WAFALME WAPYA ULAYA: Kane, Olise, Diaz waandika historia Bayern Munich
Muktasari:
- Washambuliaji hao watatu wa Bayern Munich wameandika historia baada ya wote kufunga mabao dhidi ya PSG, Jumanne, wiki hii, na hivyo Harry Kane, Michael Olise na Luis Diaz sasa wamefunga jumla ya mabao 100 katika mashindano yote msimu huu.
MUNICH, UJERUMANI: HARRY Kane, Michael Olise na Luis Diaz wamevuka mabao 100 na kuandika historia ya kipekee ya pacha yenye watu watatu katika msimu wa Ligi Kuu Ujerumani (Bundesliga).
Hii ina maana pacha hiyo ya mabao (Goal Trio), imekuwa ya msimu wa saba kwa jumla katika ligi tano bora za Ulaya kufanya hivyo.
Washambuliaji hao watatu wa Bayern Munich wameandika historia baada ya wote kufunga mabao dhidi ya PSG, Jumanne, wiki hii, na hivyo Harry Kane, Michael Olise na Luis Diaz sasa wamefunga jumla ya mabao 100 katika mashindano yote msimu huu.
Kwa kufanya hivyo, wao ni kikosi cha kwanza cha mastraika watatu kuwahi kufanya hivyo kwa klabu isiyo ya Hispania, ambako rekodi kama hizo zimewahi kufikiwa. Hayo pia ni mafanikio yaliyopatikana mara ya saba tu ndani ya karne hii.
Kane, Olise na Diaz wote walifunga katika kipigo cha Bayern Munich cha mabao 5-4 dhidi ya PSG, ambapo nahodha wa England, Kane, ndiye aliyekuwa wa kwanza kutupia, akiongeza idadi yake hadi mabao 54 katika mechi 46 msimu huu.
Wakati huohuo, Diaz alifunga mara ya 26 katika mechi 46 na Olise ana mabao 20 katika mechi 47 kwenye mashindano yote. Kulikuwa na historia zaidi kwa Kane, kwani alifunga katika mechi yake ya sita mfululizo ya Ligi ya Mabingwa.
Na ni hapo anakuwa Mwingereza wa kwanza kufanya hivyo katika mfululizo unaorudi hadi hatua ya ligi. Kane alifunga dhidi ya Union Saint-Gilloise na PSV kabla ya kufunga mabao mawili katika mchezo wa marudiano wa hatua ya 16 bora dhidi ya Atalanta.
Nahodha huyo wa England kisha alifunga katika kila mechi ya robo fainali dhidi ya Real Madrid kabla ya kufanya hivyo tena Jumanne. Licha ya mechi ya kwanza dhidi ya PSG kutoa mabao tisa, Kane anaamini ulinzi ulikuwa bado wa kiwango cha juu.
Vikosi vya mabao 100
Kane, Olise na Diaz ni washambuliaji watatu wa nmara ya kufunga mabao 100 katika mashindano yote ndani ya msimu mmoja.
Vikosi saba vilivyotangulia vyote vilifanya hivyo kwa Barcelona au Real Madrid, ambapo vinawajumuisha kina Lionel Messi, Luis Suarez na Neymar katika misimu mitatu mfululizo kati ya 2014 na 2017.
Messi pia alifanya hivyo akiwa na Cesc Fabregas na Alexis Sanchez pamoja na Samuel Eto’o na Thierry Henry katika misimu ya 2011/12 na 2008/09 mtawalia.
Kwa upande wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo na Karim Benzema walihusika katika vikosi vyote viwili vilivyofikia mafanikio hayo.
Wawili hao walifanya hivyo pamoja na Gonzalo Higuain mwaka 2011/12 na pamoja na Gareth Bale mwaka 2014/15.
MSIKIE KANE
Akizungumza na Amazon Prime, jana, Kane alieleza kuwa, “hata kama mabao tisa yalifungwa kulikuwa na ulinzi wa ajabu uwanjani.
“Unakuwa na wachezaji bora duniani. Washambuliaji bora, walinzi bora. Bila shaka, wakati mwingine washambuliaji watakuwa juu na kuonyesha ubora wao. Ukitazama mabeki wa kati wakicheza katikati wakati mwingine kushambulia pembeni dhidi yao inafaa.”