake za mahojiano alipokutana na shabiki aliyefanikiwa kumkaribia.
Shabiki huyo alimkabidhi rozari iliyobarikiwa kutoka Vatican, jambo lililomgusa sana nahodha huyo wa Argentina.
Shabiki huyo alimweleza Messi kuwa zawadi hiyo haikuwa yake pekee, bali pia ilikuwa kwa mke wake, Antonela Roccuzzo, watoto wao, baba yake na familia yake yote.
Kabla ya kumkabidhi rozari hiyo, alimshukuru nahodha huyo wa Argentina kwa furaha aliyowaletea mamilioni ya Waargentina katika kipindi chote cha maisha yake ya soka.
Messi aliipokea zawadi hiyo kwa tabasamu, akamshukuru shabiki huyo na kumpa mkono kabla ya kuendelea na safari yake.
Tukio hilo lilisambaa haraka kwenye mitandao ya kijamii, huku mashabiki wengi wakilisifu kama ishara ya heshima na upendo kwa mmoja wa wachezaji wakubwa zaidi katika historia ya soka. Wengi walieleza kuwa zawadi hiyo ilikuwa na thamani kubwa ya kiroho kuliko ya kifedha.
Messi, ambaye ni Mkatoliki, amekuwa akionyesha mara kadhaa umuhimu wa imani katika maisha yake. Kupokea rozari iliyobarikiwa na Vatican kulionekana kuwa tukio lenye maana ya pekee kwake, hasa wakati akiwa kwenye harakati za kuiongoza Argentina kutetea ubingwa wa Kombe la Dunia.
Argentina imetinga hatua ya robo fainali baada ya ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Cape Verde, huku Messi akiendelea kuwa tegemeo kubwa la timu hiyo katika mbio za kutetea taji lao la dunia akifikisha mabao saba.
Sasa Argentina inakwenda kucheza dhidi ya Misri katika mechi ya kuwania kufuzu robo fainali itakayochezwa Julai 7, 2026.