Arteta: Msimu ujao hatukosei tena
Muktasari:
- Arsenal ambayo ilikuwa na matumaini ya kushinda walau Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kuitoa Real Madrid katika robo fainali imejikuta ikiendeleza ukame wa vikombe chini ya Mikel Arteta.
LONDON, ENGLAND: KOCHA wa Arsenal, Mikel Arteta amefichua alitarajia Arsenal kushinda taji la Ligi Kuu England katika mechi yao ya mwisho nyumbani msimu huu na sasa amepanga kufanya usajili wa kishindo dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Arsenal ambayo ilikuwa na matumaini ya kushinda walau Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kuitoa Real Madrid katika robo fainali imejikuta ikiendeleza ukame wa vikombe chini ya Mikel Arteta.
"Mwanzoni mwa msimu, kama nilikuwa na picha ya kucheza mechi ya mwisho ya nyumbani siku ya mwisho na kuinua kombe la Ligi Kuu. Hicho ndicho kilichokuwa kichwani mwangu," alisema Arteta alipofanya mahojiano na Sky Sports.
"Sasa, kwa kila kitu tulichopitia katika miezi 11 iliyopita, inatakiwa tusahau na kutazama mbele ingawa bado tuna uchungu tumboni kwani mataji ndiyo kitu tulichokitamani."
Imepita misimu mitano mfululizo bila ya Arsenal kushinda taji lolote, baada ya kutolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na nusu fainali ya Kombe la Carabao, pamoja na kutolewa raundi ya tatu ya Kombe la FA na Manchester United kwa mikwaju ya penalti.
Alipoulizwa kuhusu sababu kuu za kushindwa kutimiza malengo yao msimu huu, Arteta alisema:"Kadi nyekundu na majeraha, bila shaka ndiyo vimesababisha hali hii."
Msimu huu Arsenal imekumbwa na idadi kubwa ya majeruhi kuliko timu nyingine yoyote ya Ligi Kuu na wachezaji wao wengi (6) wameonyeshwa kadi nyekundu kuliko timu yoyote.
"Tunapaswa kufanya kitu zaidi msimu ujao, kwa sababu kiwango cha ushindani kitapanda."
"Unapotazama pointi tulizokusanya misimu mitatu iliyopita, kuwa na kiwango kama hicho na bado kutoshinda taji ni jambo la nadra sana. Hii inaonyesha tuko karibu, karibu sana na tunapaswa kuendelea kuwa hapo na kuwa bora zaidi."