Utamu wa Top Six, ukizubaa umeachwa

LONDON, ENGLAND. LIGI Kuu England imekuwa na msisimiko hasa baada ya mechi za katikati ya wiki kuchezwa.

Kwa mujibu wa Mirror Arsenal, Liverpool, Aston Villa na Manchester City ndizo timu ambazo zinatajwa kuwa kwenye mbio za kuwania ubingwa hadi sasa, lakini ratiba ya mechi zao zijazo, zitaamua jambo.

Arsenal imejikita kileleni baada ya kukusanya pointi 39 baada ya ushindi wa mabao 4-3 dhidi ya Luton City, usiku wa Jumanne iliyopita.

Kikosi hicho cha Kocha Mikel Arteta kimeweka pengo la pointi mbili kileleni dhidi ya Liverpool, ambayo nayo inaonekana kuwa moto kwelikweli kwa siku za karibuni chini ya kocha wake Jurgen Klopp.

Liverpool iliichapa Sheffield United na kujikita kwenye nafasi ya pili na pointi zake 34, huku Aston Villa ikiwashangaza wengi, baada ya kukamatia nafasi ya tatu, kufuatia ushindi dhidi ya Man City, ambayo imeshuka hadi kwenye nafasi ya nne.

Aston Villa chini ya Kocha Unai Emery imekusanya pointi 32, wakati Man City ya Pep Guardiola ina pointi 30, sita nyuma ya vinara Arsenal.

Tottenham Hotspur baada ya kichapo kutoka kwa West Ham United imebaki na pointi 27, zinaifanya iendelee kubaki kwenye nafasi ya tano, ikiwa imelingana pointi na Manchester United, inayoshika nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi hiyo, baada ya mechi 15.

Man United na Spurs zipo pointi tatu nyuma kuifikia timu iliyopo kwenye Top Four, huku zikiwa zimeachwa kwa pointi tisa na vinara, Arsenal.

Kutokana na tofauti ya pointi chache zinazofanya timu hizo sita za juu kwenye msimamo wa ligi kutofautiana, mabadiliko mengi zaidi yanaweza kutokea kutokana na ratiba ngumu inayokabili timu hizo kuanzia sasa.

Mchoro wa ratiba ulivyo kwa kila timu, ambayo itaweza kupambana na kupata matokeo chanya kwenye mechi tano zijazo, basi itakuwa imejiweka kwenye nafasi nzuri zaidi ya kushindania ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu.

Arsenal inapambana kuhakikisha inaepuka kilichoikuta msimu uliopita wakati ilipoongoza ligi kwa muda mrefu kabla ya kupigwa kikumbo na Man City na hatimaye ubingwa kunyakuliwa na wakali hao wa Etihad.

Kocha Arteta na kikosi chake cha Arsenal wanasaka ubingwa wao wa kwanza wa ligi, ambapo mara ya mwisho walinyakua 2003/04, walipocheza bila ya kupoteza mchezo wowote kwenye ligi hiyo kwa msimu mzima.Mchakamchaka huo wa ratiba ngumu kwa kila timu utaanza leo, Jumamosi na hadi kufikia Krismasi na Mwaka Mpya, kila kitu kitakuwa kimefahamika kwenye mbio hizo za kusaka ubingwa wa England.

Kwa namna ratiba ya kila timu hizo sita ilivyo, timu itakayozubaa tu, basi imewekwa kando kwenye mchakamchaka huo wa kufukia taji la Ligi Kuu.

Arsenal itaanzia huko Villa Park kukipiga na Aston Villa, inayonolewa na kocha wao wa zamani, Emery, huku Liverpool itaanza na kibarua cha kuikabili Crystal Palace huko Selhurst Park, huku Man City ikiwa na shughuli na Luton, Spurs itakuwa na kasheshe la kupambana na Newcastle na Man United itakabiliana na Bournemouth huko Old Trafford. Ngoja tuone.