VIDEO: Maajabu! Uwanja mpya Man United kuingiza watu 100,000

Muktasari:
- Mmiliki mwenza wa klabu hiyo, bilionea Sir Jim Ratcliffe atatumia Pauni 2 bilioni kujenga uwanja huo utakaofahamika kwa jina la ‘Wembley ya Kaskazini’ utajengwa kwenye eneo la Old Trafford.
MANCHESTER, ENGLAND: HII ni kufuru. Manchester United itajenga uwanja mpya wenye uwezo wa kuingiza mashabiki 100,000 wanaoketi, imeelezwa.
Mmiliki mwenza wa klabu hiyo, bilionea Sir Jim Ratcliffe atatumia Pauni 2 bilioni kujenga uwanja huo utakaofahamika kwa jina la ‘Wembley ya Kaskazini’ utajengwa kwenye eneo la Old Trafford.
Uwanja wa sasa wa Old Trafford utavunjwa na kushushwa kitu kipya kabisa katika eneo hilo.

Klabu ya Manchester United imethibitisha kujenga uwanja mpya wenye uwezo wa kuingiza mashabiki 100,000 karibu na uwanja wa sasa wa Old Trafford.
Taarifa ta ujenzi wa Uwanja huo mpya imekamilisha mpango kazi wa mmiliki mwenza wa Man United Sir Jim Ratcliffe, ambaye aliahidi kufanya hivyo kufuatia uchakavu wa Uwanja wa Old Trafford.
Gharama za ujenzi wa Uwanja mpya zinatajwa kufikia Pauni2 bilioni.
Uwanja huo mpya utakuwa wa pili kwa ukubwa kwenye orodha ya viwanja vya mpira wa miguu Ulaya, kikifuatia nyuma ya Nou Camp, uwanja wa nyumbani wa Barcelona.
Serikali itasaidia kutoa pesa kuendeleza maeneo yatakayozunguka uwanja huo mpya.

Uwanja wa sasa wenye umri wa miaka 115 iliyopita, ambao umekuwa ukifahamika kama “Theatre of Dreams” umekuwa sehemu kubwa ya utajiri wa kutosha wa historia ya soka la Uingereza.
Lakini, Kikosi Kazi cha kuijenga upya Old Trafford kinachosimamiwa na mmiliki mwenza wa klabu hiyo ya Man United, bilionea Ratcliffe - kimethibitisha mpango wa kuvunja uwanja huo na kuujenga mpya kabisa katika eneo hilo.

Kikosi kazi hicho kimefichua kwamba kufanya maboresho tu ya Old Trafford ya sasa, ambayo imejenga tangu 1910, uwezo wake ungepanda tu kutoka watazamaji 74,000 hadi 87,000 wanaoketi.
Uwanja huo mpya si tu utakuwa na uwezo wa kuingiza watazamaji 100,000, lakini utakuwa na miundombinu ya kisasa kabisa ambayo ni sehemu ya maendeleo mapya kwenye historia ya Uingereza.

Mpango huo wa ujenzi wa uwanja mpya wa Man United umeungwa mkono na serikali na kwamba utafuatia baada ya ule wa Nou Camp ulioboreshwa kwa ukubwa.
Bilionea Ratcliffe alisema: “Huu ni mwanzo wa safari njema kabisa inayovutia ya kuleta kila kitakachokuwa uwanja bora kabisa wa soka, ambao utajengwa kwenye eneo la Old Trafford.

“Uwanja wetu wa sasa umekuwa na kumbukumbu bora kabisa kwa miaka 115 iliyopita, lakini sasa haupo tena kwenye orodha ya viwanja bora kabisa vya michezo duniani.
“Kwa kujenga uwanja mpya kwenye eneo lililopo karibu na huu wa sasa, hii itafanya kulinga uwepo wa Old Trafford, wakati huo tukitengeneza uwanja wa kisasa kabisa utawapa mashabiki uzoefu mpya na utakuwa hatua chache tu kutoka kwenye uwanja wetu wa kihistoria.”

Uwanja huo mpya na miradi mingine ya kimaendeleo itakayoendelezwa pembezoni mwa uwanja huo itakuwa na uwezo wa kuingiza ziada ya Pauni 7.3 bilioni kwa mwaka kwenye uchumi wa Uingereza.
Uwanja huo utakuwa na miundombinu mingi ya usafiri, maeneo mbalimbali ya michezo, elimu, burudani na biashara. Serikali imetambua uwekezaji kama kipaumbele kikubwa kwa sasa.

Faida nyingine za kijamii katika uwekezaji huo ni kujenga makazi mapya zaidi ya 17,000, jambo ambalo litaongeza watalii milioni 1.8 kwa mwaka.
Na mpango huo wa kubadili eneo hilo litachangia kupatikana kwa kufsa zaidi ya 92,000 za ajira.
Kampuni ya uhandisi iliyochaguliwa kufanya dizaini ya uwanja huo bora kabisa inaitwa Foster + Partners. Kampuni hiyo inaongozwa na mshindi wa tuzo ya uhandisi, Lord Norman Foster, rafiki wa karibu wa bilionea Ratcliffe ambaye ndiye aliyehusika kufanya maboresho makubwa kwenye uwanja wa mazoezi wa Man United, Carrington.

Man United itatumia pesa zake kujenga uwanja huo, huku serikali itasimamia ujenzi wa miundombinu mingine ya pembezoni mwa uwanja huo, eneo ambalo litafahamika kama Trafford Park.
Sir Alex Ferguson ameunga mkono ujenzi huo wa Old Trafford akiamini kwamba jambo hilo litakuja kuleta matokeo kwa siku za baadaye.
Ferguson alisema: “Man United inapaswa kufanya vitu bora nje ndani, ikiwamo uwanja wa kuchezea. Old Trafford ina kumbukumbu nyingi sana kwangu binafsi. Lakini, lazima tukubali ukweli tunahitaji kujenga nyumba mpya ili kwenda sambamba na mambo ya sasa, huku tukiamini historia mpya itaandikwa.”
Na mhandishi Lord Sebastian Coe alifichua kwamba huo ni uongezaji mkubwa zaidi uliowahi kufanywa kwenye maeneo ya miji ya Uingereza tangu ule mradi wa London 2012.

Kwenye sehemu ya upembuzi yakinifu umehusisha maoni ya zaidi ya mashabiki 50,000 wa Man United wenye tiketi za msimu, wajumbe na wakurugenzi wa klabu hiyo ambao zaidi ya nusu wote wameunga mkono ujenzi wa uwanja mpya.
Kikosi kazi kinachosimamia ujenzi huo wa uwanja inamhusisha pia beki wa zamani wa Man United na nahodha wa miamba hiyo ya Old Trafford, Gary Neville, Meya wa Jiji la Manchester, Andy Burnham na kiongozi wa halimashauri ya Trafford, Sara Todd.