Vardy amegoma kuzeeka Serie A
Muktasari:
- Vardy, 38, alijiunga na klabu hiyo ya Italia kama mchezaji huru dirisha lililopita la majira ya kiangazi baada ya kuhitimisha miaka 13 kwenye kikosi cha Leicester City.
MILAN, ITALIA: STRAIKA veterani, Jamie Vardy amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mwezi Novemba kwenye mikikimikiki ya Serie A kutokana na kiwango chake matata kabisa anachokionyesha huko Cremonese.
Vardy, 38, alijiunga na klabu hiyo ya Italia kama mchezaji huru dirisha lililopita la majira ya kiangazi baada ya kuhitimisha miaka 13 kwenye kikosi cha Leicester City.
Straika huyo alisaini mkataba wa mwaka mmoja kwenye klabu hiyo ya Serie A huku kikiwekwa kipengele cha kuongeza mwaka zaidi endapo kama timu hiyo itanusurika kushuka daraja. Na tangu alipotua kwenye timu hiyo, Vardy amekuwa moto chini ya Kocha Davide Nicola na amefunga mabao manne katika mechi 10 alizocheza katika michuano yote.
Sasa Vardy anakuwa Mwingereza wa kwanza kubeba tuzo hiyo ya mwezi huko Italia, akiwazidi wachezaji kama Paul Gascoigne, David Beckham na Paul Ince, ambao waliwahi kucheza kwenye ligi hiyo.
Vardy kiwango chake kimetambulika licha ya Cremonese, inayoshika nafasi ya tisa kwenye msimamo wa Serie A, ilipoteza mechi zote tatu ilizocheza Novemba, huku straika huyo akifunga bao lao pekee katika kichapo cha 2-1 dhidi ya Juventus.
Tuzo hiyo inatolewa kutokana na kura za mashabiki huku kwenye kinyang'anyiro hicho Vardy aliwabwaga staa wa AC Milan, Mike Maignan, mkali wa Inter Milan, Lautaro Martinez, nyota wa Napoli, David Neres, staa wa Genoa, Leo Ostigard na yule wa Udinese, Nicolo Zaniolo.
Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Serie A, Luigi De Siervo amesema: “Jamie Vardy ni mchezaji wa kweli kutoka kwenye zama nyingine.”
Vardy ameanzishwa katika mechi nane za mwisho za Cremonese na kufunga mabao mawili katika ushindi wa 3-1 dhidi ya Bologna, Desemba 1. Huko Leicester alikotoka, alifunga mabao 200 na asisti 71 katika mechi 500 alizochezea Leicester City, akiongoza kushinda mataji ya Ligi Kuu England, Kombe la FA na Ngao ya Jamii.