Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ronaldo amaliza safari ya Kombe la Dunia kwa majonzi, Hispania ikiweka rekodi

Muktasari:

  • Bao la dakika ya 90+1 lililofungwa na Mikel Merino lilitosha kuiondoa Ureno inayoongozwa na nahodha Cristiano Ronaldo na kuipeleka Hispania robo fainali huku ikiandika rekodi mpya katika historia ya Kombe la Dunia.

TIMU ya taifa ya Hispania imeendelea kuonyesha kwa nini ni miongoni mwa zinazopewa nafasi kubwa ya kutwaa Kombe la Dunia 2026 baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ureno katika mchezo wa hatua ya 16 bora uliochezwa Dallas, Marekani.

Bao la dakika ya 90+1 lililofungwa na Mikel Merino lilitosha kuiondoa Ureno inayoongozwa na nahodha Cristiano Ronaldo na kuipeleka Hispania robo fainali huku ikiandika rekodi mpya katika historia ya Kombe la Dunia.

Ushindi huo umeifanya Hispania kuwa timu ya kwanza kuwahi kucheza mechi sita mfululizo za Kombe la Dunia bila kuruhusu bao, ikiweka historia mpya ya mashindano hayo.

Mchezo ulianza kwa kasi huku Hispania ikitawala umiliki wa mpira. Mshambuliaji Mikel Oyarzabal, aliyekuwa tayari amefunga mabao manne kwenye mashindano hayo, alijaribu kufungua pazia mapema lakini shuti lake la mbali lilidhibitiwa kirahisi na kipa Diogo Costa.

Dakika chache baadaye Dani Olmo alimtengea nafasi nzuri Oyarzabal, lakini mshambuliaji huyo alipiga shuti lililokwenda nje ya lango.

Kwa upande wa Ureno, nahodha Cristiano Ronaldo naye alipata nafasi yake ya kwanza dakika ya 12, lakini alipiga kutoka pembeni ya eneo la hatari na kipa Unai Simón akaokoa bila shida.

Hispania iliendelea kushambulia kupitia Lamine Yamal na Álex Baena, lakini Diogo Costa aliendelea kuwa mwamba langoni kwa kuokoa mashambulizi kadhaa ya hatari.

Dakika ya 30, beki Pau Cubarsí alikaribia kuifungia Hispania baada ya kupokea pasi ya Pedri, lakini Costa aliokoa kwa kutumia mguu.

Ureno nayo ilijibu dakika ya 37 kupitia João Félix aliyemwandalia Ronaldo mpira ndani ya eneo la hatari, lakini nahodha huyo alipiga shuti lililodakwa na Simón.

Nafasi bora zaidi ya kipindi cha kwanza iliwakuta Wareno mwishoni mwa kipindi hicho baada ya mpira wa kona fupi kumkuta Nuno Mendes aliyepiga shuti kali lakini mpira ulimgonga beki Pedro Porro kabla ya kugonga mwamba na kutoka nje.

Kipindi cha pili kilianza kwa tahadhari kutoka kwa timu zote mbili huku nafasi za wazi zikiwa chache.

Pedri alijaribu bahati yake kwa shuti lililogongwa na mabeki na kutoka nje, kabla Álex Baena na Lamine Yamal nao kujaribu kumpima Costa bila mafanikio.

Kwa upande wa Ureno, Vitinha alitengeneza nafasi iliyomkuta Bruno Fernandes, lakini kiungo huyo akapiga mpira ulioishia kwenye nyavu za pembeni.

Kadiri dakika zilivyosonga ilionekana mchezo ungeingia muda wa nyongeza, lakini Hispania ilipata zawadi katika dakika ya kwanza ya muda wa nyongeza.

Ferran Torres alitoa pasi iliyomkuta Merino aliyekimbia kwa wakati sahihi kabla ya kuachia shuti la chini lililomshinda Diogo Costa na kuandika bao pekee la mchezo.

Ureno ilijaribu kusawazisha katika sekunde za mwisho lakini kichwa cha Bernardo Silva kilipaa juu ya lango na kuzima kabisa matumaini ya kurejea mchezoni.

Kwa ushindi huo, Hispania imefuzu robo fainali huku ikiendeleza rekodi yake bora ya kujilinda, wakati safari ya Cristiano Ronaldo katika Kombe la Dunia inaonekana kufikia tamati kwa majonzi, akiwa hajawahi kuvuka hatua ya nusu fainali zaidi ya mara moja katika maisha yake ya mashindano hayo.

Kiungo Rodri alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mechi baada ya kuiongoza Hispania kutawala eneo la kati na kudhibiti mchezo huo.