Walipa kodi mashuhuri Ligi Kuu England
Muktasari:
- Kwa mujibu wa The Times, Haaland amechangia kodi kubwa kuliko mchezaji mwingine yeyote katika ligi hiyo kwa mwaka huo.
LONDON, ENGLAND: STAA wa Manchester City, Erling Haaland anaongoza katika orodha ya wachezaji wa Ligi Kuu England waliolipa kodi kubwa zaidi, takribani Pauni 16.9 milioni mwaka jana.
Kwa mujibu wa The Times, Haaland amechangia kodi kubwa kuliko mchezaji mwingine yeyote katika ligi hiyo kwa mwaka huo.
Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Norway, mwenye umri wa miaka 25, anaripotiwa kulipwa takribani Pauni 500,000 kwa wiki.
Haaland, ambaye ni mfungaji bora wa Ligi Kuu England hadi sasa kwa msimu huu, pia hupata Pauni 10 milioni zaidi kupitia bonasi na haki za matumizi ya picha kwa mwaka.
Mkataba wake Etihad unatarajiwa kumalizika mwaka 2034.
Hata hivyo, kiasi cha kodi cha Haaland bado ni kidogo ukilinganisha na watu wengine waliopo katika sekta ya michezo na burudani nchini humo.
Kwa mujibu wa ripoti, familia ya Done, ambayo ni maarufu kwa biashara ya kamari, ililipa zaidi ya Pauni 400 milioni mwaka jana.
Mohamed Salah mwenye umri wa miaka 33, anashika nafasi ya pili katika orodha ya wachezaji wanaopata pesa nyingi, pia yeye na Haaland ndio pekee walioingia katika orodha ya 100 bora ya wanaolipa kodi kubwa, hiyo ni baada ya kusaini mkataba mnono Aprili mwaka jana. Kijumla analipa kodi ya Paun 14.4 milioni.
Mchezaji mwingine wa Liverpool, Virgil van Dijk anashika nafasi ya tano kwa kulipa kodi kubwa zaidi za EPL, akilipa Pauni 9.7 milioni.
Kiungo wa Manchester United, Casemiro anashikilia nafasi ya tatu na alilipa Pauni 10.9 milioni, huku Raheem Sterling ambaye hakuwa akicheza kabisa Chelsea alilipa Pauni 9.8 milioni.
Sterling, 31, ambaye hakuwa ameichezea Chelsea kwa miezi 18, bado alikuwa analipwa mshahara mkubwa wa Pauni 325,000 kwa wiki, katika mkataba wake uliokuwa unaendelea hadi Juni 30, 2027.
Katika orodha hiyo pia kuna wachezaji wengi kutoka Jiji la Manchester na mbali ya Haaland na Casemiro pia yumo Bruno Fernandes na Bernardo Silva (wote wakilipa kodi ya takribani Pauni 9 milioni kwa mwaka, huku Omar Marmoush alilipa Pauni 8.8 nmilioni.
Aliyekuwa mshambuliaji wa Manchester City, Gabriel Jesus, anaingia katika 10 bora kwa makadirio ya kulipa kodi ya Pauni 7.9 milioni.
Mshambuliaji mwenzake wa Arsenal, Kai Havertz amehitimisha orodha hiyo akiwa na kiwango sawa cha kodi na Jesus.
Licha ya mastaa wengi wa EPL kupata pesa nyingi kama mshahara, kiasi kikubwa kinaonekana kurudi kwa mamlaka za nchi kama sehemu ya kodi.
Mchezaji anayelipwa Pauni 300,000 kwa wiki, kiasi anachoingiza kwenye akaunti yake huwa ni kati ya Pauni 155,000 hadi Pauni 160,000, hiyo kutokana na kodi ya kati ya asilimia 47 hadi 50. Hivo mchezaji anayelipwa Pauni 15 milioni kwa mwaka hutakiwa kulipa kodi ya Pauni 7.5 milioni kwa mwaka.