Vyombo vya habari Ujerumani vyamchambua Kane
Muktasari:
- Kane alijiunga na Bayern kwa ada ya uhamisho ya Pauni 104 milioni akitokea Tottenham Hotspur kwenye dirisha la uhamisho wa majira ya kiangazi mwaka jana na tangu alipotua Allianz Arena, amekuwa akifunga tu bila ya kikwazo.
MUNICH,UJERUMANI: VYOMBO vya habari za Ujerumani zimemgeukia straika wa Bayern Munich, Harry Kane licha ya kuwa na rekodi tamu ya kufunga kwenye Bundesliga.
Kane alijiunga na Bayern kwa ada ya uhamisho ya Pauni 104 milioni akitokea Tottenham Hotspur kwenye dirisha la uhamisho wa majira ya kiangazi mwaka jana na tangu alipotua Allianz Arena, amekuwa akifunga tu bila ya kikwazo.
Katika mechi 52 za michuano yote, Kane, 31, amefunga mabao 54 na kuasisti 17.
Alishindwa Kiatu cha Dhahabu cha Bundesliga katika msimu wake wa kwanza na aliweka rekodi za mabao kibao.
Hata hivyo, gazeti la Bild linamshutumu Kane kwa kushindwa kung’ara kwenye mechi kubwa.
Baada ya Bayern kutoka sare ya 1-1 dhidi ya Bayer Leverkusen, Jumamosi iliyopita, mwandishi wa kolamu kwenye gazeti hilo la Bild, Walter M. Straten aliandika: “Kazi kubwa, mafanikio kidogo. Harry Kane anazurura tu pale mbele.”
Kane alipata maumivu ya enka mwishoni mwa mchezo huo na kutolewa kwenye dakika 86 na taarifa ya Bayern ilisomeka: “Harry Kane alipata maumivu ya enka katika mechi ya Bundesliga dhidi ya Bayer Leverkusen, Jumamosi. Vipimo vilifanywa Jumapili kujua ukubwa wa tatizo lake. Ataendelea kupatiwa matibabu.”
Kane aliibua wasiwasi mkubwa kama atakuwapo kwenye kikosi cha Bayern Munich kitakachocheza na Aston Villa kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya leo Jumatano.
Na kocha wa Bayern, Vincent Kompany alisema: “Tunaamini sio siriazi sana. Mimi sio daktari, lakini natumai atacheza dhidi ya Aston Villa, Jumatano.”