Wanafaa kabisa kutua Madrid

MADRID, HISPANIA. REAL Madrid inajiandaa kuwa bize kwelikweli kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi kuleta straika mpya baada ya Karim Benzema kuripotiwa kwamba ataachana na klabu hiyo mwaka huu.

Straika huyo Mfaransa anaonekana tayari akili yake ameshaielekeza kwenye kuhamia Saudi Arabia kujiunga na Al Ittihad. Hivyo, Benzema, 35, ataondoka Santiago Bernabeu baada ya miaka 14 na kuvuna mataji 24 makubwa.
Huko Saudi Arabia atakwenda kulipwa Pauni 342 milioni kwa mkataba wa miaka miwili atakayokuwa Al Ittihad.

Hata hivyo, Real Madrid watakuwa kwenye kasheshe zito la kumpata straika mwingine wa aina yake, wakati Benzema akiondoka kwenye timu hiyo akiwa amefunga mabao 353. Kwenye kusaka straika mwingine wa kuja kurithi buti za Benzema huko Bernabeu, hii hapa orodha ya wakali wanane wanaotosha kabisa kwa kazi hiyo.

1. Harry Kane; Staa huyo wa Tottenham, 29, amekuwa na msimu mzuri kabisa akifunga mabao 30 kwenye Ligi Kuu England. Lakini, timu yake imemaliza kwenye nafasi ya nane na kukosa tiketi ya michuano ya Ulaya, hivyo kupata nafasi ya kwenda kujiunga na timu itakayompa nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, kutamvutia.

2. Cristiano Ronaldo; Mreno huyo, 38, anaweza kuwa chaguo la muda mfupi, lakini uzuri anajua jinsi mambo yanavykwenda Bernabeu. Ronaldo alitamba na Real Madrid kwa miaka tisa na kuwa kinara wa mabao wa timu hiyo. Kwa sasa Ronaldo yupo huko Saudi Arabia akikipiga kwenye kikosi cha Al Nassr alijiunga akitokea Man United.

3. Victor Osimhen; Straika huyo wa Napoli ni moja ya majina yanayosakwa kwelikweli kwenye dirisha hili la usajili. Timu kibao zinamtaka baada ya kufunga mabao 25 msimu huu na kingine umri wake ndiyo kwanza miaka 24. Saini yake itaibua vita kali kutokana na timu nyingine ikiwamo Bayern Munich na Man United kuhitaji huduma yake pia.
 

4. Marcus Rashford; Rashford, 25, alikuwa na msimu mzuri huko Manchester United, alipofunga mabao 30 katika mechi 55 za michuano yote. Akinaswa atakwenda kuunda safu matata na Vinicius Jr na Rodrygo huko Madrid. Mkataba wake Old Trafford utafika tamati 2024, hivyo Los Blancos wanaweza kutumia hilo kumnasa kirahisi.
 

5. Erling Haaland; Kwenye umri wa miaka 22, Haaland tayari ameshaonyesha kuwa yeye ni balaa kwenye kufunga, akipachika nyavuni mara 52 katika mechi 51 akiwa na Manchester City msimu huu. Madrid wanamsaka kwelikweli. Kingine kinachoelezwa ni kwamba Haaland mwenyewe mipango yake ya baadaye ni kwenda kucheza Real Madrid.

6.Kylian Mbappe; Real Madrid ilishindwa kumnasa Mbappe mwaka jana, bila ya shaka inaweza kujaribu kunasa saini yake kwenye dirisha hili hasa kutokana na Benzema kuondoka. Mbappe mwenyewe atakuwa tayari kutua Bernabeu. Ni jambo la wazi, Mfaransa huyo atakapoachana na Paris Saint-Germain, basi Madrid linaweza kuwa chaguo bora.
 

7.Lautaro Martinez; Martinez, 25, amefurahia msimu mzuri Inter Milan alikofunga mabao 21 katika mechi 37 za Serie A msimu huu. Ametinga fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, bila shaka ni huduma nzuri kuwa nayo kikosini. Tayari jina lake limekuwa likitajwa kwenye timu nyingi, lakini Madrid wakimnasa watakuwa wamepata mtu wa maana.

8. Kai Havertz; Fowadi huyo wa Chelsea litakuwa chaguo la kushtua Madrid. Lakini, lisemwalo tayari miamba hiyo ya Bernabeu inahusishwa na mpango wa kunasa saini yake na huenda akanaswa kwenye kuvaa buti za Benzema. Havertz amekuwa muhimu Chelsea amefunga mabao kibao ya ushindi la mambo yangekuwa mabaya zaidi The Blues.