Wa kuipa ubingwa Arsenal ni hawa

MANCHESTER, ENGLAND. ARSENAL bado inasaka wachezaji watatu ili kuboresha kikosi chenye nguvu na uwezo wa kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu.
Licha ya kutumia pesa nyingi msimu uliopita kwenye usajili wa kiangazi, kikosi cha kocha Mikel Arteta kwa sasa kipo katika nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu England, pointi moja nyuma ya vinara Manchester City.

Chini ya kocha Arteta, Arsenal imezidi kuimarika baada ya kumaliza katika nafasi ya pili msimu uliopita. Timu hiyo ilikaribia kubeba ubingwa wa ligi, hata hivyo ikaborongga dakika za lalasalama.

Wamiliki wa klabu hiyo walifanya uwekezaji mkubwa ndani ya klabu hiyo ili kumuunga mkono kocha huyo, huku wakiwasajili masupastaa Declan Rice, Jurrien Timber na Kai Havertz kwa jumla ya Pauni 205 milioni, ilhali David Raya akitua kwa mkopo. Kwa sasa wachezaji hao wamekuwa na mchango mkubwa tangu walipotua kwani matunda yameanza kuonekana licha ya kutolewa kwenye michuano ya Kombe la Carabao na West Ham United.

Mkataba wa kumsajili Rice kutoka West Ham kwa Pauni 105 milioni umekuwa wa mafanikio Arsenal na nyota huyo wa kimataifa wa England anaonekana kuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi hicho.

Lakini, aliyekatishwa tamaa zaidi ni Havertz ambaye ameshindwa kuzoea maisha ya Jiji la London baada ya uhamisho wake wa Pauni 65 milioni kutoka Chelsea. Je, Arsenal inapaswa kufanya nini dirisha la Januari, 2024 litapofunguliwa?
Ukiangalia kikosi cha sasa cha Arsenal utaamini kwamba kuna nafasi tatu ambazo inapaswa kufikiria kuongeza mastaa matata kabisa katika dirisha dogo ikiwa ni beki wa kushoto, kiungo wa kati na mshambuliaji.
Kwa mujibu wa ubashiri uliofanywa na kompyua ya xGOLD ambayo imetumika kuchagua aina ya wachezaji ambao wanastahili kusajiliwa na wanovutia zaidi sokoni  imechagua nyota watatu ambao Arsenal inapaswa kuwasajili ili kuboresha kikosi msimu huu.


Pervis Estupinan- (Brighton-Pauni 30 milioni)
Arsenal ilimsajili beki wa kimataifa wa Ukraine, Oleksandr Zinchenko ambaye anacheza beki wa kushoto, lakini pia anaweza kucheza katika nafasi tofauti. Mara nyingi beki huyo anapenda kuingia ndani ya eneo la hatari na lile la kati kwenye sehemu ya kiungo.

Kwa mujibu wa xGold Arsenal inakosa beki wa kushoto anayecheza nafasi yake halisi. Pia haina beki mwenye uwezo wa kutengeneza mashambulizi ya moja kwa moja, ndio maana Estupinan akapendezwa kwani ana sifa ya uchezaji kama beki wa kushoto, hivyo Arsenal itafaidika zaidi endapo itampata.


Khephren Thuram-     Nice- Pauni 35 milioni
Ni kiungo wa kati wa Nice ambaye Arsenal inapaswa kumfuatilia na thamani yake imetajwa hapo juu. Khephren ni mtoto wa nyota wa zamani wa kimataifa wa Ufaransa, Lilian Thuram na pia mdogo wake na Marcus Thuram anayeichezea AC Milan. Khephren Thuram ana uwezo wa kucheza aina zote za mechi ngumu, na atakuwa mtu sahihi Arsenal ikimsajili kwani ataongeza kitu kwenye kikosi.


Serhou Guirassy-         Stuttgart- Pauni 15 milioni
Ni mshambuaji wa kimataifa wa Guinea ambaye ni moto wa kuotea mbali Ligi Kuu Ujerumani (Bundesliga) anayekipiga Stuttgart. Fowadi huyo mwenye umri wa miaka 27 ameanza msimu kwa kiwango bora kwani katika michezo tisa ametupia kambani mabao 15 Bundesliga. Kitu cha kushangaza ni kipengele cha kununuliwa ambacho ni Pauni 15 milioni. Inafahamika kwamba safu ya ushambuliaji ni eneo jingine ambalo Arsenal inaangazia zaidi ukizingatia Gabriel Jesus anasumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara na pengine fowadi huyu anaweza kuwa sululisho.