Arsenal bado kidogo tu kunasa saini ya Zubimendi

Muktasari:
- Arsenal imekuwa ikimfukuzia Zubimendi, 26, tangu majira ya kiangazi ya mwaka jana baada ya kukoswa na kiwango chake huko Sociedad na kwenye hilo inaripotiwa kuishinda Real Madrid kwenye vita ya kunasa saini ya staa huyo.
ARSENAL imeripotiwa kufikia kwenye hatua nzuri ya kumsajili kiungo wa Real Sociedad, Martin Zubimendi katika dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi huko Ulaya.
Arsenal imekuwa ikimfukuzia Zubimendi, 26, tangu majira ya kiangazi ya mwaka jana baada ya kukoswa na kiwango chake huko Sociedad na kwenye hilo inaripotiwa kuishinda Real Madrid kwenye vita ya kunasa saini ya staa huyo.
Kwa mujibu wa Fabrizio Romano, Arsenal imekubali kulipa Pauni 50 milioni kuvunja mkataba wa kiungo huyo ili akakipige Emirates msimu ujao.
Hata hivyo, mashabiki wa Arsenal hawajafurahishwa sana na taarifa hizo za kusajiliwa kwa kiungo mkabaji kwa sababu wanatambua tatizo lao kubwa lipo kwenye nafasi ya mshambuliaji wa kati.
Kilio cha mashabiki wa Arsenal ni kuona timu yao inafanya usajili wa straika wa kiwango cha dunia, kitu ambacho kimeshindwa kufanyika kwa miaka mitatu mfululizo, ambayo imeshuhudia timu hiyo ikishika nafasi ya pili kwenye mikikimikiki ya Ligi Kuu England.
Rafael Leao
CHELSEA imeripotiwa kuanzisha mazungumzo ya kunasa huduma ya winga wa AC Milan, Rafael Leao kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi. Miamba hiyo ya soka ya Serie A ipo tayari kuachana na staa huyo wa kimataifa wa Ureno mwenye umri wa miaka 25 kwa ada ya uhamisho ya Pauni 63.5 milioni. Kiwango bora kwenye Serie A kimemfanya Leao asakwa na vigogo wengi Ulaya.
Joan Garcia
ARSENAL imeripotiwa kuwa kwenye hatua za mwisho kabisa kukamilisha usajili wa kipa wa Kihispaniola, Joan Garcia, anayekipiga katika kikosi cha Espanyol ya Hispania. Kipa huyo mwenye umri wa miaka 24 anatazamwa kama mtu sahihi wa kwenda kumpa ushindani wa namba David Raya kwenye kikosi hicho kinachonolewa pia na kocha Mhispaniola, Mikel Arteta, anayetaka kipa mwingine.
Jobe Bellingham
BORUSSIA Dortmund imeripotiwa kuwa kwenye mchakamchaka wa kuwania hduma ya staa wa Sunderland, Jobe Bellingham, 19, kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi ili akakipige huko Ujerumani. Dortmund inamtaka Jobe apite kwenye njia alizopita kaka yake, Jude Bellingham, ambaye alinaswa na miamba hiyo ya Bundesliga kabla ya kuuzwa kwa pesa nyingi Real Madrid.
Darwin Nunez
MIAMBA ya soka ya Italia, Napoli imeripotiwa kumfukuzia kwa karibu straika wa Liverpool na Uruguay, Darwin Nunez, 25, kunasa saini yake kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi. Napoli inahitaji kuboresha safu yao ya ushambuliaji baada ya kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, hivyo inahitaji huduma za wachezaji wenye uzoefu wa michuano mikubwa.
James McAtee
NOTTINGHAM Forest imeripotiwa kuwa kwenye mchakato wa kunasa huduma ya kiungo mshambuliaji wa Manchester City, James McAtee, 22. Lakini, ushindani wa kupata saini yake ni mkali kutokana na staa huyo kuwa na rada za timu nyingine kama Tottenham Hotspur na Bayer Leverkusen, ambazo zinaweza kumpa nafasi ya kwenda kucheza michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Florian Wirtz
KIUNGO wa Kijerumani anayesakwa na Manchester City katika dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi, Florian Wirtz, ameripotiwa kufikia makubaliano ya kutua Bayern Munich. Sasa mabingwa hao wa Bundesliga wamepanga kulipa Pauni 87.1 milioni ili kunyakua saini ya Wirtz, 22, ambaye amekuwa kwenye kiwango bora kabisa klabu Bayer Leverkusen.
William Saliba
ARSENAL imeripotiwa kuanzisha mazungumzo na beki wa kati wa Ufaransa, William Saliba, 24, kwa ajili ya kumsainisha mkataba mpya utakaomfanya aendelee kubaki Emirates kwa muda mrefu. Arsenal inafanya hivyo ili kuepuka chokochoko za Real Madrid inayoripotiwa kuhitaji huduma ya beki huyo ili akajiunge na timu yao huko Bernabeu msimu ujao.