Steven Gerrard ‘akomaa’ na PSG Ligi ya Mabingwa Ulaya
Muktasari:
- Gerrard ametoa utabiri huo kufuatia kiwango kikubwa kilichooneshwa na mabingwa hao wa Ufaransa katika hatua ya nusu fainali dhidi ya Bayern Munich.
GWIJI wa Liverpool na mchambuzi wa soka, Steven Gerrard, ameitabiria Paris Saint-Germain (PSG) kutetea taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA Champions League) msimu huu.
Gerrard ametoa utabiri huo kufuatia kiwango kikubwa kilichooneshwa na mabingwa hao wa Ufaransa katika hatua ya nusu fainali dhidi ya Bayern Munich.
Kauli ya nahodha huyo wa zamani wa Liverpool inakuja baada ya PSG kuibuka na ushindi wa kusisimua wa 5-4 dhidi ya Bayern Munich katika mchezo wa kwanza wa nusu fainali uliopigwa Jumanne, Aprili 28, 2026 jijini Paris.
Katika mechi hiyo ya kihistoria, Khvicha Kvaratskhelia na Ousmane Dembélé kila mmoja alifunga mabao mawili, huku João Neves akifunga moja na kuwapa faida mabingwa hao watetezi kuelekea mechi ya marudiano.
Akizungumza kupitia TNT Sports, Gerrard amesema amekuwa akiipa nafasi PSG tangu mashindano yalipoanza msimu huu 2025-2026.
"Imekuwa ni PSG tangu mwanzo. Sijaweka dau la kifedha, lakini chaguo langu lilikuwa PSG. Baada ya fainali ya mwaka jana, naona wako vizuri sana wanapokuwa kwenye kiwango chao bora, ni vigumu sana kuwafunga," amesema Gerrard.
Gerrard ameongeza kuwa, PSG ina uwezo wa kipekee wa ‘kubadili gia’ na kuongeza kasi inapocheza mechi kubwa za Ulaya, akilinganisha uwezo huo na ule wa Real Madrid wa miaka ya nyuma.
Licha ya ushindi huo wa nyumbani, PSG inakabiliwa na kibarua kigumu kwenye mechi ya mkondo wa pili itakayopigwa wiki ijayo Mei 6, 2026, itakapoelekea Ujerumani kuvaana na Bayern Munich.
Bayern waliofungiwa mabao na Harry Kane, Michael Olise, Dayot Upamecano na Luis Díaz katika mchezo wa kwanza, watahitaji ushindi wa bao moja tu (kutokana na sheria ya mabao ya ugeni kuondolewa) ili kupeleka mechi hiyo kwenye muda wa ziada au matuta.
Ikiwa PSG itafanikiwa kuvuka hatua hiyo, itacheza fainali ya pili mfululizo Mei 30, 2026, mjini Budapest, Hungary dhidi ya mshindi kati ya Arsenal na Atlético Madrid ambao walitoka sare ya 1-1 katika mechi ya mkondo wa kwanza iliyopigwa jana jijini Madrid, Hispania.