Utaamua unarudi tena Ulaya
Muktasari:
- Kwenye Ligi Kuu England, kasheshe litaanzia huko City Ground, wakati Nottingham Forest itakapokabiliana na Chelsea. Ni mechi ya kibabe, huku rekodi zikionyesha miamba hiyo imekutana mara 16 kwenye ligi, The Blues ikishinda sita na Forest nne.
LONDON, ENGLAND: LIGI Kuu za Ulaya zinarejea baada ya kupisha mikikimikiki ya mechi za kimataifa, huku mashabiki wakitarajia kuona kasheshe zito zitakalotokea kwenye Ligi Kuu England, La Liga, Bundesliga, Serie A na Ligue 1. Mambo ni moto.
Kwenye Ligi Kuu England, kasheshe litaanzia huko City Ground, wakati Nottingham Forest itakapokabiliana na Chelsea. Ni mechi ya kibabe, huku rekodi zikionyesha miamba hiyo imekutana mara 16 kwenye ligi, The Blues ikishinda sita na Forest nne.
Chelsea imeshinda mara nyingi ugenini kuliko nyumbani kwenye mechi dhidi ya Forest, ikifanya hivyo mara nne. Je, itashinda tena?
Mechi hiyo itapigwa Jumamosi hii, ambapo pia kutakuwa na purukushani za Brighton kucheza na Newcastle United, Burnley na Leeds United, Crystal Palace na Bournemouth, Sunderland na Wolves, wakati Manchester City itamalizana na Everton ya kocha David Moyes. Rekodi ya Man City na Everton, kwenye Ligi Kuu England zimekutana mara 56, ambapo sare ni 11, tu huku Man City ikishinda 27, mara 15 uwanjani Etihad, huku Everton imeshinda 18, mara saba tu ndiyo ilifanya hivyo kwenye uwanja wa ugenini huko Etihad.
Kutakuwa na London derby pia, wakati Fulham itakapokuwa nyumbani kucheza na Arsenal, ambapo rekodi za miamba zinasoma kwenye mechi ilizokutana kwenye ligi ni mara 36, sare ni nane, huku Arsenal ikiwa imetawala, ikishinda 24, mara 12 ugenini na Fulham imeshinda nne tu, zote ilipocheza Craven Cottage.
Jumapili zitapigwa mechi mbili, zote kali, lakini macho na masikio ya wengi yataelekezwa huko Anfield, ambapo Liverpool itakabiliana na Manchester United.
Rekodi za mahasimu hao ni kwamba wamekutana mara 66 kwenye mechi za Ligi Kuu England, sare ni 17, huku Liverpool ikishinda 20, mara 12 nyumbani na Man United imeshinda 29, mara 12 kwenye Uwanja wa Anfield.
Mechi nyingine itashuhudiwa Tottenham Hotspur ikikipiga na Aston Villa, wakati Jumatatu kutakuwa na mechi moja, ambapo West Ham itacheza na Brentford.
Kwenye La Liga, Sevilla itakipiga na Mallorca kwenye mechi za Jumamosi, ambapo zitashuhudia pia Barcelona ikicheza na Girona, Villarreal na Real Betis na Atletico Madrid ikicheza na Osasuna. Jumapili, zitachezwa mechi nne tu, ambapo Elche itamaliza ubishi na Athletic Bilbao, wakati Celta Vigo itacheza na Real Sociedad, Levante na Rayo Vallecano, huku Real Madrid itakuwa ugenini kucheza na Getafe.
Bundesliga, FC Cologne itacheza na Augsburg, FC Heidenheim na Werder Bremen, Mainz 05 na Bayer Leverkusen, RB Leipzig na Hamburger SV, Wolfsburg na VfB Stuttgart na Bayern Munich itakuwa na kasheshe zito la kukabiliana na Borussia Dortmund katika Dabi ya Ujerumani maarufu kama ‘Der Klassiker’. Mechi mbili zitachezwa Jumapili huko kwenye Bundesliga, ambapo Freiburg itacheza na Eintracht Frankfurt na St Pauli itacheza na Hoffenheim.
Kwenye Serie A, Lecce itacheza na Sassuolo, Pisa na Hellas Verona, wakati Torino itamaliza ubishi na Napoli na AS Roma ni vuta nikuvute dhidi ya Inter Milan. Mechi hizo za kibabe zitapigwa Jumamosi, wakati Jumapili kutakuwa na mechi tano, ambapo Como 1907 itacheza na Juventus, Cagliari na Bologna, Genoe na Parma, Atalanta na Lazio, huku AC Milan ikipima ubavu na Fiorentina.
Huko kwenye Ligue 1, Nice patachimbika na Lyon, wakati Angers itatesti mitambo yake na AS Monaco, huko Marseille ikiwa na shughuli pevu mbele ya Le Havre.
Kasheshe la Ligue 1 kwa Jumapili, Lens itacheza na Paris FC, Lorient na Brest, Rennes na Auxere, Toulouse na Metz na Nantes itakipiga na Lille.