Manchester United kupasuka mamilioni kisa mastaa wake

Muktasari:
- Mastaa kama Marcus Rashford na Antony wapo katika harakati za kutaka kuondoka lakini hadi sasa hakuna ofa rasmi iliyowasilishwa kwenda Man United kutoka timu zinazohusishwa nao.
MANCHESTER, ENGLAND: MANCHESTER United ipo katika hatari ya kutumia mamilioni kwa msimu ujao ili kuwaondoa katika timu wachezaji ambao haiwahitaji.
Mastaa kama Marcus Rashford na Antony wapo katika harakati za kutaka kuondoka lakini hadi sasa hakuna ofa rasmi iliyowasilishwa kwenda Man United kutoka timu zinazohusishwa nao.
Mbali ya Rashford na Antony, Jadon Sancho ambaye alitolewa kwa mkopo msimu uliopita, yeye pia anataka kuondoka kwani sio chaguo la kocha Ruben Amorim.
Alejandro Garnacho aliachwa kwenye kikosi cha kwanza kilichocheza fainali ya Europa League mwisho wa msimu uliopita na hivi karibuni alionekana amevaa jezi ya Aston Villa yenye jina la Rashford.
Hata hivyo, ili kuwauza au kuwatoa kwa mkopo mastaa hawa lazima kutakuwa na hasara kwa Man United kwani timu zinazowahitaji zinafahamu kwamba Man United inahitaji kuwandoa mastaa hao kwa udi na uvumba.
Garnacho, Rashford na Antony wana mikataba hadi 2028 na lama watandoka kwa mkopo katika dirisha hili Man United wanatarajiwa kugharamia mishahara yao kama ilivyo kawaida kwenye mikataba ya mikopo ambapo timu yenye mchezaji hutoa kidogo na ile timu anayokwenda hutoa kidogo pia.
Lakini kwa sasa Man United italazimika kutoa kiasi kikubwa zaidi cha pesa cha mshahara kwa sababu timu zinazowahitaji zinafahamu jinsi mashetani wekundu wanavyotaka sana kuwaachia wachezaji wao ili waweze kuweka sawa vitabu vyao.
Vilevile timu ambazo zinawahitaji mastaa hawa zinatarajiwa kuja na ofa ndogo zaidi kwani ni lazima Man United imetaka au haikutaka iwauzie kuliko kuendelea kusalia na mastaa hao ambao mishahara yao ni mikubwa.
Kuanzia kwa Rashford, Sancho na Antony hawa ni miongoni mwa mastaa wanaolipwa zaidi United.