Vicheko vyatawala Liverpool, usajili wa 2024/25

Muktasari:
- Kwa mujibu wa tovuti ya Football Insider, Liverpool hadi sasa inaweza kutumia hadi Puni 154 milioni dirisha hili la usajili bila ya kuvunja sheria hiyo ya usawa wa matumizi ya pesa.
LIVERPOOL, ENGLAND: WAKATI timu kibao zikihaha kutaka kuuza baadhi ya wachezaji kabla ya Juni 30, ili kuendana na sheria za mapato na matumizi za Ligi Kuu England, mambo ni tofauti kwa Liverpool.
Kwa mujibu wa tovuti ya Football Insider, Liverpool hadi sasa inaweza kutumia hadi Puni 154 milioni dirisha hili la usajili bila ya kuvunja sheria hiyo ya usawa wa matumizi ya pesa.
Liverpool ambayo kwa sasa ipo chini ya kocha mpya, Arne Slot aliyejiunga nayo akitokea Feynoord , mbali ya kuwa na uwezo wa kutumia pesa hizo inaweza ikawa zaidi ya hapo ikiwa baadhi ya mastaa wanaodaiwa kuwa katika mpango wa kuondoka wataondoka.
Majogoo hawa kutoka Jiji la Liverpool wanaweza kuwauza mastaa wao Virgil van Dijk na Mohamed Salah ambao mikataba yao imebakisha mwaka mmoja kabla ya kuisha.
Wachezaji hawa wawili wanaweza kuwapa zaidi ya Pauni 100 milioni, hivyo itawafanya kuweza kusajili mastaa wapya kwa kutumia hadi Pauni 200 milioni.
Mbali ya Salah na van Dijk kuna uwezekano pia Liverpool ikamuuza Luis Diaz ambaye anawindwa na baadhi ya timu za Hispania ikiwemo Barcelona.
Kwa sababu mkataba wake unamalizika mwaka 2027, inawezekana akauzwa kwa pesa nyingi hivyo itazidi kuiweka Liverpool katika nafasi nzuri.
Hata hivyo, Liverpool haionekani kuwa na mpango wa kusajili sana katika dirisha hili ingawa inaweza ikafanya hivyo ikiwa itauza baadhi ya wachezaji wao muhimu.
Timu nyingi kwa sasa zimekuwa zikipambana kwa ajili ya kuuza walau wachezaji wawili kabla ya Juni 30, ambayo ndio tarehe ya mwisho ya kuweka mahesabu sawa ambayo inaitaka timu kutumia kwa mujibu wa vile ilivyoingiza na ikiwa itatumia zaidi ya kile ilichoingiza kiasi cha vitabu kuonyesha kuna hasara, adhabu ya kupokwa pointi inaweza kuikuta kama ilivyokuwa msimu uliopita kwa Everton.