Van Dijk: Hali haikuwa nzuri Liverpool, niliitisha kikao cha wachezaji
Muktasari:
- Beki huyo raia wa Uholanzi, amefichua kuwa, yeye ndiye aliyeitisha kikao hicho cha wachezaji ambacho kocha Arne Slot hakuhudhuria kufuatia kichapo cha mabao 2-1 kilichotolewa na Manchester United mwishoni mwa wiki iliyopita, ikiwa ni kipigo cha nne mfululizo kwa Liverpool msimu huu.
Imefahamika kuwa, beki na nahodha wa Liverpool, Virgil Van Dijk, aliitisha mkutano wa wazi wa wachezaji wenzake, ili kuzungumzia masuala mbalimbali ya timu hiyo, ambayo ilipitia changamoto za kukosa matokeo mazuri, kabla ya ushindi dhidi ya Eintracht Frankfurt, Jumatano Oktoba 22, 2025.
Beki huyo raia wa Uholanzi, amefichua kuwa, yeye ndiye aliyeitisha kikao hicho cha wachezaji ambacho kocha Arne Slot hakuhudhuria kufuatia kichapo cha mabao 2-1 kilichotolewa na Manchester United mwishoni mwa wiki iliyopita, ikiwa ni kipigo cha nne mfululizo kwa Liverpool msimu huu.
Van Dijk anaamini mazungumzo hayo yalichangia ushindi mnono wa mabao 5-1 dhidi ya Eintracht Frankfurt iliyokuwa nyumbani nchini Ujerumani, kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Amesema kabla ya hapo, hali haikuwa nzuri, kwani kila mchezaji hakuwa na furaha na huenda suala hilo lilichangia matokeo ambayo yaliwakabili, lakini aliona kuna haja ya kukutana kwa pamoja kama wachezaji, ili kupeana moyo wa kupambana.
“Hali haikuwa nzuri kabisa kambini, kila mchezaji alionekana kukata tamaa, ninaamini hilo lilichangia kwa kiasi kikubwa kupata matokeo ambayo hayakuwa mazuri kwetu, niliona kuna haja ya kuitana, na nilifanya hivyo kama kiongozi wa wachezaji wote wa Liverpool kwa sasa, nashukuru nimefanikiwa kwa hilo.
“Baada ya mechi dhidi ya Man United, kila mchezaji alifadhaika, nilichokifanya ni kuhakikisha tunarudi kwenye hali ya kuwa tayari kupambana kabla ya mechi ya Ulaya dhidi ya Eintracht Frankfurt, tuliambiama ukweli na kila mmoja wetu alikubali tumekosea na tuna haja ya kurekebisha mambo kwa kupata matokeo mazuri,” amesema beki huyo mwenye miaka 34.
Kuelekea mechi ya Ligi ya EPL dhidi ya Brentford itakayochezwa kesho usiku, Van Dijk ameongeza: “Tulifanya tathmini ya kina na kocha wetu Slot, tumejipanga vizuri na ninaamini tutapata matokeo yatakayowafurahisha mashabiki wote wa Liverpool.
“Tunafahamu haitakuwa mechi rahisi, lakini mipango yetu itatuwezesha kupambana na kupata matokeo yatakayoturudisha kwenye mstari kwenye mechi ya Ligi ya EPL!”