Ubelgiji yazima ndoto za Marekani, kuivaa Hispania robo fainali
Muktasari:
- Matokeo hayo yameipa tiketi Ubelgiji kufuzu hatua ya robo fainali ambayo sasa itakutana na Hispania katika mechi ya kuitafuta nusu fainali.
SEATTLE, MAREKANI: NDOTO za waandaaji wenza wa Kombe la Dunia 2026, Marekani zimezimwa mapema baada ya kuchapwa mabao 4-1 na Ubelgiji katika mechi ya hatua ya 16 bora iliyopigwa kwenye Uwanja wa Lumen Field mjini Seattle, Marekani.
Matokeo hayo yameipa tiketi Ubelgiji kufuzu hatua ya robo fainali ambayo sasa itakutana na Hispania katika mechi ya kuitafuta nusu fainali.
Ubelgiji ilianza mchezo kwa kasi na kufunga bao la mapema dakika ya tisa kupitia Charles De Ketelaere aliyemalizia vizuri shambulizi la kushtukiza na kuwatibulia mipango wenyeji.
Marekani ilionyesha uhai dakika ya 31 baada ya Malik Tillman kusawazisha bao hilo na kuamsha matumaini ya mashabiki, lakini furaha yao ilidumu kwa muda mfupi tu kwani dakika mbili baadaye De Ketelaere aliifungia Ubelgiji bao la pili na kuifanya timu hiyo kwenda mapumziko ikiwa inaongoza.
Ubelgiji iliendelea kutawala mchezo kipindi cha pili na dakika ya 57, Hans Vanaken akaandika bao la tatu lililozima kabisa ndoto za Marekani ya kuvuka hatua inayofuata baada ya kutumia vyema nafasi. Dakika 90, Romelu Lukaku akafunga bao la nne na kuifanya timu hiyo kumaliza mchezo kwa ushindi mnono.
Licha ya Marekani kufanya mabadiliko na kuongeza nguvu eneo la ushambuliaji katika dakika za mwisho, safu ya ulinzi ya Ubelgiji ilisimama imara huku kipa wake akihakikisha hakuna bao lingine lililopatikana hadi filimbi ya mwisho.
Ushindi huo unaifanya Ubelgiji kuendeleza safari yake katika michuano hiyo na sasa itakutana na Hispania, ambayo imetinga robo fainali baada ya kuiondoa Ureno kwa ushindi mwembamba wa bao 1-0 katika mchezo mwingine wa hatua ya 16 bora uliopigwa Julai 6, 2026.
Ubelgiji na Hispania zitakutana katika mchezo wa robo fainali utakaochezwa Julai 10, kwenye Uwanja wa Los Angeles (SoFi Stadium) kuisaka tiketi ya kutinga nusu fainali.
Hispania inaingia robo fainali ikiwa na historia kubwa katika Kombe la Dunia. Mabingwa hao wa mwaka 2010 wamewahi kuvuka hatua hiyo na kutwaa ubingwa, lakini tangu walipofanya hivyo waliishia hatua ya makundi mwaka 2014 na kutolewa katika hatua ya 16 bora mwaka 2018 na 2022.
Kufuzu robo fainali mwaka 2026 kunamaanisha La Roja imerudi kivingine katika hatua hiyo baada ya miaka 16.
Kwa upande wa Ubelgiji, bado inasaka taji lake la kwanza la Kombe la Dunia licha ya kuwa miongoni mwa mataifa yenye rekodi nzuri.
Mafanikio makubwa ya timu hiyo ni kumaliza nafasi ya tatu mwaka 2018, huku pia ikifika nusu fainali mwaka 1986. Sasa imetinga robo fainali ya Kombe la Dunia 2026 ikiwa na matumaini ya kuandika historia mpya.