Arbeloa aula Fulham
Muktasari:
- Arbeloa, mwenye umri wa miaka 43 na aliyekuwa kocha wa Real Madrid, alisema anajivunia kupewa nafasi ya kuiongoza Fulham, akieleza kuwa ni hatua muhimu katika maisha yake ya ukocha.
LONDON, England: KLABU ya Fulham imemtangaza rasmi Alvaro Arbeloa kuwa kocha wake mpya kwa mkataba wa miaka mitatu, akichukua nafasi ya Marco Silva ambaye ameondoka kujiunga na Benfica ya Ureno.
Arbeloa, mwenye umri wa miaka 43 na aliyekuwa kocha wa Real Madrid, alisema anajivunia kupewa nafasi ya kuiongoza Fulham, akieleza kuwa ni hatua muhimu katika maisha yake ya ukocha.
"Ni heshima kubwa kwangu kuanza hatua hii mpya Fulham, klabu kongwe zaidi jijini London. Ninahisi wajibu mkubwa na ninawashukuru mwenyekiti Shahid Khan pamoja na makamu mwenyekiti Tony Khan kwa kuniamini na kunikabidhi jukumu hili katika Ligi Kuu England," alisema Arbeloa.
Mwenyekiti wa Fulham, Shahid Khan, alisema Arbeloa ni kocha mwenye malengo makubwa na anaamini uzoefu wake katika moja ya klabu kubwa duniani utainufaisha Fulham.
"Alvaro ni mtu mwenye ndoto na malengo makubwa. Amefanya kazi akiwa karibu na baadhi ya wachezaji bora, klabu kubwa na mifumo bora ya soka duniani. Tunaamini uzoefu huo utakuwa na manufaa makubwa kwa Fulham," alisema Khan.
Aliongeza kuwa amefurahishwa na msisitizo wa Arbeloa wa kuwapa nafasi wachezaji chipukizi kutoka akademi pamoja na falsafa yake ya kucheza soka la kushambulia.
Arbeloa alipata uungwaji mkono mkubwa katika mchakato wa ajira hiyo kupitia mapendekezo mazuri kutoka kwa rais wa Real Madrid, Florentino Perez, pamoja na kocha mpya wa klabu hiyo, Jose Mourinho, ambaye aliwahi kufanya kazi naye katika Uwanja wa Santiago Bernabeu.
Kocha huyo aliondoka Real Madrid mwishoni mwa msimu uliopita baada ya kuinoa timu kwa muda tangu Januari kufuatia kuondoka kwa Xabi Alonso. Katika kipindi hicho, aliiongoza Madrid katika mechi 28 za mwisho za msimu, ikipeleka kumaliza nafasi ya pili katika La Liga huku ikitolewa na Bayern Munich katika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Arbeloa anarithi mikoba ya Marco Silva, ambaye aliamua kujiunga na Benfica licha ya Fulham kumwekea mezani ofa ya kuongeza mkataba.
Makamu mwenyekiti wa Fulham, Tony Khan, alisema mwezi uliopita kuwa Silva awali alikuwa ameonyesha nia ya kuendelea kubaki klabuni, lakini baadaye alibadili msimamo wake na kuishangaza bodi kwa kuondoka baada ya kuitumikia Fulham kwa mafanikio kwa kipindi cha miaka mitano.
Kabla ya Arbeloa kuteuliwa, makocha Thomas Frank na Kieran McKenna walikuwa wakitajwa kuwania nafasi hiyo. Hata hivyo, McKenna alionekana kuwa ghali kutokana na gharama za ada ya kuvunja mkataba wake, mshahara na gharama za benchi lake la ufundi.
Arbeloa sasa anatarajiwa kuanza ujenzi wa kikosi chake, huku akitajwa kuwa na nia ya kuwasajili baadhi ya wachezaji aliokuwa akifanya nao kazi Real Madrid, akiwemo kiungo mshambuliaji Franco Mastantuono, beki wa kushoto Fran Garcia na mshambuliaji Gonzalo Garcia.