Utabiri wa Opta wazua mjadala AFCON 2025
Muktasari:
- Utabiri huo uliwakasirisha mashabiki wa Misri. Opta ilitegemea akili mnemba (AI) na uchambuzi wa takwimu katika kutoa makadirio yake, sambamba na mashindano kufikia hatua ya nusu fainali. Mifumo ya kidijitali ilionyesha kuwa Morocco, wenyeji wa mashindano, na Senegal wana nafasi kubwa zaidi ikilinganishwa na timu nyingine zilizofuzu.
RABAT, MOROCCO: UTABIRI uliotolewa na mtandao wa kimataifa wa takwimu Opta Jumapili jioni umezua mjadala na mabishano makubwa kabla ya mechi za nusu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), baada ya kuzipa timu za taifa za Senegal na Morocco nafasi kubwa ya kufika fainali.
Utabiri huo uliwakasirisha mashabiki wa Misri. Opta ilitegemea akili mnemba (AI) na uchambuzi wa takwimu katika kutoa makadirio yake, sambamba na mashindano kufikia hatua ya nusu fainali. Mifumo ya kidijitali ilionyesha kuwa Morocco, wenyeji wa mashindano, na Senegal wana nafasi kubwa zaidi ikilinganishwa na timu nyingine zilizofuzu.
Timu ya taifa ya Misri ilikata tiketi ya nusu fainali baada ya ushindi wa kusisimua wa mabao 3-2 dhidi ya mabingwa watetezi Ivory Coast, katika mechi ya mwisho ya robo fainali, na sasa itakutana na Senegal, waliowashinda Mali 1-0 kwa tabu.
Morocco ilifika hatua hiyo baada ya ushindi wa kuridhisha wa mabao 2-0 dhidi ya Cameroon, huku Nigeria wakifuzu baada ya kuifunga Algeria 2-0, hivyo kukamilisha orodha ya timu nne zinazowania ubingwa.
Kwa mujibu wa utabiri wa Opta, Morocco ina nafasi ya asilimia 57.15 ya kuifunga Nigeria na kufuzu fainali, wakinufaika na uthabiti wa kiufundi chini ya kocha Walid Regragui, mwendelezo mzuri wa matokeo yao katika mashindano, pamoja na mchango wa wachezaji wao nyota, akiwamo Achraf Hakimi.
Kwa upande mwingine, nafasi za Nigeria hazijaondolewa kabisa, kwani wana uwezekano wa asilimia 42.85 wa kufuzu, kutokana na safu yao kali ya ushambuliaji inayoongozwa na Victor Osimhen, mfungaji bora wa timu hiyo na mmoja wa wachezaji waliovutia zaidi kwenye mashindano.
Katika nusu fainali ya pili, takwimu zinaipa Senegal nafasi ya asilimia 55.13 kufika fainali, ikilinganishwa na 44.87 kwa Misri, wakiongozwa na nahodha wao na nyota wa Liverpool, Mohamed Salah.
Utabiri huo umejikita kwenye ubora wa Senegal katika mikutano ya ana kwa ana dhidi ya Misri katika miaka ya karibuni, ambapo Simba wa Teranga waliwafunga Mafarao kwa mikwaju ya penalti katika fainali ya AFCON ya mwaka 2022, kabla ya kurudia mafanikio hayo katika mechi za kufuzu Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar.