Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

VAR ilivyoiminya Man United EPL

Muktasari:

  • Kiungo huyo wa kimataifa wa England, Barkley alifunga bao hilo la kusawazisha dakika ya 64 baada ya Man United kutangulia dakika ya 53 kwa bao la Casemiro.

MANCHESTER, ENGLAND: MASHABIKI wa Manchester United wamekasirishwa na kitendo cha teknolojia ya video inayomsaidia mwamuzi (VAR) kukubali bao la kusawazisha la Ross Barkley katika mchezo dhidi ya Aston Villa, Jumapili jioni.

Kiungo huyo wa kimataifa wa England, Barkley alifunga bao hilo la kusawazisha dakika ya 64 baada ya Man United kutangulia dakika ya 53 kwa bao la Casemiro.

Hata hivyo, licha ya ushindi mnono wa mabao 3-1 iliyoupata Mashetani hao wekundu, utata umeibuka kwa mashabiki kuchukizwa na VAR kukubali bao hilo licha ya mfungaji kuonekana wazi alikuwa ameotea.

Katika marudio ya picha ya bao hilo, ilionyesha Amadou Onana alikuwa eneo la kuotea huku akiwa amemzuia kipa wa Man United, Senne Lammens na kuukwepa mpira uliopigwa na mfungaji Barkley.

Licha ya mwamuzi kufanya marudio ya bao hilo, lilikubaliwa na ilionekana Onana hakumzuia kipa na kuugusa mpira uliokuwa ukienda golini.

Kutokana na utata huo hasa baada ya kituo cha matangazo uwanjani kuposti katika mtandao kuwa lilikuwa bao halali, mashabiki wa Man United waliushambulia ujumbe huo na kuona VAR iliwanyima haki na halikustahili kuwa bao.

Ujumbe ulisomeka; “Uamuzi wa mwamuzi wa kutoa bao ulikaguliwa na kuthibitishwa na VAR, Onana alikuwa kwenye nafasi ya kuotea, lakini hakuonekana kumzuia kipa wala kugusa mpira.”

Baada ya kuusoma ujumbe huo, mashabiki wa Man United waliandika katika mtandao huo;

Wa kwanza aliandika “Onana alikuwa mbele ya kipa akiwa ameotea na mpira ulimgusa.”

Mwingine alisema: “Onana mwenyewe alionyesha kuwa mpira ulimgusa...” huku wa tatu akiongeza: “Nina uhakika Onana aligusa mpira, lakini ni suala la tofauti ndogo sana... sina pingamizi kubwa bao kuhesabiwa.”

Wa nne aliandika: “(Mpira) hakuugusa Onana hakuna ushahidi wa moja kwa moja lakini kwa kusogeza mwili wake kuelekea au kuondoka kwenye mpira anamchanganya kipa, hiyo ni kuingilia mchezo na ni kuotea, siyo?”

Wa tano alisema: “Huu ni uamuzi mbaya sana. Hata kama mpira haumgusi Onana yuko moja kwa moja mbele ya kipa.”

Akizungumza na Sky Sports, mchambuzi wa soka, Gary Neville, alisema Onana huenda alikiri kugusa mpira baada ya bao kuhesabiwa.

Alisema: “Kuna hali inaonekana hapo, labda Onana. Je, anamzuia Lammens? Hilo lingekuwa. Lammens hana nafasi kwenye hili.

“Hakuna kabisa nafasi, shuti la Ross Barkley lilikuwa sahihi sana. Nafikiri ilikuwa vizuri, siamini kama hilo (bao) litaondolewa. Je, lilimgonga mgongoni, lilimgusa? Unawezaje kuona? Haiwezekani kujua kwa uhakika kama mpira ulimgusa Onana au la. Ulikuwa karibu sana naye, hilo ni wazi.

“VAR wanathibitisha. Tunawasikia wanatazama kama kulikuwa na mguso wowote kwa Onana. Hapo ndipo ilipofikia. Huwezi kuwa na uhakika kama mpira ulimgusa Onana, ila yeye pekee ndiye anajua, na ni vigumu akakubali.”

Katika mechi hiyo, Man United ilionyesha kiwango safi ikiongozwa na safu ya ushambuliaji iliyokuwa na Amad Diallo, Matheus Cunha na Bryan Mbeumo, huku Bruno Fernandes akiwa katika kiwango bora kabisa akicheza nyuma yao.

Washambuliaji hao waliisumbua safu ya beki ya Villa na United ilipata bao la kwanza la Casemiro kabla ya shangwe hiyo kutibuliwa na Barkley.

United iliongeza mabao yake yakifungwa na Cunha na Benjamin Sesko aliyetokea benchi na kufunga la tatu.

Manchester United sasa ipo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikiwa na tofauti ya pointi tatu dhidi ya Aston Villa.

United sasa itaifuata Bournemouth Ijumaa usiku kabla ya mapumziko ya mechi za kimataifa.

Hata hivyo, inakabiliwa na mchezo mgumu dhidi ya Leeds United ambao inapambana kuepuka kushuka daraja, kisha itaifuata Chelsea.

Pia bado ina kibarua kigumu dhidi ya Liverpool kabla ya msimu kumalizika ikiwa inataka kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.