Viwanja hivi vimetelekezwa

RIO DE JANEIRO, MAREKANI. NI pesa nyingi sana hutumika kwenye kujenga viwanja vya mpira wa miguu na michezo mingine duniani, lakini baada ya hapo huwa na mwisho mbaya.
Achana na viwanja vilivyochezewa Kombe la Dunia kule Qatar ambavyo vimebomolewa, kuna baadhi ya viwanja hadi sasa vimetelekezwa na vimekuwa makazi ya ndege na wadudu wengine.
Hii inaonekana baada ya kutotumika kwa muda mrefu. Leo tumekuletea viwanja vitano vilivyotelekezwa ambavyo baadhi vimebomolewa kabisa na vingine vimeendelea kuwa makazi ya watu wasio na makazi na wadudu mbalimbali.
5. Maracana – Brazil
Unaitwa The Estadio Jornalista Mario Filho, au Maracana Stadium, ni moja ya viwanja maarufu kuwahi kutokea kwenye soka duniani.
Uwanja huu unapatikana huko Rio de Janeiro, Brazil. Ulijengwa na serikali ya Brazil na ukatumika kwa ajili ya kuandaa fainali za Kombe la Dunia mwaka 1950 na 1947.
Hadi kufikia mwaka 1950, ulikuwa ndio uwanja mkubwa zaidi kuwahi kutokea duniani ambao ulikuwa na uwezo wa kuingiza mashabiki 199,854.
Ulitumika kwa mechi ya fainali ya Kombe la Dunia kati ya Brazil na Uruguay na baada ya hapo ukawa sehemu ya kuandaa matamasha mbalimbali ya muziki.
Uwanja huu ulitelekezwa rasmi mwaka 2016 baada ya michuano ya Olimpiki.
Kwa sasa umebaki tupu, hauna umeme, baadhi ya viti vimeibiwa, mageti yameharibika.
4. Donbass Arena – Ukraine
Moja kati ya viwanja vya kisasa kuwahi kujengwa nchini Ukraine, kiwanja hiki kiliwahi kuandaa michuano ya Euro 2012 na UEFA Cup.
Michoro na dizaini nzima ya uwanja huu iliundwa na kampuni ya ArupSport, ambayo pia imetengeneza viwanja vingine vikubwa barani Ulaya kama City of Manchester Stadium (Manchester, England), Allianz Arena (Munich, Ujerumani), na Sydney Football Stadium (Sydney, Australia).
Lakini kazi ya kuujenga ilikuwa ya kampuni ya Uturuki, ENKA.
Uwanja huu umetelekezwa kutokana na mgogoro unaoendelea baina ya Urusi na Ukraine, Ulikuwa ukitumiwa sana na Shakhtar ambao kwa sasa wamehamia Lviv na Kharkiv baada ya eneo hilo kuwa sehemu ya vita.
3. Pontiac Silverdome – Marekani
Ilitumika kiasi cha Dola 55 milioni mwaka 1975 kujenga uwanja huu ambao ulikuwa na uwezo wa kuingiza mashabiki 80,000 na ulikuwa ukitumiwa na timu ya mpira wa rugby ya Detroit Lions.
Uwanja huu pia ulikuwa ukitumika kwa mpira wa miguu ingawa muda mwingi Detroit ndio walikuwa wakiutumia na tangu waondoke mwaka 2002, uwanja huu hautumiki tena na umebakia kama uchafu maeneo ya mjini.
Uliwahi kutumika kwa ajili ya kuandaa Kombe la Dunia mwaka 1994, ulifungwa rasmi mwaka 2015 na ukabomolewa mwaka 2017.
2. Lluis Sitjar – Hispania
Estadio Lluis Sitjar ulikuwa uwanja wa nyumbani wa RCD Mallorca. Ulikuwa ukiingiza mashabiki wasiopungua 18,000 na ulitumiwa na Mallorca kwa miaka zaidi ya 50 hadi walipouacha mwaka 1999 kuhamia Iberostar Stadium ambao wanautumia kwa sasa.
Wakiwa kwenye uwanja huu wa Sitjar, Mallorca walifanikiwa kushinda mataji mawili ya Ligi Kuu nchini Hispania miaka ya 1960.
Uwanja huu ulipewa jina la aliyekuwa raisi wao Lluis Sitajar Castella. Mwaka wao wa mwisho kucheza hapa walimaliza nafasi ya tatu kwenye La Liga.
Baada ya kuondoka kwao uwanja huu ulifungwa mwaka 2007 na ukabomolewa rasmi mwaka 2014.
1. Stadion za Luzankami - Jamhuri ya Czech
Unapatikana huko Brno nchini Jamhuri ya Czech. Ulikuwa ni uwanja wa mpira wa miguu ambao ulitumiwa na FC Zbrojovka Brno, hadi sasa unashikilia rekodi ya kuwa uwanja ulioingiza mashabiki wengi kwenye mechi moja ya Ligi Kuu nchini Czech.
Lakini tangu FC Zbrojovka Brno iache kuutumia uwanja huu hakuna timu nyingine ilioutumia, miti imeota kwenye maeneo mbalimbali ya majukwaa na imekuwa ni nyumba ya watu wasio na makazi, ulifungwa rasmi mwaka 2001.