HAKUNA KULALA: Wakubwa vitani Ufaransa Ligi ya Mabingwa Ulaya
Muktasari:
- Bayern Munich inakwenda kwenye mchezo huu ikiwa na rekodi nzuri baada ya kutwaa taji hili mara sita huku PSG ikilitwaa taji hilo mara moja.
PARIS, UFARANSA: MABINGWA watetezi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, PSG wanatarajiwa kuvaana na mabingwa wa Ligi Kuu Ujerumani (Bundesliga), Bayern Munich katika mchezo wa kwanza wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mjini Paris, Ufaransa, kesho, huku picha kubwa ikiwa.
Bayern Munich inakwenda kwenye mchezo huu ikiwa na rekodi nzuri baada ya kutwaa taji hili mara sita huku PSG ikilitwaa taji hilo mara moja.
Timu hizi mbili zimezoeleka kuwa na mechi zenye ushindani mkali, baada ya zote kufuzu hatua hii kwa kuwaondoa vigogo, PSG wakiitoa Liverpool huku Bayern wakiiondosha Real Madrid.
Kila timu imefunga mabao 38 katika mashindano ya msimu huu, idadi kubwa kuliko timu nyingine yoyote, hali inayoongeza hamasa kuelekea pambano hili.
PSG wanahitaji ushindi ili kufika fainali kwa mara ya pili mfululizo, lakini watakutana na kigingi kigumu dhidi ya Bayern ambao wamekuwa mwiba kwao katika misimu ya hivi karibuni.
Ushindi wa mabao 2-1 wa Bayern Munich katika hatua ya makundi msimu huu uliendeleza rekodi ya ushindi wa mechi tano mfululizo dhidi ya PSG.
Hata hivyo, PSG wanaweza kujipa matumaini kutokana na uzoefu wa msimu uliopita ambapo walipoteza mapema dhidi ya Arsenal, lakini wakarejea kwa nguvu hatua za mtoano na hatimaye kuwatupa nje.
Macho yote yatakuwa kwa nahodha wa Paris, Marquinhos, ambaye anakaribia kufikisha mechi 120 katika Ligi ya Mabingwa akilingana na rekodi ya Mbrazili mwenzake, Roberto Carlos, ambaye kwa sasa ameachana na soka.
Marquinhos atakutana na mshambuliaji hatari wa Bayern Munich, Harry Kane, ambaye tayari amefunga mabao 12 msimu huu ikiwamo pia mechi tano mfululizo za mashindano hayo.
Huo utakuwa mchezo wa 16 kati ya timu hizi kwenye Ligi ya Mabingwa, ambapo Bayern wanaongoza kwa ushindi mara tisa dhidi ya sita za Paris.
Bayern pia wameshinda mechi tano zilizopita kati yao, ikiwemo ushindi wa 2-1 jijini Paris, msimu huu. PSG wamefanikiwa kufika nusu fainali kwa misimu mitatu mfululizo, rekodi ambayo haijawahi kufikiwa na klabu yoyote ya Ufaransa. Kwa upande mwingine, Bayern wanacheza nusu fainali kwa mara ya 22 katika historia yao, wakishinda 11 kati ya hizo.
DONDOO MUHIMU
Huu ni mchezo wa 16 kati ya Paris Saint-Germain na Bayern Munich chini ya mwavuli wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambapo Bayern wanaongoza kwa ushindi mara 9 dhidi ya 6 za Paris, huku wakishinda mechi tano zilizopita mfululizo, ikiwemo ushindi wa mabao 2-1 walioupata jijini Paris katika mechi ya nne ya hatua ya makundi katika msimu huu.
Katika michezo mitatu ya hatua za mtoano, Bayern Munich wameibuka washindi mara mbili, fainali ya mwaka 2020 kwa ushindi wa 1-0 na hatua ya 16 bora msimu wa 2022/23 kwa jumla ya mabao 3-0. Paris walifanikiwa kusonga mbele katika robo fainali ya msimu wa 2020/21 kwa faida ya bao la ugenini baada ya sare ya jumla ya 3-3.
PSG wameshinda mechi tatu pekee kati ya 11 za hivi karibuni za UEFA dhidi ya timu za Ujerumani (sare mbili na kupoteza sita).
Hii itakuwa mara ya tatu kwa Paris kukutana na wapinzani kutoka Ujerumani katika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa, ambapo waliifunga RB Leipzig mabao 3-0 mwaka 2019/20 kabla ya kupoteza kwa jumla ya 2-0 dhidi ya Borussia Dortmund, msimu wa 2023/24.
Klabu hiyo ya jijini Paris imefanikiwa kufika nusu fainali kwa misimu mitatu mfululizo, rekodi ambayo haijawahi kufikiwa na klabu yoyote ya Ufaransa katika historia ya mashindano ya Klabu Bingwa Ulaya au Ligi ya Mabingwa. Kwa ujumla, PSG wamefika nusu fainali mara tano, wakishinda mara mbili na kupoteza mara tatu.
Iwapo PSG watashinda, huo utakuwa ushindi wa 100 katika historia ya mashindano hayo, na kuwafanya kuwa klabu ya kwanza ya Ufaransa kufikia mafanikio hayo. Ushindi wao wa kwanza ulikuwa mwaka 1994/95, walipoifunga Bayern mabao 2-0 nyumbani katika hatua ya makundi.
Kwa upande wa wachezaji, nahodha Marquinhos anaweza kufikisha mechi ya 120 katika Ligi ya Mabingwa na kulingana na Roberto Carlos.
Naye Nuno Mendes, akiwa na umri wa miaka 23 na siku 313, anaweza kuwa Mreno mwenye umri mdogo zaidi kufikisha mechi 50, akivunja rekodi ya Cristiano Ronaldo.
Kwa upande wa Bayern, wamefanikiwa kushinda mechi 14 kati ya 16 za mwisho za UEFA dhidi ya timu za Ufaransa (wakipoteza mbili), pamoja na kushinda sita kati ya saba walizocheza ugenini.
Pia wameshinda mechi tano kati ya saba za hatua za mtoano za mikondo miwili dhidi ya timu za Ufaransa, na kushinda zote tatu za mechi za mkondo mmoja, ikiwemo ushindi wa 3-0 dhidi ya Lyon katika nusu fainali ya msimu wa 2019/20.
Bayern unich kwa sasa wamefika nusu fainali mara ya 22 katika historia ya mashindano ya Ulaya, wakishinda 11 kati ya 21 zilizopita katika hatua hiyo. Hata hivyo, wameshinda mara moja kati ya sita za mwisho za nusu fainali kwa mabao 3-0 dhidi ya Lyon 2019/20, na kupoteza zote tano za hivi karibuni za mikondo miwili.
Naye mshambuliaji Kane ameweka rekodi yake bora ya mabao katika Ligi ya Mabingwa kwa kufunga mara 12 msimu huu akivunja rekodi yake ya mabao 11 msimu uliopita.
Idadi hiyo pia ni kubwa zaidi kuwahi kufungwa na mchezaji Mwingereza katika msimu mmoja wa mashindano hayo. Kane pia amefunga katika mechi tano mfululizo za Ligi ya Mabingwa kwa mara ya kwanza katika maisha yake ya soka akiwa mchezaji wa pili wa England kufanya hivyo baada ya Steven Gerrard 2007/08.
MKOCHA WANASEMAJE?
Akizungumzia mchezo huo, kocha wa PSG, Luis Enrique alisema timu yake bado inaendelea kukua licha ya kuwa mabingwa watetezi, ilhali mshambuliaji Ousmane Dembele akisisitiza kuwa wana njaa ya mataji zaidi.
Naye Vincent Kompany wa Bayern Munich aalisema wanakabiliwa na changamoto kubwa, lakini wana imani ya kufanya vizuri, huku kiungo wa timu hiyo, Joshua Kimmich akiongeza kuwa timu bora Ulaya sasa zinakutana katika hatua hii. Baada ya mchezo huo kesho kutakuwa na mechi nyingine ya nusu fainali kati ya Atletico Madrid ambayo itavaana na Arsenal nchini Hispania.