Waamuzi kuvalishwa kamera Kombe la Dunia la Klabu 2025

Muktasari:
- Kwa mara ya kwanza katika historia ya soka, katika mashindano ya FIFA, waamuzi watakaochezesha mechi za Kombe la Dunia la Klabu za mwaka huu, 2025, yatakayofanyika Marekani, watavalishwa kamera (body cameras).
SOKA kwa asilimia kubwa linazidi kuhamia katika teknolojia na baada ya kushuhudiwa kwa matumizi ya marudio ya picha za video zinazomsaidia mwamuzi kutafsiri makosa uwanjani (VAR), teknolojia ya kuamua kama mpira umevuka mstari na nyingine nyingi, sasa inakuja nyingine na hii inahusu kamera za waamuzi wa kati.
Kwa mara ya kwanza katika historia ya soka, katika mashindano ya FIFA, waamuzi watakaochezesha mechi za Kombe la Dunia la Klabu za mwaka huu, 2025, yatakayofanyika Marekani, watavalishwa kamera (body cameras).
Lengo la kuwavisha kamera hizo, ni kuongeza uwazi na ushirikishwaji wa mashabiki katika mchakato wa kutoa maamuzi uwanjani.
Kamera hizi zitatumika kurekodi mtazamo wa waamuzi moja kwa moja kutoka mahali walipo uwanjani, hivyo kuwapa mashabiki na watazamaji fursa ya kuona jinsi maamuzi yanavyotolewa kwa karibu na moja kwa moja.
Teknolojia hii inalenga kuongeza imani ya mashabiki kwa maamuzi ya waamuzi na kupunguza lawama zisizo na msingi zinazotolewa dhidi yao.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi, sehemu ya picha zitakazorekodiwa na kamera hizo zitakuwa zikirushwa mubashara wakati wa mechi, hivyo kutoa picha halisi ya tukio linaloendelea, ikiwa ni pamoja na hali ya mechi, mazungumzo ya waamuzi na mazingira halisi yanayowaathiri wakati wa kufanya maamuzi.
Mbali na kamera hizo kwa waamuzi, kutakuwa pia na matumizi ya teknolojia mpya ya kusaidia kubaini mchezaji aliyeotea kwa haraka na kwa usahihi zaidi.
Mfumo huu utatumia akili bandia (AI), kamera nyingi pamoja na sensa za mpira, kusaidia maamuzi ya haraka na ya kweli kuhusu nafasi ya mchezaji aliyepo kwenye eneo la kuotea.
Pamoja na teknolojia hiyo, mfumo wa VAR (Video Assistant Referee) utaendelea kuwa na jukumu la kuhakikisha uhalali wa taarifa zinazopatikana kutoka kwenye mfumo mpya. VAR itahakikisha kuwa hata maamuzi madogo au yenye utata yanazingatia ukweli kwa kutumia picha na taarifa za kisasa zaidi.
Kwa mujibu wa FIFA, lengo kuu ni kuendeleza uwazi, usahihi na matumizi ya teknolojia katika soka, ili kuhakikisha haki inatendeka kwa timu zote na mashabiki wanapata burudani ya kiwango cha juu bila sintofahamu ya maamuzi.
Ikiwa mafanikio ya matumizi ya kamera za waamuzi yatakuwa ya kuridhisha, huenda teknolojia hiyo ikaanza kutumika pia katika mashindano mengine makubwa kama Kombe la Dunia, Ligi ya Mabingwa na hata ligi mbalimbali za kitaifa kote duniani.