Kocha Liverpool bado anamtetea Wirtz
Muktasari:
- Staa huyo wa Ujerumani, Wirtz alianzia benchini katika mechi dhidi ya Manchester United kwenye mikikimikiki ya Ligi Kuu England, Jumapili iliyopita.
LIVERPOOL, ENGLAND: KOCHA wa Liverpool, Arne Slot amemtetea kiungo wake ghali Florian Wirtz baada ya kushambuliwa sana kutokana na kuanza maisha yake Anfield kwa kasi hafifu.
Staa huyo wa Ujerumani, Wirtz alianzia benchini katika mechi dhidi ya Manchester United kwenye mikikimikiki ya Ligi Kuu England, Jumapili iliyopita.
Liverpool ilipambana na kuibwaga Bayern Munich kwenye mchakato wa kunasa saini ya Wirtz na hivyo kulipa ada ya Pauni 116 milioni kumpata staa huyo akitokea Bayer Leverkusen, ambako alikuwa matata kwelikweli kwenye Bundesliga.
Hata hivyo, tangu alipojiunga na Liverpool, staa huyo hajahusika kwenye bao lolote licha ya kuitumikia miamba hiyo ya Anfield kwenye mechi tisa.
Slot anaamini Wirtz ugumu alianza nao kwenye maisha yake huko Liverpool ni kutokana na ugenini kwenye ligi na ni suala la muda tu.
Slot amesema: "Unapochukuliwa kwa pesa nyingi, watu wanachokitazama zaidi ni mabao na asisti, lakini ninachoweza kukisema, angekuwa na asisti sita au saba hadi sasa. Ukitazama kwenye pasi, amekuwa akipiga bahati mbaya kwake halikupatikana bao, mfano mmoja mzuri kwenye ile mechi ya Chelsea na alimtengenezea nafasi nzuri sana Mo Salah."
Maelezo hayo ya Slot yameungwa mkono na nahodha wa Liverpool, Virgil van Dijk, ambaye anafahamu presha ilivyo pindi mchezaji anaposajiliwa kwa pesa nyingi. Van Dijk alijiunga na Liverpool kwa ada ya Pauni 75 milioni kwenye dirisha la Januari 2018 na sasa amekuwa na mchango mkubwa katika kikosi hicho cha Anfield.
Kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi, Liverpool ilitumia pesa nyingi pia ikimsajili straika Alexander Isak kwa ada iliyovunja rekodi Uingereza ya Pauni 130 milioni. Wachezaji wengine waliosajiliwa ni dirisha hili ni Hugo Ekitike na Milos Kerkez.