Waarabu kuongeza mzigo kwa Ederson Man City

Muktasari:
- Staa huyo wa kimataifa wa Brazil ameanza kuhusishwa na timu hiyo katika siku za karibuni kwa kile kinachoelezwa kwamba alipishana kauli na kocha Pep Guardiola ambaye ametoa ruhusa kama akipata timu aende.
AL ITTIHAD ya Saudi Arabia imepanga kuongeza ofa ili kufikia Pauni 30 milioni kuhalikisha inaipata saini ya kipa wa Manchester City, Ederson Santana de Moraes maarufu kama Ederson katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Staa huyo wa kimataifa wa Brazil ameanza kuhusishwa na timu hiyo katika siku za karibuni kwa kile kinachoelezwa kwamba alipishana kauli na kocha Pep Guardiola ambaye ametoa ruhusa kama akipata timu aende.
Pia Ederson anataka kupata changamoto mpya na pesa nyingi zaidi ambazo Uarabuni amewekewa mezani.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka vyanzo mbalimbali Al Ittihad ambayo inamtaka na Mohamed Salah inataka kumpa Ederson mshahara unaofikia mara tatu zaidi ya ule anaoupata kwa sasa wa Pauni 180,000 kwa wiki.
Kipa huyo namba moja na tegemeo Man City mkataba wake unatarajiwa kumalizika 2026. Tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 43 za michuano yote, huku 26 akimaliza bila kufungwa.
ARSENAL imevutiwa na winga wa Stade Rennais, Desire Doue na imepanga kuwasilisha ofa katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi ambapo timu kibao pia zinahitaji huduma yake ikiwa ni pamoja na Tottenham Hotspur. Doue mwenye umri wa miaka 18, amezivutia timu nyingi kutokana na kiwango alichoonyesha tangu kuanza kwa msimu huu. Mkataba wake unatarajiwa kumalizika ifikapo 2026.
IKIWA Manchester itafikia makubaliano ya kumwajiri Maurico Pochettino kama kocha mkuu katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi, kuna uwezekano wa asilimia nyingi akawachukua Conor Gallagher na Trevoh Chalobah kutoka Chelsea. Mastaa hao inaelezwa kuwa ni moja ya sababu za Pochettino kugombana na mabosi wa Chelsea, alihitaji wasiuzwe katika dirisha lijalo, lakini mabosi walishaamua kuwauza.
BEKI wa Barcelona anayecheza kwa mkopo, Real Betis, Chadi Riad, 20, anatarajiwa kuwasili England ndani ya wiki hii kwa ajili ya kufanyiwa vipimo vya afya kabla ya kusaini mkataba na Crystal Palace. Inaelezwa Palace itailipa Barcelona kiasi cha Pauni 12 milioni kwa ajili ya kumsajili staa huyu wa kimataifa wa Morocco. Msimu uliopita Chadi alicheza mechi 30.
ASTON Villa imefikia makubaliano ya kumsajili kiungo wa Luton Town, Roas Barkley katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Supastaa huyo aliyewahi kuhusishwa na Manchester United katika wiki za hivi karibuni, kwa sasa anaruhusiwa kuondoka Luton kwa sababu katika mkataba wake kuna kipengele cha kumruhusu kufanya hivyo ikiwa timu itashuka daraja.
KIUNGO wa Fiorentina na Morocco, Sofyan Amrabat, 27, anatarajiwa kuingia katika mazungumzo na wawakilishi wa Manchester United juu ya hatima yake ikiwa atasaini mkataba wa kudumu au atarudi Fiorentina. Amrabat ambaye alijiunga na Man United dirisha lililopita mkataba wake una kipengele cha kumsainisha moja kwa moja ikiwa Man United watavutiwa na kiwango chake.
KIUNGO wa Tottenham Hotspur na Denmark, Pierre-Emile Hojbjerg, 28, amewaambia kwamba anataka kuondoka dirisha lijalo kutafuta timu itakayompa nafasi kubwa ya kucheza katika kikosi cha kwanza tofauti na ilivyo sasa akiwa na Spurs. Mara kadhaa Atalanta ambayo imefuzu kucheza Ligi ya Mabingwa kwa msimu ujao imetajwa kumtaka.
MABINGWA wa Bundesliga, Bayer Leverkusen wapo katika hatua nzuri kuwania saini ya kiungo wa Girona, Mhispania Aleix Garcia, 26, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi kwa ada ya uhamisho inayodaiwa kufikia Euro 20 milioni. Kocha Xabi Alonso ameripotiwa kufanya mazungumzo binafsi na staa huyo ili kumshawishi ajiunge naye.